1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mamilioni yagharimia masomo ziada kwa wanafunzi Ujerumani

Hamidou, Oumilkheir18 Januari 2013

Hofu na wasiwasi, watoto wao wasije wakashindwa kufanya vizuri katika mitihani ya kumaliza masomo shuleni huwafanya wazee wengi watoe mamilioni ya fedha kuwalipa walimu wanaotoa mafunzo ya ziada majumbani.

https://p.dw.com/p/17N5X

Kufaulu vizuri masomo ndio linaloangaliwa kama sharti kwa mtu kuweza kuwa na matumaini mema ya kupata kazi. Hivyo ndivyo wazee wengi wanavyoiangalia hali ya mmbo siku hizi. Si ajabu kwa hivyo ikiwa wazee, wenye kujiweza, wanafanya kila wawezalo kuhakikisha watoto wao wanamaliza vizuri masomo yao shuleni. Ikiwa watoto hawafanyi vizuri shuleni, wanalipwa watu ili waje kuwasaidiwa. Kila mtoto mmoja kati ya wanne mwenye umri wa miaka 17 nchini Ujerumani, ameshawahi, angalao mara moja kulipiwa mwalimu aje kumsaidia ili aweze kujiendeleza vizuri shuleni. Paul anatokea Dortmund. Na ingawa hivi sasa yuko kidato cha nne, lakini anasema na yeye pia analo la kuelezea:

"Nilipokuwa shule ya msingi, nilikuwa nikifanya vizuri sana katika mitihani yote niliyofanya alama zangu daima zilikuwa nzuri. Na matokeo ya mtihani wangu wa kwanza katika shule ya sekondari ya Gymnasium yalikuwa kidogo.........."

Paul anaona bora asimalize kusema. Katika shule ya sekondari ya Gymnasium, mambo hayaendi vizuri sana, alama anazopata ni mbaya. Na hasa katika fani ya hesabu. Wazee wake wakaamua kumtafutia Paul mwalimu ili aje kumsaidia nyumbani. Katika wakati ambapo wanafunzi wenzake wanapumzika na kujishughulisha na mambo mengine, Paul analazimika kujifunza hesabu kwa bidii, saa moja kwa wiki. Kinachomtuliza ni ule ukweli kwamba wako wengi kama yeye wanaokumbwa na kishindo kama hicho nchini Ujerumani. Uchunguzi wa hivi karibuni umeonyesha asilimia 15 ya wanafunzi wa kijerumani wanapatiwa msaada wa kuendelea vyema na masomo yao shuleni. Katika madarasa ya juu kwa mfano katika shule za sekondari za Gymnasium idadi ya wanaopatiwa msaada kama huo inafikia asili mia 20. Stefan Biermann ni miongoni mwa wale wanaosaidia. Mwanafunzi huyo wa fani ya hesabu amekuwa akitoa mafunzo ya hesabu tangu miaka kumi iliyopita. Amegundua kwamba wanafunzi kupitia kile kijulikanacho kama "Mfumo wa G8 -" wanakabwa na shinikizo kubwa la kufanya vyema shuleni. Mfumo huo wa G8 unamaanisha ule utaratibu unaolazimisha mtihani wa kidato cha 12 - Abitur, kufanywa, baada ya mwanafunzi kupitisha miaka minane katika shule ya sekondari ya Gymnasium badala ya miaka 9 kama ilivyokuwa hapo awali katika baadhi ya majimbo ya magharibi ya Ujerumani.

"Kutokana na mfumo huu wa miaka minane ya Gymnasium, ninahisi takriban kila mwanafunzi anahitaji kusaidiwa. Na hasa katika fani ya hesabu, hakuna anayeweza kukwepa. Wazee wanawatafuta waalimu hao kupitia matangazo katika magazeti au yale ya Ebay kupitia mtandao. Kila mmoja anajitahidi kumpata mtu ambaye anaweza kusaidia kutoa mafunzo katika fani ya hesabu."

Makundi ya kila aina yanawania soko la masomo ya ziada

Mahitaji ni makubwa. Na hivyo hivyo ndivyo idadi ya wanaotoa mafunzo hayo ilivyo kubwa. Taasisi kadhaa, majukwaa kupitia mtandao wa Intaneti au hata watu binafsi - makundi ni mengi tu ya watu wanaojibwaga katika soko la kutoa mafunzo. Na ili kumpata mwalimu anayefaa, wazazi mara nyingi wanakuwa tayari kugharimia kwa muda mrefu mafunzo hayo ya ziada kwa ajili ya watoto wao.

