Makubaliano kati ya kikosi cha rais na majeshi ya kawaida yafikiwa Burkina Faso | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.09.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Makubaliano kati ya kikosi cha rais na majeshi ya kawaida yafikiwa Burkina Faso

Viongozi wa Jumuiya ya ECOWAS kuwasili Ouagadougou kwa mazungumzo zaidi na pande zinazohusika,wakati Rais Kafando akitangaza kurudi madarakani.

Rais Michel Kafondo

Rais Michel Kafondo

Wanajeshi wa kikosi maalum cha ulinzi wa rais RSP, ambao walikuwa nyuma ya mapinduzi nchini Burkina Faso, wamefikia makubaliano na majeshi ya kawaida yaliotiifu kwa serikali . Makubaliano hayo yaliotiwa saini usiku wa kuamkia leo, yana lengo la kuepusha matumizi ya nguvu na machafuko katika taifa hilo la Afrika magharibi.

Makubaliano hayo ambapo wamehusika pia viongozi wa kijadi yamepatikana wakati wapatanishi wakitarajiwa kuwasili mji mkuu Ouagadougou. Kwa mujibu wa masharti ya makubaliano, kikosi cha ulinzi wa rais kimekubali kuondoka katika mitaa ya mji mkuu na kurudi makambini, na wanajeshi wa kawaida watiifu kwa serikali watarudi nyuma kilomita 50 nje ya mji mkuu.

Burkina Faso Proteste und Gewalt

Umma ulipojitokeza kupinga mapinduzi

Kiongozi mmoja wa Jumuiya ya kikabila alisema, lengo ni kuepusha mapigano kati ya wanajeshi, kwani ni wao wenye wajibu wa kuwalinda raia na mali zao, na akatoa wito wa kusameheyana. Kikosi cha ulinzi wa rais ambacho kiliiuvamia mkutano wa baraza la mawaziri wiki moja iliopita na kuwakamata Rais Michel Kafondo na mawaziri kadhaa, kitabakia katika kambi Naba Kom nambari II katika mji mkuu na wanapaswa kuondoa silaha zao katika muda wa masaa 72.

Makubaliano hayo hata hivyo hayakuleta maafikiano kuhusu kikosi hicho kupokonywa silaha , kama majeshi ya kawaida yalivyotaka.Baada ya mkutano wa dharura wa Jumuiya ya uchumi ya Afrika magharibi ECOWAS mjini Abuja Nigeria jana , marais wa Senegal, Togo, Benin, Ghana, Niger na Nigeria watakwenda Burkina Faso leo kuhakikisha rais Kafondo anarejeshwa madarakani, ambaye muda mfupi uliopita , ametangaza kuwa amerudi tena madarakani.

Viongozi hao wanatarajiwa kushiriki katika duru ya pili ya mazungumzo leo hii. Kiongozi wa mapinduzi Brigedia Jenerali Gilbert Diendere alisema hapo mapema kwamba hana nia ya kubakia madarakani na atarejesha madaraka kwa utawala wa kiraia na akaongeza,"Tumo katika kujadiliana na kila mtu. Tunasubiri kitakachoamuliwa na na Ecowas. Tumekua tukiwasiliana kila wakati na Ecowas , kwa hiyo tunasubiri ."

Burkina Faso Ouagadougou Putsch

Wanajeshi wa RSP kurudi kambini

Mpango ulioandaliwa na marais wa Senegal na Benin unatoa wito wa kutolewa msamaha kwa waliohusika na mapinduzi hayo na kuwaruhusu wafuasi wa rais wa zamani Blaise Compaore, wagombee uchaguzi ujao. Campaore aliyeitawala Burkina Faso kwa miaka 27 aliangushwa na vuguvugu la upinzani wa umma Oktoba mwaka jana 2014 na kukimbilia uhamishoni nchi jirani ya Cote d´Ivoire. Brigedia Jenerali Diendere ,mkuu wa zamani wa majeshi wakati wa utawala wa Compaore, alidai kiongozi huyo wa zamani hakuhusika na mapinduzi hayo na wala yeye binafsi hakupata kuwasiliana naye tangu alipoangushwa.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman,Reuters, Dpa

Mhariri: Mohamed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com