1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makovu ya mashambulizi ya wanamgambo Msumbiji

John Juma
2 Machi 2022

Makovu ya machafuko yaliyofanywa na wanamgambo wenye itikadi kali za dini ya Kiislamu nchini Msumbiji yamewaacha na hofu maishani pamoja na masimulizi ya kuvunja moyo. 

https://p.dw.com/p/47uBK
Mosambik Vertriebene Bevölkerung In Cabo Delgado
Picha: DW

Zara Alifa Assumane mwenye umri wa miaka 62 anakumbuka kwa masikitiko makubwa, eneo ambako jamaa yake aliuawa.

Anasema miaka miwili iliyopita shangazi yake aliuawa. Ulimi ukanyofolewa. Akachinjwa kisha kichwa chake kikawekwa mlangoni mwao.

Wanamgambo walimfanyia unyama huo kama adhabu kwa sababu ya kuthubutu kujibizana nao walipokuwa wakiwahangaisha wakaazi wa kaskazini mwa Msumbiji.

Kumbukumbu nzito zisizosahaulika

Baada ya kisa hicho Zara aliikimbia nyumbani kwao Mocimboa da Praia na sasa anaishi kambini eneo la Montepuez, umbali wa kilomita 150.

Watu wengi wana masimulizi ya kusikitisha kutokana na madhila ya wanamgambo hao. Ishara ya mashambulizi hayo yametapakaa kila mahali.
Watu wengi wana masimulizi ya kusikitisha kutokana na madhila ya wanamgambo hao. Ishara ya mashambulizi hayo yametapakaa kila mahali.Picha: Marcelino Mueia/DW

”Bado nina wasiwasi. Siwezi kuacha kukikumbuka kisa kile. Wakati wanamgambo wenye itikadi kali za dini ya Kiislamu walipofika karibu na nyumbani kwetu walituamuru kila mmoja kutoka nje. Shangazi yangu alijibizana nao, na papo papo wakamuua kikatili. Wakamkata mikono na kutenganisha kisha wakaiweka kwenye kiwiliwili chake- mlangoni kwetu huku kichwa chake pia wamekitenganisha na kiwiliwili chake.” Amesema Zara Assumane huku akihuzunika.

Visa hivyo vya kikatili vilifanyika machoni pa mtoto wake wa kiume ambaye wakati huo alikuwa mikononi mwa wanamgambo hao baada ya kutekwa nyara.

Utulivu waanza kurejea japo kuna hofu

Kwa sasa kuna hali ya utulivu kidogo Msumbiji. Kambi inayowahifadhi wakimbizi imezidi kuwa kubwa na inawahifadhi maelfu ya wakimbizi. Mashirika ya kiutu yanatoa misaada ikiwemo maji na hata dawa. Uchumi pia umeanza kuimarika.

Vinyozi, mafundi cherahani na wachuuzi wengine wamefungua vioski na maduka kutoa huduma na kuuza bidhaa zao, huku wakipokea malipo hata kwa njia ya simu.

Watoto wanayauza mayai yaliyotagwa na kuku wanaofugwa na wakimbizi wenyewe kambini.

Pembezoni mwa barabara ni kibanda cha burudani. Watu hufika hapo kutizama filamu na soka. Mfano kwenye kibanda cha matangazo kimeandikwa wataonyesha mechi kati ya Barcelonas na Napoles.

Kambi inayowahifadhi wakimbizi imezidi kuwa kubwa na inawahifadhi maelfu ya wakimbizi.
Kambi inayowahifadhi wakimbizi imezidi kuwa kubwa na inawahifadhi maelfu ya wakimbizi.Picha: DW

Kundi la al-Shabaab ambalo halina uhusiano wowote na wanamgambo wa Somalia licha ya majina yao kufanana, limekuwa likishambulia miji na vijiji na kuwafurusha takriban watu 800,000. Zaidi ya watu 3,700 miongoni mwao raia 1,600 tayari wameuawa kufuatia machafuko hayo.

