1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Manchester United yamtimua Jose Mourinho

18 Desemba 2018

Manchester United imefuta kazi kocha Jose Mourinho baada ya klabu hiyo kuwa na mwanzo mbaya kabisa wa msimu katika karibu kipindi cha miaka 30.

https://p.dw.com/p/3AIUx
Fußball Mimik Trainer Jose Mourinho
Picha: picture-alliance/Offside/M. Atkins

Mechi ya mwisho kwa Mreno huyo mwenye umri wa miaka 55, iliisha kwa kichapo cha 3-1 dhidi ya vinara wa ligi Liverpool Jumapili iliyopita na kuwaacha nyuma katika nafasi ya sita na pengo la pointi 19 dhidi ya wapinzani hao.

Ndio mwanzo mbaya kabisa wa United katika ligi tangu mwaka wa 1990 na hata matumaini ya kutinga nafasi nne za kwanza na kujikatia tiketi ya kucheza Champions League yako hatarini huku klabu hiyo ikiwa nyuma kabisa ya nafasi hizo na pengo la pointi 11.

Licha ya klabu hiyo kutinga hatua ya mtoano ya ligi ya mabingwa Ulaya – wanakabiliwa na kibarua kikali katika hatua ya 16 za mwisho dhidi ya Paris Saint-Germain – mchanganyiko wa matokeo, mazingira mabaya miongoni mwa wachezaji na ukusoaji wa sera ya bodi ya usajili wa wachezaji vimedhihirisha kuwa sababu kuu za uamuzi wa kumtimua.

"Manchester United inatangaza kuwa Jose Mourinho ameondoka klabu hii maramoja,” Imesema taarifa ya klabu hiyo.

"Klabu hii ingependa kumshukuru Jose kwa kazi yake wakati alipokuwa na Manchester United na kumtakia kila la kheri katika siku za usoni.

"kocha mpya atateuliwa kwa ajili ya kushikilia usukani hadi mwisho wa msimu huu, wakati klabu ikiendelea na mchakato mkali wa kumleta kocha mpya wa mkataba wa kudumu.”

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Josephat Charo