Maoni : Fursa iliopotezwa - Mkutano wa Kilele Marekani na Afrika | Matukio ya Afrika | DW | 07.08.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Maoni : Fursa iliopotezwa - Mkutano wa Kilele Marekani na Afrika

Mkutano wa Kilele kati ya Afrika na Marekani ulikuwa na maneno matamu Afrika ni bara lenye matumaini makubwa na ahadi ya uwekezaji wa dola bilioni 14 kwa ajili ya uchumi wa Afrika lakini kwa kweli ni fursa iliopotezwa

.

Daniel Pelz wa Idhaa ya Kingereza kwa Afrika-DW.

Daniel Pelz wa Idhaa ya Kingereza kwa Afrika-DW.

Mbali ya wanadiplomasia na wawakilishi wa biashara na hata Rais Barack Obama mwenyewe hakuna walichoweza kutarajia ziada ya hicho katika mkutano huo.Mada ya mkutano huo ilikuwa ikijulikana wazi : maslahi ya kiuchumi ni kipau mbele cha kwanza! Masuala ya maendeleo, demokrasia na utawala wa sheria yalikuwa hayana umuhimu.

Wageni na demokrasia ya mashaka

Ingawa katika orodha ya wageni Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe hakualikwa,viongozi wengine waliruhusiwa kwenda Washington licha ya kwamba hawakujitolea katika kupigania kuwa na utawala wa sheria katika nchi zao. Mfano ni Rais Yoweri Museveni wa Uganda ambaye anataka kutawala milele na hiyo hata kuibadili katiba. Upinzani unakandamizwa nchini humo na kutokana na sheria kali ya kupiga vita ushoga ambayo hivi karibuni imebatilishwa na mahakama ya katiba Museveni ameshutumiwa duniani kote. Pia Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alikaribishwa katika mkutano huo mjini Washington licha ya kwamba anashtakiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kutokana na kuhusishwa na ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 nchini mwake ambapo takriban watu 1,000 waliuwawa.

Kualikwa kwa Museveni, Kenyatta na wengine kama hao kungeliweza kueleweka iwapo Obama angeliutumia mkutano huo wa kilele kuzungumza nao juu ya masuala ya demokrasia na haki za binaadamu katika mazungumzo binafsi ya kidiplomasia.Lakini ameliacha suala hilo katika wito wa jumla kama vile " Afrika inahitaji zaidi kuwa na uongozi bora" wito ambao baadhi ya wageni waalikwa hao wanatarajiwa kuupuzilia mbali.

Ni kuhusu fedha

Ukweli ni kwamba ulikuwa ni mkutano wa kilele kuhusu masoko, rasilmali za asili kutoka Afrika, uwekezaji na ajira.

Ni jambo zuri kwamba baada ya muda mrefu China kuwekeza barani humo sasa makampuni ya Marekani nayo yanawekeza kwa kiwango kikubwa lakini huo sio ufumbuzi wa matatizo ya Afrika.Ni muhimu kwamba fedha haziishi kwenye mifuko ya makampuni ya Marekani au wanasiasa wala rushwa wakati wafanyakazi wa kienyeji wakiendelea kuzama kwenye dimbwi la umaskini kwa kupokea mishahara duni.

Obama mwanasiasa halisi

Kwa mfano kama kweli serikali ya Marekani inataka kuisaidia Afrika ihakikishe kuna mfumo wa kusambaza maji unaofanya kazi kwa ufanisi katika sehemu nyingi za Afrika badala ya Obama kutamka katika kipindi cha usoni kampuni ya Coca Cola itaipatia Afrika maji safi ya kunywa kutoka kwenye chupa.Huo ni mtizamo finyu wa kibiashara kwa sababu kama nusu ya watu wanaoishi Afrika wanaishi kwa kutegemea pungufu ya dola 1.25 kwa siku kwa hiyo sio rahisi kumudu kinywaji cha Coca- Cola.

Hitimisho la mkutano huo limedhihirisha kwamba Obama anayetaka kuboresha dunia ni mwanasiasa halisi.Dira yake ya hamasa aliyoitowa wakati alipozuru Ghana hapo mwaka 2009 haipo tena.Sasa sera ya Marekani kwa Afrika inakuribiana na ile ya China: Fanya biashara na Afrika,chukuwa utajiri wa mali asili wa bara hilo na imarisha fursa za mauzo ili kuimarisha uchumi wao wenyewe.Hiyo ndio siasa hasa na pia ndio mwenendo lakini umaskini wa Afrika hauna maana kwao.

Mwandishi : Daniel Pelz/Mohamed Dahman

Mhariri :Yusuf Saumu

Matangazo

IJUE DW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com