Hata hivyo mifano ya mashambulizi yaliyomkuta shangazi yake Assumane ni machache siku hizo.

Vikosi vya kigeni vyasaidia kupambana na wanamgambo Msumbiji

Tangu mwezi Julai mwaka uliopita, vikosi vya jeshi vya Rwanda na kutoka jumuiya ya kimaendeleo ya nchi za kusini mwa Africa SADC, vimekuwa vikivisaidia vikosi vya Msumbiji kushika doria na kuwadhibiti wanamgambo.

Jimbo la Cabo Delgado lililoko kaskazini mwa Msumbiji ndilo eneo pekee la Msumbiji lenye idadi kubwa ya Waislamu nchini humo. Ni jimbo lenye utajiri mkubwa wa gesi asilia na madini mengine.

Juhudi za kuchimba gesi zimevutia uwekezaji mkubwa zaidi barani Afrika, ukiwemo mradi wenye thamani ya dola bilioni 20 unaosimamiwa na kampuni ya nishati TotalEnergies.

Jimbo la Cabo Delgado lina utajiri wa gesi asilia na limevutia uwekezaji mkubwa Afrika.
Jimbo la Cabo Delgado lina utajiri wa gesi asilia na limevutia uwekezaji mkubwa Afrika.

Eneo la Montepuez nchini humo lina utajiri wa vito vya rubi. Kampuni ya uchimbaji madini ya Uingereza ya Gemfields huendesha shughuli zake katika eneo hilo.

Miongoni mwa mambo yanayochochea uanamgambo ni kushindwa kwa uwekezaji wa gesi kusaidia kuboresha viwango vya maisha ya wananchi katika taifa hilo ambalo ni kati ya mataifa maskini zaidi ulimwenguni.

Karibu na uwanja wa ndege wa Pemba ambako ndege kutoka Lesotho na Botswana zipo, kuna kambi ya kijeshi ambayo wanajeshi wa kigeni wanaosaidia katika vita dhidi ya wanamgambo wanatumia kama kituo chao cha operesheni.

Shirika la misaada la Afrika Kusini Joint AId Management ni miongoni mwa mashirika yanayowasaidia wakimbizi kambini. Mkurugenzi wake mtendaji Killen Otieno amefanya kazi nchini Somalia, Sudan Kusini na maeneo mengine yanayokumbwa na machafuko. Lakini anasema yaliyoikumba Msumbiji ni ya kusikitisha mno.

Vikosi kadhaa vya kigeni vikiwemo vya Rwanda vinavisaidia viko Msumbiji kusadia katika vita dhidi ya wanamgambo.
Vikosi kadhaa vya kigeni vikiwemo vya Rwanda vinavisaidia viko Msumbiji kusadia katika vita dhidi ya wanamgambo.Picha: Roberto Paquete/DW

"Katika miaka yangu 30 ya kufanya kazi katika maeneo ya migogoro, sijawahi kushuhudia hali kama hii niliyoishuhudia Cabo Delgado.” Amesema Otieno.

Nini huchochea uanamgambo Msumbiji?

Wakaazi wa kaskazini mwa Msumbiji huhisi kutengwa na serikali kwa muda mrefu. Waasi wa kikomunisti eneo hilo walipambana vikali katika vita vya wenyewe kwa wenyewe wakati nchi hiyo ilipotumbukia katika kile kilichokuwa kama Vita Baridi.

Wakati huo, waasi walitaka kuchukua udhibiti wa nchi. Kwa sasa wanamgambo wanataka kuunda dola lakini malengo kamili hayajajulikana.

Cornielo Manuel mwenye umri wa miaka 31 ambaye zamani alikuwa mvuvi anasema walipovamiwa, washambuliaji walijitambulisha kama al-Shabaab. Walifyatua risasi na kuacha damu ya watu ikitapakaa ardhini.

Cornelio amesema alihesabu takriban watu 50 ambao anadai waliuawa siku hiyo.

(AFPE)