1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Man City wapepea, Man United hoi Ligi Kuu ya England

8 Agosti 2022

Ligi Kuu ya England ilianza mwishoni mwa wiki ambapo mabingwa Manchester City walikuwa na mechi ngumu huko London dhidi ya West Ham.

https://p.dw.com/p/4FGtB
Fußball Bayern München v Manchester City | Erling Haaland
Picha: Justin Casterline/Getty Images/AFP

Ila mshambuliaji wao mpya Erling Haaland aliyafanya mambo kuwa rahisi katika uwanja ambao umekuwa ni changamoto kwa City kutoa ushindi kwa muda sasa.

City walipata ushindi wa 2-0 Haaland akiwa mfungaji wa magoli yote mawili na kocha Pep Guardiola anasema anafurahishwa na njaa au hamu ya ufungaji magoli aliyo nayo Haaland ambaye hakufurahishwa na kitendo cha kutolewa uwanjani baada ya kufunga mabao yake mawili.

"Jinsi alivyouchukua mpira kwa haraka ili aupige mkwaju wa penalti, nilipenda sana na kama mtu mwengine angekuja akauchukua ule mpira angempiga ngumi usoni, nina uhakika angefanya hivyo, na hiyo ni ishara nzuri, kwasababu inaonyesha anavyojiamini, malengo na alivyo sawa kisaiokolojia, Na hapakuwa na shaka kwasababu alifunga," alisema Guardiola.

United washushiwa kipigo nyumbani kwao

Ila mambo hayakuwa mazuri katika nusu ya pili ya Manchester, upande mwekundu wa Manchester kulikuwa na majonzi kwani licha ya kuwa nyumbani kwao Old Trafford na kuwa ni mechi ya kwanza kabisa ya kocha wao mpya Erik Ten Hag, Manchester United walirambishwa magoli 2-1 na Brighton & Hove Albion.

Erik Ten Hag amesema anafahamu fika kwamba kibarua alicho nacho ili kuirudisha timu hiyo kule ilikokuwa karibu mwongo mmoja uliopita, ni kikubwa mno.

Fußball Trainer Erik ten Hag
Kocha wa Manchester United Erik Ten HagPicha: Mike Egerton/PA/dpa/picture alliance

"Najua haya yangetokea ila nafikiri tungecheza vyema, hilo ni wazi. Ila najua pia kwamba mambo haya hayatofanyika kwa usiku mmoja tu na tulicheza vizuri katika mechi za kabla msimu. Leo tulikuwa na mchezo mbaya sana kipindi cha kwanza na tunastahili kujifunza kutokana na hilo, ni wazi kabisa," alisema Ten Hag.

Licha ya Anthony Martial kutoshiriki mechi hiyo kutokana na jeraha alilolipata, Cristiano Ronaldo alianza kama mchezaji wa akiba huku Christian Eriksen akianzishwa kama mshambuliaji.

Ten Hag alikuwa na haya ya kusema kuhusiana na suala hilo.

"Kwa sasa Cristiano Ronaldo amefanya mazoezi na sisi kwa siku kumi tu na huo ni muda mfupi sana kwa ajili ya kucheza dakika 90. Kwa hiyo, hiyo ndiyo sababu hasa ambayo hatukumuanzisha," alisema Ten Hag.

Makamu bingwa Liverpool walihitaji umahiri wa Mo Salah na mshambuliaji wao mpya Darwin Nunez ili waweze kutoa sare ya mabao mawili kwa vijana wapya Fulham baada ya Aleksander Mitrovic kupachika wavuni magoli mawili yaliyoifanya Fulham kuwa kifua mbele.