1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Manchester United yamteua Erik Ten Hag kuwa meneja mpya

21 Aprili 2022

Manchester United imethibitisha leo kuwa Erik ten Hag ataondoka Ajax na kuwa meneja wa klabu hiyo msimu ujao.

https://p.dw.com/p/4AFJN
Fußball Trainer Erik ten Hag
Picha: Wolfgang Rattay/REUTERS

Ten Hag mwenye umri wa miaka 52, ambaye ametia saini kandarasi ya miaka mitatu, anakabiliwa na kibarua kigumu cha kuirudisha hadhi ya Manchester United ambayo imecheza misimu mitano mfululizo bila ya kushinda taji.

Raia huyo wa Uholanzi anakuwa meneja wa tano kwenye klabu ya Old Trafford tangu kustaafu kwa meneja mkongwe Sir Alex Ferguson mnamo mwaka 2013, wakati huo ukiwa wa mwisho kwa Manchester United kushinda taji la ligi kuu ya Premia.

"Ni heshima kubwa kuteuliwa meneja wa Manchester United, na nafahamu uzito wa kibarua kilichoko mbele yangu” alisema Ten Hag.

Meneja huyo anaelekea kushinda taji lake la tatu la ligi kuu ya Uholanzi akiwa na Ajax, na aliiongoza klabu hiyo mabingwa mara nne wa ligi ya mabingwa Ulaya hadi nusu fainali ya Champions League kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 2019, hiyo ikiwa mara ya kwanza kwa Ajax kufika nusu fainali ya mashindano hayo katika muda wa miaka 22.