"Mafunzo ya mwisho ambayo nililazimika kuyasitisha msimu wa kiangazi kwa sababu za ukosefu wa wakati, nilitoa kwa muda wa miaka mitano. Kuanzia kidato cha kwanza hadi kidao cha tano."

Stefan Biermann kawaida analipisha Euro kumi kwa saa moja - ni bei ya hisani kwa sababu wale wote anaowapatia mafunzo hayo anawajua tangu zamani. Lakini mtaalamu wa fani ya hesabu au mwalimu mstaafu wa hesabu anaweza kulazimisha alipwe kati ya Euro 25 hadi 35 kwa kila saa moja. Nchini Ujerumani Euro bilioni moja hadi bilioni moja na nusu zinatolewa kwa mwaka kugharimia mafunzo ya ziada kwa watoto, anakadiria mtaalamu mashuhuri anayechunguza masuala yanayohusiana na elimu, Klaus Klemm. Mtaalamu huyo anakosoa mfumo huu ulioenea wa kutoa mafunzo ya ziada akisema:

"Ninapouangalia mfumo huu, ninahisi kwa njia moja au nyengine kuna uzembe katika mifumo jumla ya elimu, pale wazazi wanapolazimika kutoa fedha zaidi na watoto na vijana nao kutumia wakati wao zaidi ili kulifikia lile ambalo kimsingi lilikuwa jukumu la shule kulifikia. Kwamba tuna mfumo ambao unazusha suala kama mwishowe mtu atafanikiwa kupata alama nzuri, kama hatofeli na kulazimika kufuata aina nyengine ya masomo, kutegemea kama wazee wake wanajimudu kifedha kuweza kugharimia, hilo nahisi mie linakwenda mbali mno."

Kusema kweli lakini mitindo ya wanafunzi kupatiwa mafunzo ya ziada, sio mtindo ulioenea Ujerumani tu. Uchunguzi uliosimamiwa na umoja wa Ulaya umeonyesha kwamba mtindo wa kutoa mafunzo ya ziada ili kuinua kiwango cha elimu kwa baadhi ya watoto umeenea hasa katika nchi za kusini mwa Ulaya. Katika nchi za Ulaya ya magharibi mtindo huo umeanza kupata nguvu tangu miaka kumi hivi iliyopita. Hali kama hiyo imeonekana pia katika nchi za Ulaya ya mashariki. Waalimu katika nchi hizo wanalazimika kutoa mafunzo ya ziada ili kujiongezea mapato yao. Pekee nchi za Ulaya ya kaskazini zinaonyesha kutekeleza kile ambacho mtaalamu wa masuala ya elimu Klaus Klemm anakipigania: yaani kuwepo mfumo wa elimu utakaopelekea kumalizika kiu cha watoto na wanafunzi kupatiwa mafunzo ya ziada.

Masomo ziada sio dawa

Kipi kinabidi kifanywe ili kuimarisha mfumo wa elimu nchini Ujerumani? Mtaalamu wa masuala ya elimu Klaus Klemm anasema:"Kuna miito kuhusiana na mfumo jumla wa elimu, misaada wanayoihitaji wanafunzi ili waweze kufanya bidii zaidi shuleni, iimarishwe katika mfumo wenyewe wa elimu. Hapo watu wanalenga ule mfumo wa shule kufunguliwa siku nzima, ili mchana wanafunzi waweze kushughulikiwa na kuangaliwa kama wamefanya kazi zao kama inavyotakikana na kadhalika. Na hasa kwa wale watoto ambao nyumbani hawezi kufanya hivyo. Hadi sasa lakini hakuna ushahidi wowote kama hilo linaweza kusaidia."

Ushahidi kwamba mfumo wa shule ya siku nzima sio lazima iwe ndo ufumbuzi wa matatizo umeonekana Ufaransa ambako licha ya shule kufnguliwa siku nzima, lakini watoto wanategemea zaidi msaada wa waalimu kutoka nje, kuwashinda wenzao wa Ujerumani. Na hata msaada huo haumaanishi kwamba alama za mitihani shuleni zinakuwa nzuri anasema Paul ambaye kwa muda wa mwaka mmoja na nusu amekuwa akipatiwa mafunzo ya ziada ya hesabu.

Kwa sasa wazazi wa Paul wameamua kutoendelea kumpatia mwalimu wa kumsaidia katika fani ya hesabu. Mwaka mmoja na nusu wanahisi inatosha.

Mwandishi:Hülsewig,Sola/Hamidou Oummilkheir

Mhariri:Josephat Charo