Makubaliano ya kuboresha Miji yafikiwa nchini Equador | Masuala ya Jamii | DW | 21.10.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Makubaliano ya kuboresha Miji yafikiwa nchini Equador

Makubaliano mapya ya muongozo wa kutatua matatizo yanayosababishwa na ongezeko la Miji yafikiwa katika mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu makaazi na maendeleo endelevu kwenye maeneo ya Mijini unaofahamika kama Habitat 3.

Makubaliano hayo mapya ambayo yanajulikana kwa jina la New Urban Agenda, NUA, yanafikiwa baada ya karibu miaka miwili ya mazungumzo yaliyokuwa yanaendelea kichinichini yakilenga kupatikana msimamo wa  pamoja katika kutoa kipaumbele kwenye maendeleo ya miji na majiji katika kipindi cha muda mrefu kijacho. Makubaliano hayo sasa yatatumika kama muongozo kwa maafisa wa mipango pamoja na mamlaka husika linapokuja suala la maendeleo katika miji kwa miongo ijayo.

Hata hivyo, kinyume na makubaliano ya mwaka jana ya Paris kuhusu mabadiliko ya tabia nchi ambayo yalihitaji utekelezaji wa kisheria kuhusu ongezeko la joto duniani, makubaliano haya ya NUA ni ya hiari, lakini akizungumza kwenye mkutano huo

"Makubaliano haya mapya yatatusaidia kuweka mipango ya hatua ambayo tutachukua kwa miaka 20 ijayo na tunathibitisha kuwa tutatekeleza mipango ili kufikia makubaliano yaliyofikiwa. Hapo kabla, hatukuwahi kuona kuwa  mipango miji ni tatizo linalohitaji kuzingatiwa." alisema Rais Rafael Correa wa Equador.

Frau in den Slums in Südafrika (AP)

Moja ya maeneo duni ya kuishi mjini Johannesburg, Afrika Kusini

Waziri wa Mazingira wa Ujerumani, Barbara Hendricks, amesema makubaliano hayo yana maana kubwa, kwa kuwa jamii ya kimataifa imejitolea kuboresha miji na sasa miji itakuwa katika nafasi nzuri ya kupambana na umasikini na kujiimarisha ili kuweza kuthibiti mabadiliko ya tabia nchi. 

Hata hivyo, mtaalamu wa masuala ya tabia nchi na miji kutoka shirika lisilo la kiserikali nchini Ujerumani Germanwatch, Lisa Junghans, ameyakosoa makubaliano hayo kwa kusema kuwa yamepungukiwa na taarifa muhimu.

Mkurugenzi wa Habitat 3, Joan Clos, amesema idadi ya watu wanaioshi mijini inaongezeka kwa kasi ambapo mpaka sasa kuna watu wapatao bilion 3.7 waishio mijini na inadhaniwa kuwa ifikapo mwaka 2050 idadi hii itaongezeka na kufikia bilion 7.

Mkutano huo hufanyika kila baada ya miaka 20 kujadili hatima ya miji mikubwa duniani kutoka nchi zote ambazo ni wanachama wa Umoja wa Mataifa. Wawakilishi kutoka nchi 190 duniani walihudhuria katika mkutano huu wa tatu, baada ya ule wa mwaka 1976 na 1999.

Mwandishi: Celina Mwakabwale/Reuters/DPA

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com