Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani. | Magazetini | DW | 06.01.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani.

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanasema Obama hajasema vipi atang'oa mizizi ya ugaidi.

Rais Barack Obama akifafanua hoja juu ya suala la ugaidi.

Rais Barack Obama akifafanua hoja juu ya suala la ugaidi.

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanatoa maoni yao juu ya rais Obama, ugaidi, na juu ya hali ya ajira nchini Ujerumani.

Gazeti la Osnabrücker linakumbusha kwamba katika mwaka 2008 takriban kila suala lilifungamanishwa na kuondoka madarakani kwa rais George Bush ambae hakuwa maaruf duniani. Kuondoka kwake pia kulifungamanishwa na uwezekano wa kumalizika kwa ugaidi.


Gazeti hilo linasema matumaini hayo yalitiwa rutuba na uamuzi wa kumpa rais Barack Obama tuzo ya amani ya Nobel.Lakini mhariri wa gazeti la Osnabrücker anatamka kuwa hali halisi ni nyingine.

Anaeleza kuwa magaidi wa Al-Qaeda bado wanaendelea kuangamiza watu.Idadi kubwa ya vifo nchini Afghanistan vya askari wa Marekani na wa nchi nyingine za Nato, pamoja na jaribio la shambulio la kigaidi nchini Marekani; hayo yamewafanya watu watambue hali halisi ambayo siyo ya kufurahisha.

Gazeti Osnabrücker linatilia maanani kwamba, nchini Marekani pia, ghafla umezuka mjadala mkali juu ya njia za kupambana na ugaidi na juu ya suala la Afghanistan.

Gazeti hilo linasema pamoja na kuongeza idadi ya wanajeshi mara tatu nchini Afghanistan, rais Obama sasa anazungumza kama George Bush. Sasa anazungumzia juu ya vita dhidi ya mtandao wa kigaidi. Lakini mhariri wa gazeti la Osnabrücker anatilia maanani kwamba rais huyo bado hajatoa jawabu thabiti ,kujibu swali,vipi ataweza kupambana na mizizi ya ugaidi.

Gazeti la Rheinische Post leo linazungumzia juu ya uamuzi wa Kansela Angela Merkel wa Ujerumani wa kuunda kamati ya baraza la mawaziri itakayoshughulikia suala la Afghanistan.

Gazeti hilo linasema hatua hiyo inathibitisha kwamba kiongozi huyo wa Ujerumani ameliweka suala la Afghanistan moyoni. Gazeti hilo pia linatilia maanani kwamba Kansela Merkel ameunda kamati hiyo ya watu wenye utaalamu, watakaotayarisha mwongozo wa pamoja, kabla ya kufanyika mjini London, kwa mkutano wa kimataifa juu ya Afghanistan.

Gazeti la General -Anzeiger limenukuu usemi wa mtaalamu Robert Baden Powel aliesema "jitayarisheni".

Gazeti hilo limenukuu usemi huo kuhusiana na hali ya ajira nchini Ujerumani. Gazeti limeeleza kuwa watu nchini Ujerumani walijitayarisha kuona idadi ya wasiokuwa na ajira ikipanda hadi kufikia milioni nne na laki moja. Lakini gazeti linasema hali hiyo haijatokea.

Mhariri wa gazeti la Landeszeitung anaunga mkono kwa kusema kwamba hakuna alietarajia kuona ukakamavu huo katika soko la ajira katika mazingira ya mgogoro mkubwa wa uchumi.

Hatahivyo, mhariri wa gazeti hilo anaelezea msingi wa ukakamavu huo- Idara kuu ya ajira ilitenga kiasi cha Euro bilioni 5 kwa ajili ya kulipa mishahara ya watu wanaofanya kazi kwa saa pungufu. ....

Mwandishi/Mttullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Othman, Miraji