1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Uhuru wa vyombo vya habari bado washambuliwa

Ines Pohl
2 Mei 2019

Tawala kandamizi duniani ni adui mkubwa wa uhuru wa vyombo vya habari, lakini anaandika Ines Pohl kwenye maoni yake akihoji kwamba uholela kwenye mitandao ya kijamii na ukimya wa wanademokrasia navyo vinachangia.

https://p.dw.com/p/3Hphz
Reporter ohne Grenzen Logo
Picha: Getty Images/AFP/B. Guay

Kupiga marufuku machapisho, kuvibana vyanzo vya kiuchumi, na kuwafunga watu ni tabia zinazofahamika za tawala kandamizi duniani, ambazo kwazo huwa zinakusudia kuminya uwezo wa watu kuelezea mawazo yao. Lakini tawala katili si adui pekee wa uhuru wa vyombo vya habari duniani.

Kuna hatari nyengine ambazo si rahisi kuziona – hasa katika ulimwengu wa sasa wenye maumbile ya kusambaza haraka taarifa kupitia mtandao wa Intaneti: watu kupitia mashine hizo wanaweza kusambaza kwa kasi ya ajabu taarifa na picha za uzushi kwa lengo la kupotosha.

Habari za uzushi, kampeni za kashfa na vitisho kwenye mitandao ya kijamii sasa yamekuwa mambo ya kawaida. Kadiri siku zendavyo mbele, hata wataalamu wa kweli wa mawasiliano nao wanajikuta kwenye mtando wa mitandao. Kwa mfano, vituo vya televisheni vya Russia Today, RT, na Al Jazeera. Daima, mawasiliano kupitia mitandao ya kijamii ni ya kirafiki zaidi, wakati mwengine ya kuchekesha na ya utani.

Katika dunia changamano, yanatumika kurahisisha mambo. Juu ya hayo, mataifa mengi sasa yanazidi kujaribu kuugeuza ulimwengu mchanganyiko wa Intaneti kuwa dunia finyu inayodhibitiwa ndani ya mipaka yao. Ndicho tunachokishuhudia Iran, China na pia hata Urusi na Uturuki.

Ines Pohl
Na Ines Pohl, mhariri mkuu wa DWPicha: DW/P. Böll

Lakini kuna jawabu moja tu kwa hali hii: nalo ni kwamba watu lazima wajifunze kutafautisha uongo kutoka ukweli, na kwa hivyo elimu kuhusu vyombo hivi vipya vya habari lazima viwe sehemu ya mtaala wa masomo skuli, na lazima kuwe na jitihada za kuwavutia watu wazima kwenye ulimwengu huu.

Hatima ya hayo ni uhakikisho kuwa sio tu uhuru wa vyombo vya habari hauhatarishwi, bali pia na uhuru wa mtu kuelezea maoni yake kwenye faragha nao upo bila kitisho cha kukandamizwa kwa njia moja ama nyengine.

Mchango wetu kwenye kuhatarisha uhuru wa habari

Lakini ni ajabu kuwa wanasiasa waitwao wa kidemokrasia kutoka kote duniani, wakiwemo wa Ulaya kwa ujumla na hasa wa hapa Ujerumani, wanashindana kuiparatia China.

Haijalishi kwamba uhuru wa vyombo vya habari haupo kwenye nchi hii na matangazo ya idhaa za kigeni kama vile Deutsche Welle yamezuiliwa kwenye taifa hilo. Wafanyabiashara wanapoiangalia China wanachokiona ni biashara tu na sio haki za binaadamu.

Hali ni sawa na kwa Iran, ambako kinachojadiliwa ni fursa za kiuchumi tu, licha ya kwamba zaidi ya waandishi wa habari 20 hivi sasa wameshikiliwa kwenye magereza ya mateso. Nchini Bangladesh na Pakistan, waandishi wa blogu wanahatarisha maisha yao kwa kuandika tu ripoti zinazokosoa ukuwaji wa siasa kali za kidini nchini mwao. Uungwaji mkono kutoka nje ya mataifa yao, kwa hakika, ni mdogo. 

Angalia dunia inavyomsherehekea mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia ati kwa kuwa tu wanawake sasa wanaweza kuendesha gari, kwenda sinema, na hata kwenye viwanja vya michezo. Lakini kwa nini hakuna ukosowaji pale ambapo sote tunajuwa kuwa mwandishi wa blogu, Raif Badawi, anaozea jela?
Orodha inaweza ikawa kuendelea kwa muda mrefu. Ni orodha ya msiba.

Na leo, kuliko nyengine zote, ni siku bora zaidi ya kuwapima wanasiasa namna wanavyojitolea kupambana na mashambulizi haya dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari. Je, madikteta wanazingatia hasa maadili yetu? Je, wanasiasa wetu wako tayari kuacha biashara na madikteta hao endapo maadili haya yanavunjwa waziwazi? Je, wako tayari kutoa misaada ya maendeleo kwa kuihusisha na uhuru wa habari na haki za binaadamu?

Haya ni maswali ya kuwalenga wanasiasa wetu kwenye siku hii tunapoadhimisha Uhuru wa Vyombo vya Habari duniani.