Maoni: Ulaya ithamini mafanikio ya umoja | Matukio ya Kisiasa | DW | 26.05.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Maoni: Ulaya ithamini mafanikio ya umoja

Uchaguzi wa Bunge la Ulaya umedhihirisha kitu kwamba vyama vinavyopinga Umoja wa Ulaya na kuchukia wageni vinazidi kuja juu, lakini Christoph Hasselbach anasema Ulaya inapaswa kujifunza kuyathmini mafanikio ya Umoja huo.

Christoph Hasselbach wa Dawati la DW, Ulaya.

Christoph Hasselbach wa Dawati la DW, Ulaya.

Hakuna anayeweza kusema kwamba ilikuwa haiepukiki, lakini ilikuwa inatarajiwa. Bunge lijalo la Ulaya litakuwa na sura mchanganyiko zaidi kuliko hili linalomaliza muda wake. Wawakilishi kutoka mirengo yote ya kisiasa - vyama vinavyoelemea siasa za mrengo wa kushoto na vile vilivyolalia sana kulia - watakwenda Strasbourg kwa makundi mwaka huu kuliko wakati mwengine wowote hapo kabla.

Ama kwenye suala la waliojitokeza kupiga kura, taswira ni ya mchanganyiko, katika baadhi ya nchi watu wengi zaidi walipiga kura mwaka huu kuliko miaka iliyopita, lakini wale waliopiga kura walikwenda kwenye visanduku kuvichagua vyama vyenye mashaka na Umoja wa Ulaya.

Kwa ujumla, hamu ya watu kuelekea Umoja wa Ulaya inashuka kwa kiwango cha kuogofya, ingawa vyama vyote vilijaribu kadiri vilivyoweza kuwashajiisha wapiga kura. Kwa mara ya kwanza, walichagua kuwa na wagombea wakuu kutembea bara zima na kufanya midahalo. Walijaribu sana kuufanya uchaguzi huu kuwa na sura binafsi na hata kuwa hai na unaomuhusu moja kwa moja mpiga kura, lakini mafanikio yalikuwa haba.

Wenye siasa kali hawana ajenda ya pamoja

Jambo pekee lenye uhakika ni kwamba bunge litaendelea kufanya kazi licha ya maadui wote hao ndani yake lenyewe. Wawakilishi kutoka vyama vya UKIP cha Uingereza, National Front cha Ufaransa na People's Party cha Denmark, hapana shaka, watatoa hotuba kali za hasira, lakini hawatakuwa na uwezo wa kuzuia chochote kisipite. Sababu ni kuwa wenyewe wana tafauti kubwa sana baina yao - maana wamejikita sana kwenye utaifa wa nchi zao wenyewe.

Kwa msingi huo huo, mara zote balagha yao imekuwa ikielekezwa moja kwa moja kwa wapiga kura wao kwenye nchi zao. Wanahiyari kuwa sauti ya wasioridhika kuliko kuwa na mtazamo wa pamoja baina yao.

Hii itawapelekea wale wenye msimamo wa kati na ambao wanapendelea Umoja wa Ulaya kusimama pamoja. Si kweli vile wengine wanavyoamini kuwa wanasiasa wenye siasa kali za kupinga Umoja wa Ulaya ni kitisho kikubwa. Hapana, hawako hivyo, angalau kwa kiwango cha Bunge la Ulaya.

Ulazima wa kuthamini mafanikio ya Umoja wa Ulaya

Yumkini kitu kinachokera zaidi ni ile hali ya wapiga kura kujitenga mbali na siasa barani Ulaya. Kwa watu wengi, inaonekana kuwa mafanikio makubwa ya Umoja wa Ulaya yamekuwa jambo la kimaumbile mno kiasi ya kwamba wanafikiri kila jambo litaendelea kama lilivyo.

Wanadhani mambo kama vile amani, uhuru wa kusafiri, kusoma na kufanya kazi, sarafu ya pamoja, na biashara huria Ulaya kote yatabakia tu milele.

Wakati wa kampeni za uchaguzi, ilikuwa rahisi kupata hisia kwamba Umoja wa Ulaya ni kuhusiana na kupiga marufuku balbu za umeme na kuweka sawa vitango-pepeta tu, licha ya kwamba muongozo huo ulishafutwa kitambo.

Ukweli ni kuwa mafanikio haya si ya milele kama wanavyodhani, tunaweza kuyapoteza. Tunapaswa kuendelea kuyapigania.

Mwandishi: Christoph Hasselbach/DW Europe Desk
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com