Maoni ya wahariri.
6 Mei 2008Wahariri wa magazeti kadhaa ,leo ,katika maoni yao wanaliangalia tatizo la ulevi miongoni mwa vijana nchini Ujerumani.
Gazeti la WESTFALEN POST linazungumzia juu ya mkasa wa maiti tatu za watoto wachanga zilizokutwa ndani ya friji.
Na mhariri wa gazeti la LEIPZIGER VOLKSZEITUNG anapongeza uamuzi juu ya kuwaadhibu vikali madereva wanaokimbia kana kwamba wanafukuzwa.
Ripoti mpya inaonesha kuwa tatizo la ulevi linazidi kuwa kubwa miongoni mwa vijana nchini Ujerumani. Gazeti la ALLGEMEINE ZEITUNG linauliza kwa nini vijana wengi wanatumia ulevi kama njia ya kuyakabili maisha yao.
Mhariri wa gazeti hilo anajibu swali lake kwa kueleza kuwa vijana hao wanakunywa pombe sana kutokana na shinikizo la maisha kuzidi kuwa kubwa katika jamii. Wanalazimika kuonesha uwezo wa ushindani ambao hawana.
Gazeti linafafanua kuwa vijana hao hawana mifano bora ya kuiga na ndiyo sababu kwamba mifumo yao ya maadili imetenguka.Lakini mhariri wa gazeti hilo anawaambia vijana wa kijerumani ;kuvuta na kulewa siyo suluhisho.
Mhariri wa gazeti la DRESDENER NEUESTEN NACHRICHTEN anaunga mkono wazo la kupiga marufuku matangazo ya biashara juu ya sigara na ulevi .
Anasema anaeghabishwa na tabia ya vijana wanaolewa ,kiasi cha kupoteza fahamu,hana budi aunge mkono hatua kali za kuzuia ulevi- ikiwa pamoja na kupiga marufuku mambo yote yanayotukuza sigara na pombe.
Mhariri wa gazeti la DRESDENER NEUESTEN NACHRICHTEN anatilia maanani kuwa pombe sasa , imekuwa uraibu wa hatari miongoni mwa vijana wa kijerumani.
Lakini, mhariri huyo anasema vijana hao wanafuata mfano wa watu fulani, kwani nchini Ujerumani watu milioni kumi wanautatika kupita kiasi.Vijana wanaiga tu.
Mapema wiki hii Ujerumani ilishtushwa tena ,kutokana na habari juu ya kukutwa maiti tatu za watoto wachanga ndani ya friji. Juu ya hayo gazeti la WESTFALENPOST linauliza vipi balaa kama hilo linaweza kutokea bila mtu kujua.
Mhariri anauliza iwapo hakuna mtu alieomwona mama aliewabeba watoto hao tumboni. Jee hakuna mtu aliemwona mama huyo alivyokuwa mjamzito mara tatu? Ili kuepusha balaa kama hilo mhariri anashauri juu ya kuweka vitengo vya msaada, ambapo akina mama wanaweza kupeleka watoto ikiwa wanashindwa kuwahudumia.