1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini hii leo

7 Aprili 2010

Yalivosema leo magazeti ya Ujerumani

https://p.dw.com/p/Mp3d
Rais Barack Obama wa Marekani akiwaarifu waandishi wa habari katika Ikulu ya Washington, Machi 26, 2010, baada ya kumpigia simu Rais Dmitry Medvedev wa Urusi kuzungumza juu ya mkataba mpya wa kupunguza silaha za hatari, START.Picha: AP

Magazeti ya leo ya hapa Ujerumani yalijishughulisha sana na operesheni za jeshi la Ujerumani huko Afghanistan, na hasa nini kifanywe kutokana na kuuwawa wiki iliopita wanajeshi watatu wa Kijerumani na kujeruhiwa wengine wanane katika mapambano na waasi wa Kitaliban. Uzito ulitiliwa juu ya haja ya kuliongezea uwezo wa kisilaha jeshi la Ujerumani.

Lakini pia suala la mkakati mpya wa kinyukliya wa Marekani ulipata uwanja katika magazeti. Kwa mfano, gazeti la  DIE  BADISCHE ZEITUNG  linalochapishwa mjini  Freiburg lilikuwa na haya ya kusema:

"Tangazo la Rais Barack Obama kuachana na kutengeneza   silaha mpya za kinyukliya na kuahidi kupambana na shambulio lolote lislokuwa la kinyukliya kwa kutumia silaha zisizokuwa za kinyukliya ni ishara ya kisiasa, na ni kuachana wazi wazi na ile nadharia ya kinyukliya ya mtangulizi wake, George Bush. Hatua kwa hatua, Barack Obama anakaribiana na lile lengo lake la kupunguza kwa sehemu kubwa sana silaha za kinyukliya za nchi yake. Pamoja na Obama, mdahalo juu ya kuachana na silaha za kinyukliya ambao baada ya kumalizika Vita Baridi ulisahauliwa kwa  sehemu kubwa, sasa unarejea katika ajenda ya majadiliano ya kimataifa.. Peke yake hilo ni jambo kubwa ambalo ni zuri."

Na kwa maoni ya gazeti la SAABRÜCKER ZEITUNG:

" Barack Obama anajidhihirisha kama mwanasiasa anayetambua ukweli halisi wa hali ya mambo, na ambaye anawania kile kitu kinachowezekana badala ya kujichovya katika ndoto zinazovutia. Rais huyo wa Marekani anatambua kwamba maendeleo ya kweli yanaweza tu kupatikana katika suala la kuachana na silaha za kinyukliya ikiwa ataweza kulifanya bunge la nchi yake liwe upande wake. Ndio maana hasa ile hati iliowasilishwa jana imetoa mibadala yote kwa tahadhari. Kwa ujumla, Obama, mshindi wa zawadi ya amani ya Nobel, kupitia mkakati wake huo, anaimarisha kuaminiwa Marekani. Na jambo hilo linafanyika hasa katika wakati muwafaka, siku mbili kabla ya kutiwa saini mjini Prague mkataba wa kupunguza silaha za hatari, na wiki moja  kabla ya kuanza mkutano wa usalama wa kinyukliya mjini Washington.

Na kutoka Kusini mwa Ujerumani, gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG lilikua na haya ya kusema juu ya mada hiyo hiyo:

"Na tena wananung'unika watu wote, wale wanaojishughulisha na amani na wale wanaopalilia vita baridi. Kuna wale  wanaosema kwamba mkakati wa siasa ya kinyuliya, ambapo sasa Rais Obama anataka, angalau, kupunguza matumizi ya vyombo hivyo vya kishetani, hauendi mbali vya kutosha. Mwishowe rais huyo hajaamini kusema wazi wazi kabisa na kuahidi kwamba nchi yake haitakuwa ya mwanzo katika kutumia silaha za kinyukliya kwenye hujuma. Lakini watu wa mrengo wa shoto hawatambui kwamba jambo kama hilo litawakasirisha Wamarekani wa mrengo wa kulia. Pale rais huyo alipowaambia majenerali wake- pia marafiki na maadui kote duniani-kwamba dola hiyo kuu itatatafakri na, kiutendaji, kufanya iwe vigumu kutumia silaha hiyo kubwa kati ya silaha zote, basi yeye anayafanya maisha ya hapa kwenye sayari hii kuwa ya amani zaidi. Lile lengo la kuachana kabisa na silaha linabaki kuwa mbali, lakini  Obama anaisafisha njia ya kuelekea huko."

Gazeti la SCHWERINER VOLKSZEITUNG liliandika juu ya mdahalo wa kulipatia silaha jeshi la Ujerumani:

"Magari machache ya vifaru, matatizo ya kupata msaada kutoka jeshi la anga, makosa katika  utayarishaji- hayo ni mambo yasioingia akilini katika operesheni ambayo kwamba kila siku kuna suala la uhai na kifo. Hilo ndilo suala ambalo waziri wa ulinzi, zu Guttenberg, na mtangulizi wake waliliachilia, na ndio maana upungufu huu ulio wazi na wa hatari hadi leo bado ungaliko. Bila ya shaka mtu hawezi kusema kwamba hakutakuweko hatari kabisa katika operesheni za huko Afghanistan. Na kuwa na silaha hakubadilsihi sana hali hiyo. Lakini hakuna sababu ya kuaminika kwamba vijana wa jeshi la Ujerumani wana upungufu wa vifaru madhubutina na wanalazimika kupiga doria na magari ya kijeshi yasiokuwa ya vifaru. Hapa mipango imekuwa ni mibaya, na matumizi ya fedha yanapunguzwa mahala sipo."

Hivyo ndivyo lilivoandika SCHWERINER VOLKSZEITUNG.

Nalo gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG, likitumalizia uchambuzi huu wa magazeti ya Ujerumani hii leo, liliandika hivi kuhusu kuweko wanajeshi wa Kijerumani Afghanistan:

"Mwanzoni malalamiko yalikuwa juu ya upungufu wa vifaru. Hali imeboreka. Upungufu mkubwa, na jambo hilo limelalamikiwa  muda mrefu, ni katika helikopta. Na licha ya ombi la  Shirika la NATO kwa nchi shirika, jambo hilo halijafua dafu hadi sasa. Ni Wamarekani tu wenye, unaweza kusema, idadi inayofaa ya vyombo hivyo. Kwa hivyo, wale wahakiki wa hii leo inafaa wakumbuke haya pale suala la bajeti ya wizara ya ulinzi itakapojadiliwa tena bungeni Ujerumani."

 Hivyo ndivyo lilivohoji gazeti la Frankfurter Allgemeine Zeitung.

Mwandishi: Othman Miraji/Dt Agenturen.

Mpitiaji: Abdul-Rahman, Mohammed