Mandela alazwa tena hospitali | Matukio ya Afrika | DW | 08.06.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Mandela alazwa tena hospitali

Rais mstaafu wa Afrika Kuisini Nelson Mandela na shujaa wa mapambano dhidi ya utawala wa ubaguzi amelazwa tena hospitali Jumamosi(08.06.2013) baada ya hali yake kuwa mbaya kutokana na kupata tena maambukizi ya mapafu.

Mzee Nelson Mandela.

Mzee Nelson Mandela.

Mandela mwenye umri wa miaka 94,ambaye hapo mwaka 1994 amekuwa kiongozi wa kwanza mweusi kwa taifa hilo lenye nguvu kubwa kabisa za kiuchumi barani Afrika kufuatia uchaguzi wa kihistoria ulioshirikisha makabila yote, amewahi kulawa hospitali mara tatu tokea mwezi wa Disemba.Taarifa ya serikali imesema kwamba alikuwa akikabiliwa na maambukizi hayo kwa siku kadhaa sasa.

Serikali imesema kwamba hali yake ilizidi kuwa mbaya saa moja na nusu asubuhi na ilibidi kupelekwa katika hospitali ya Pretoria ambapo hali yake bado haijakuwa nzuri lakini iko thabiti.Msemaji wa ofisi ya rais Mac Maharaj amekiambia kituo kimoja cha televisheni cha ndani ya nchi kwamba madaktari wamewahakikishia kuwa yuko katika hali ya utulivu na kwamba ameanza kupumua mwenyewe.

Hata hivyo maneno yaliyotumiwa na serikali hususan neno la hali yake kuwa "mbaya" ni sababu ya kuwatia wasi wasi wananchi milioni 53 wa Afrika Kusini ambao kwao Mandela anaendelea kubakia kuwa alama kuu ya mapambano dhidi miongo kadhaa ya utawala wa wazungu walio wachache nchini Afrika Kusini.

Hali yake ni dhaifu

Mzee Mandela alipotembelewa na Rais Jacob Zuma hapo tarehe 29 mwezi wa Aprili 2013.

Mzee Mandela alipotembelewa na Rais Jacob Zuma hapo tarehe 29 mwezi wa Aprili 2013.

Mshindi huyo wa Tuzo ya Amani ya Nobel alijiuzulu akiwa rais hapo mwaka 1999 baada ya kuwepo madarakani kwa muhula mmoja na amejitenga na siasa kwa muongo mzima.Mara ya mwisho alionekana hadharani wakati wa fainali za michuano ya soka Kombe la Dunia mjini Johannesburg hapo mwaka 2010.

Pia aliwahi kuonekana kwa muda mfupi katika habari za televisheni ya taifa hapo mwezi wa Aprili wakati alipotembelewa nyumbani kwake na Rais Jacob Zuma.

Chama tawala nchini Afrika Kusini kilitumia nafasi hiyo kuwajulisha wananchi kwamba Mandela alikuwa katika hali nzuri ,juu ya kwamba alionekana kuwa amekonda na dhaifu akiwa ameketi kwenye kiti akiwa kimya bila ya kusema chochote huku kichwa chake kikiwa kimeegemezwa na mto.

Anasumbuliwa na maambukizi ya mapafu

Mzee Nelson Mandela katika picha ya mwezi wa Juni 2010.

Mzee Nelson Mandela katika picha ya mwezi wa Juni 2010.

Tokea aache kujishughulisha na harakati za kuhudumia wananchi ,amekuwa akiutumia muda wake kati ya nyumba yake ya kifahari ilioko Johannesburg na Qunu kijiji kilioko katika jimbo la kimaskini la Eastern Cape ambako ndiko alikozaliwa na kutumia maisha yake ya ujanani.

Mandela alilazwa hospitali kwa wiki tatu hapo mwezi wa Disemba kutokana na maambukizi ya mapafu na baada ya kufanyiwa upasuaji wa kuondowa vijiwe kwenye nyonga.

Huo ulikuwa ni muda mkubwa kwa Mandela kubakia hospitali tokea kuachiliwa kwake kutoka gerezani hapo mwaka 1990 baada ya kutumia kifungo cha takriban miongo mitatu gerezani katika kisiwa cha Robben karibu na mji wa Cape Town kwa kula njama ya kuupinduwa utawala wa ubaguzi wa rangi Afrika Kusini.

Matatizo yake ya maambukizi ya mapafu yameanzia tokea wakati alipokuwa kifungoni katika kisiwa cha Robben ambapo aliuguwa kifua kikuu.

Ni mtakatifu mno

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe.

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe.

Juu ya kwamba bado anahusudiwa sana, pia kuna wanaomkosowa nchini mwake na Afrika kwa jumla ambapo wanaona aliwaridhia mno wazungu baada ya kipindi cha utawala wa ubaguzi ambao ni asilimia 10 ya idadi ya wananchi wa Afrika Kusini.

Licha ya kukubaliwa kutekelezwa kwa sera za kuleta uwiano katika hali ya maisha ya wananchi zaidi ya miaka 10 sasa,Afrika Kusini inaendelea kuwa mojawapo ya jamii zenye ukosefu mkubwa wa usawa duniani ambapo wazungu bado wanadhibiti sehemu kubwa ya uchumi wa nchi hiyo.

Kwa wastani familia ya mzungu kipato chake ni mara sita zaidi ya kile inachopata famili ya mtu mweusi.

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe mwenye umri wa miaka 89 amekaririwa akisema katika kipindi simulizi kilichorushwa na televisheni ya Afrika Kusini mwezi huu kwamba "Mandela kidogo amekwenda mbali mno katika kuzitendea wema jamii za watu wasio weusi na mara nyengine kwa hasara ya weusi "

Amesema huo ni " Utakatifu mno,kuwa mwema kupindukia".

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters

Mhariri:Mtullya Abdu