Magazetini
21 Januari 2010Chama cha Demokratik cha rais Barack Obama kimepoteza kiti cha seneti katika jimbo la Massachusetts ambalo hadi sasa lilikuwa ngome thabiti ya chama hicho nchini Marekani. Jee kupoteza kiti hicho kuna maana gani kwa rais Obama.?
Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanatoa maoni yao.
Gazeti la Frankfurter Rundschau linasema matokeo ya uchaguzi katika jimbo la Massachusetts ni maafa kwa rais Obama. Mhariri wa gazeti hilo anasema ikiwa chama cha rais Obama kimepoteza kiti katika jimbo ambalo hadi sasa lilikuwa ngome ya chama hicho, hiyo ni ishara kwamba chama hicho kimo katika hatari ya kupigwa radi katika uchanguzi wa bunge utakaofanyika baadae mwaka huu nchini Marekani.
Mhariri wa gazeti la Frankfurter Allgemeine anaeleza wazi juu ya kushindwa kwa chama cha rais Obama katika uchaguzi wa seneti kwenye jimbo la Massachusetts:
Kuchaguliwa kwa mjumbe wa chama cha Republican kuwa seneta wa jimbo la Massachusetts , lililokuwamo mnamo mikono ya akina Kennedy kwa dahari za miaka, kutagubika siasa za Marekani na za rais Obama. Mhariri wa gazeti hilo anasema matokeo ya uchaguzi huo ni tetemeko la ardhi la kisiasa nchini Marekani.
Gazeti hilo pia linatilia maanani kwamba chama cha Obama kilipoteza kiti hicho jana, siku ambapo aliadhimisha muda wa mwaka mmoja tokea aingie madarakani.
Maana ya kupoteza kiti hicho ni kwamba chama cha Demokratik sasa kimepoteza wingi wake katika seneti.
Gazeti la Märkische Oderzeitung linasema
ushindi wa mjumbe wa chama cha
Republican katika jimbo la Massachusetts ni
pigo kubwa kwa wananchi milioni 45 wa
Marekani wasiokuwa na bima ya afya.
Na gazeti la Wetzlarer linakubaliana na tathmini hiyo kwa kusema kwamba watu wa jimbo la Massachusetts wametumia vikaratasi kuupinga mpango wa rais Obama wa kuleta mageuzi katika mfumo wa afya. Gazeti hilo linasema chama Demokratic hakikupoteza tu, ngome yake kuu, bali pia kimepoteza wingi wake katika seneti.
Ndiyo kusema, mhariri wa gazeti hilo anaeleza, sasa kuna hatari ya kushindikana kwa mpango wa rais Obama wa kuleta mageuzi katika mfumo wa afya.
Na gazeti la Thüringische Landeszeitung
linatathmini ifuatavyo matokeo ya uchaguzi
katika jimbo la Massachusetts:
"Yumkini watu katika sehemu zingine za
dunia wanashindwa kuelewa kwa nini
Wamarekani wengi wanaipinga bima ya
afya itakayotolewa na serikali.
Lakini msimamo wa watu hao una maana gani kwetu?" Gazeti la Thüringische Landeszeitung linafafanua kwa kusema, ikiwa rais Obama anashindwa nchini mwake kuchukua hatua zilizopaswa kuchukuliwa siku nyingi, ni hatua gani atakazoweza kuzichukua katika medani ya kimataifa-yeye kama rais mwenye nguvu.?
Mwandishi Mtullya Abdu/Duetsche Zeitungen.
Mhariri: Miraji Othman