Maoni ya Christina Bergmann | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.01.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Maoni ya Christina Bergmann

Rais Barack Obama wa Marekani amechukua hatua ya kwanza juu ya kuifunga jela ya Guantanamo.

default

Mwisho wa jela ya Guantanamo unakaribia?

Rais Barack Obama wa Marekani ametoa agizo la kuifunga jela ya kijeshi ya Guantanamo katika muda wa miezi 12 ijayo ijayo.

Rais Obama amepania. Mapema kabisa alipokuwa anagombea urais,aliahidi kuifunga jela hiyo ya kijeshi .Na aliitekeleza ahadi hiyo siku ya pili tu baada ya kuingia Ikulu.Ni hatua iliyokuwa inasubiriwa na dunia nzima. Hakuna maneno yanayoweza kuelezea umuhimu wa ishara ya hatua hiyo.

Jela ya Guantanamo, inawakilisha kinyume cha siasa,haki na sheria za Marekani sawa na kukiukwa haki za binadamu kulikotendeka katika jela ya Abu Ghraib nchini Irak, chini ya usimamizi wa Marekani. Mbele ya macho ya watu duniani, Marekani imepoteza uadilifu ,kutokana na jela ya Guantanamo.Watu wenye siasa kali waliitumia jela hiyo kwa lengo la kuchochea chuki .Ndiyo sababu kwamba kuondolewa kwa jela ya Guantanamo pia kutakuwa hatua ya kupambana na ugaidi.

Rais Obama alisema katika siku yake ya kwanza Ikulu, kwamba uamuzi wa kuifunga Guantanamo maana yake ni kurejea kwa Marekani katika mkondo wa kutekeleza sheria.

Uamuzi wa kusimamisha kwa muda kesi zote, kuchunguza njia zilizotumika katika kuwatia mbaroni watuhumiwa 245 waliopo katika jela hiyo, na kupiga marufuku matendo ya utesaji hata kwa maafisa wa ujasusi, sambamba na kuchunguza vigezo vyote viliyvotumika na jeshi la Marekani na idara za ujasusi- hatua zote hizo zinathibitisha dhamira ya Marekani ya kurejea katika sheria zinazotambuliwa kimataifa.

Hatahivyo inafaa kutambua kwamba maagizo hayo yote ni mwanzo tu wa mchakato mrefu na mgumu.Kufungwa kwa jela ya Guantanamo hakutafanyika mara moja-watu asilani wasijihadae juu ya hayo! Katika jela hiyo bado wapo watu waliotenda uhalifu mkubwa.Kwa hiyo haitawezekana kuwaachia huru tu, watu kama hao. Mahakama yoyote ya kiraia itakataa ushahidi unaotokana na mazingira ya jela ya Guantanamo. Rais Obama amezingatia hayo yote na ndiyo sababu amefanya upambanuzi katika maagizo aliyotoa.Pia ameteua jopo litakalowashughulikia wafungwa- jee kitatokea nini kwa watu hao?

Rais Obama ametoa muda wa mwaka mmoja kwa wanasheria wake, wanajeshi na wanadiplomasia ili waweze kutatua matatizo mengi. Kwa mfano pana matatizo yanayohusu hatima ya kundi la waiguri-watu 17 kutoka China wasiokuwa na hatia yoyote, lakini hawawezi kurudi nyumbani China, kwa sababu huenda wakateswa iwapo watarejea.

Sasa ni zamu ya nchi ambazo kwa muda wa miaka mingi zimekuwa zinataka kufungwa kwa jela ya Guantanamo.Kwenye mkutano wao mjini Brussels wiki ijayo,mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya yumkini wataunga mkono mabadiliko katika siasa ya Marekani. Umoja wa Ulaya utapaswa kutoa ishara, kuonesha kuwa nazo zina wajibu wa kutimiza. Mapambano dhidi ya ugaidi yanahitaji juhudi za pamoja. Obama ameshachukua hatua ya kwanza muhimu.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com