1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makampuni ya kigeni ya kilimo nchini Msumbiji, yawatia hofu wakulima

2 Januari 2014

Wakulima nchini Msumbiji wamekumbwa na hofu ya kunyang'anywa sehemu ya mashamba yao na kupewa makampuni ya kigeni yanayotumia teknolojia ya kisasa katika sekta ya kilimo.

https://p.dw.com/p/1AkX8
Rais wa Msumbiji Armando Guebuza akiwa na mkewe Maria Guebuza
Rais wa Msumbiji Armando Guebuza akiwa na mkewe Maria GuebuzaPicha: picture-alliance/dpa

Kumekuwa na hofu miungoni mwa wakulima katika baadhi ya maeneo nchini Msumbiji kutokana na serikali hiyo kwa kushirikiana na shirika la misaada la Brazil, ABC na shirika la misaada la Japan JICA, kuanza mradi wa mpango maalum wa kilimo kwa teknolojia mpya ya nchi zenye hali ya hewa ya Kisavanna, unaojulikana kwa jina la Prosavanna. Mradi ambao umesababisha wengi wa wakulima kunyang'anywa sehemu ya mashamba yao na kuingizwa chini ya umiliki wa makampuni ya kigeni yanayoendesha mradi huo.

Aidha Kutokana na serikali ya Msumbiji kuvutiwa na teknolojia hiyo ya kilimo inayofanya kazi vizuri katika nchi za Tropic ambapo inayotumika sana nchini Brazil, imeamua kuingiza mradi huo nchini humo kwa lengo la kuongeza uzalishaji katika sekta hiyo kwenye eneo la Nacala, lenye ukubwa wa hecta milioni 14.5, kaskazini mwa msumbiji, kwenye hali ya hewa inayofanana na mji Cerrado Nchini Brazil, kwenye mafanikio makubwa ya matumizi ya teknolojia hiyo.

Hata hivyo asilimia 80 ya wakazi wapatao milioni 4.5 waliopo katika eneo la Nacala msumbiji, wanaishi mashambani na kufanya kuwepo kwa idadi kubwa ya watu wanaoishi huko, ambapo mradi wa teknolojia hiyo utawaathiri kwa kiwango kikubwa, tofauti na ukilinganisha na nchi nyingine walipofanikisha mpango huo ambapo hakuna wakazi wengi katika maeneo ya mashambani.

Mojawapo ya maeneo ya wazi nchini Msumbiji
Mojawapo ya maeneo ya wazi nchini MsumbijiPicha: Ange-Benjamin Brida

Wakulima kunyang'anywa mashamba yao

Hofu iliyopo miungoni mwa wakulima ni hiyo ya kunyang'anywa mashamba yao, ambapo wengi wao wanajaribu kutetea haki yao ya umiliki kwa kuzingatia sheria ya kimila ya umiliki ardhi nchini humo inayojulikana kwa jina la DUAT, ingawaje hati hiyo haijatoa uhakika wa umiliki wa moja kwa moja.

Shirika la habari la IPS, limezungumza na baadhi ya waathirika wa zoezi hilo, na kubaini hayo. Rodolfo Razao mwenye umri wa miaka 78, mkulima anayetokea katika wilaya ya Monapo kwenye jimbo la Nampula nchini Msumbiji, alipata hati miliki ya shamba lake lenye ukubwa wa heka 10 mwaka 2010, lakini amefanikiwa kulima heka 7 pekee na heka nyingine tatu za shamba lake zimechukuliwa na kampuni moja ya kilimo kutoka Afrika Kusini, inayomiliki shamba lenye ukubwa wa hekta elfu 10, kaskazinimashariki mwa nchi hiyo, na hadi sasa hakuna popote anapoweza kufungua madai yake, wakati mkulima mwingine aliyefanya mahojiano na IPS katika eneo la Nacololo, ambaye ni mjane mwenye watoto saba, Brigida Mohamad mwenye umri wa miaka 50, alionekana kuhofia mmoja wa watoto zake, kupoteza haki ya kupata tena shamba lake lililochukuliwa na kampuni hiyo hiyo ya kutoka Afrika kusini.

Mmoja wa wananchi amesema, licha ya athari zitokanazo na teknolojia hiyo mpya ya kilimo nchini msumbiji, Ujio wa wawekezaji katika mradi huo wa kilimo, nao umekuwa tishio kwa wananchi, kwani baadhi yao wataathirika na zoezi zima la mpango huo.

Serikali yasema inawaboreshea mbinu kilimo

Mratibu wa mradi huo wa kilimo, Calisto Bias, ameliambia shirika la habari la IPS kuwa, wakulima hawatapoteza haki ya kumiliki ardhi yao, na kuongeza kuwa nia kuu ya mpango huo ni kuwasaidia kuishi ndani ya eneo la mradi huo na kuwasaidia kuboresha mbinu zao za kilimo.

Hata hivyo, afisa maliasili wa Shirika la mazingira la Msumbiji, Sheila Rafi amesema mradi huo utateteresha mfumo mzima wa maisha ya watu wa jamii hizo, waliokuwa wakitegemea mashamba yao kwa kilimo cha chakula,ambapo wawekezaji wataingiza mfumo wa kuwaajiri kwa ajilimya kuzalishia makampuni hayo.

Wanaharakati kupinga mpango huo

Wanaharakati wa mashirika ya kijamii yapatayo 23 mjini Maputo, na mashirika ya kimataifa yapatayo 43 yameandika barua ya wazi kwa serikali ya Msumbiji, Japan na Brazil, zinazosimamia mradi huo, na kutaka kusitishwa kwa zoezi hilo, kutokana na kutofuata sheria na kutotumiwa demokrasia ya ushirikishi wa maoni ya wananchi kabla ya kuamua kupitisha mradi huo, ambao kwa upande mwingine una athari za kimazingira.

Mwandishi: Diana Kago/IPS
Mhariri: Mohamed Abdul Rahman