Magazeti ya Ujerumani kuhusu Afrika | Magazetini | DW | 16.03.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Magazeti ya Ujerumani kuhusu Afrika

Sera mpya ya Visa inayofikiriwa na Umoja wa Ulaya kukabiliana na wimbi la wahamiaji kutoka Afrika,kujiuzulu rais wa Mauritius Ameenah Fakim ni masuala yaliyoandikwa kuhusu Afrika katika magazeti ya Ujerumani wiki hii

Suala la wahamiaji barani Ulaya na sera mpya inayofikiriwa na Umoja huo kuhusu masharti ya visa kwa nchi ambazo zitashindwa kushirikiana na Umoja huo katika mpango wa kuwapokea wahamiaji watakaorudishwa barani Afrika kwa kukataliwa ukaazi katika nchi za Ulaya,pamoja na kujiuzulu rais wa Mauritius Ameenah Gurib baada ya kashfa ya rushwa ni miongoni mwa mada ambazo wahariri wa magazeti nchini Ujerumani wamejishughulisha nazo kuhusu Afrika.

Neue Zürcher Zeitung

Mhariri wa gazeti hilo ameanza kwa kueleza kwamba halmashauri ya Umoja wa Ulaya inataka kuitumia sera ya utoaji visa kama karata yake,kwa kuweka wazi kwamba nchi itakayoshindwa kutoa ushirikiano katika utaratibu wa kuwapokea wahamiaji wanaokataliwa hifadhi Ulaya basi itakabiliwa na masharti magumu ya visa za kuingia nchi za Ulaya. Kwa miaka kadhaa Umoja wa Ulaya umekuwa ukihangaika kutafuta njia za kuimarisha utaratibu wa kuwarudisha wahamiaji wasiokuwa na vibali vya kukaa ulaya,hata hivyo mafanikio ya juhudi hizo ni ndogo kutokana na utaratibu huo kutegemea sana ushirikiano wa  nchi za asili wanakotokea wahamiaji hao. Kwa mujibu wa takwimu za halmashauri ya Umoja wa Ulaya  kila mwaka kuna wahamiaji zaidi ya 500,000 ambao wanaishi katika nchi za Ulaya waliokataliwa hifadhi na asilimia 40 tu ya wahamiaji hao ndio wanaoweza kurudishwa katika nchi zao za asili. Sasa basi kutokana na hali hiyo Umoja wa Ulaya unataka kutumia sera yake ya utoaji visa kama karata ya kuupangua mchezo.Kwa maana hiyo visa ya Schengen itatolewa kwa kuzingatia utaratibu maalum ambao utazifanya nchi zisizotoa ushirikiano kwa Umoja huo wa Ulaya wa kupokea wahamiaji kukabiliwa na masharti magumu.Kamishna anayehusika na masuala ya uhamiaji katika Umoja wa Ulaya Dimitris Avramopoulus amesema Umoja huo  utafanya mara kwa mara tathmini ya ushirikiano wa nchi hizo na Umoja huo.

Kuhusu Mauritus

 

Neue Zürcher limeandika pia kuhusu hatua iliyochukuliwa na rais wa Visiwa vya Mauritius Ameenah Gurib Fakim ya kujiuzulu baada ya kashfa ya rushwa. Gazeti hilo linasema hatua hiyo ni wazi kwamba sasa imelifanya bara zima la Afrika kutokuwa katika nafasi hiyo kubwa kabisa ya uongozi wa nchi.Mhariri anasema

Kwa hakika kila kitu kilikuwa shwari na Jumatatu nchi hiyo ya visiwa ya Mauritius ilikuwa katika shamrashamra ya kutimiza miaka 50 ya uhuru walioupata kutoka kwa waingereza.Na nchi hiyo ya bahari ya hindi ambayo ni pepo ya watalii  daima ikionekana kuwa nchi inayoongozwa vizuri ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika,na juu ya hilo ndio pekee iliyokuwa imebakia kuongozwa na mwanamke. Lakini ghafla akalazimika rais Ameenah Gurib-Fakim kuachia ngazi kutokana na kadhia ya rushwa iliyomuandama.Gazeti la L Express la Mauritius mwezi uliopita wa Februati lilifichua kwamba rais huyo alitumia kadi ya mkopo ya benki iliyotolewa na shirika la msaada la kimataifa la Planet Earth Institute akiwa nchi za nje kujinunulia nguo,viatu,mapambo na vitu vingine vya kibinafsi kwa gharama ya sio chini ya Yuro 25,000.Japo rais Gurib amedai hakutenda kosa lolote kwakuwa fedha hizo alizirudisha.

Die Tageszeitung

Afrika kusini pia imeangaziwa wiki hii na gazeti la Die Tageszeitung limezungumzia kuhusu kukauka kwa maji kutokana na ukame ambako kumesababisha kizazaa katika mji wa Capetown huku watu wakisubiri kile kilichoitwa ''Day Zero''au siku ambayo hakuna hata tone la maji litakalotoka kwenye mabomba ya maji katika mji huo.Hata hiyo siku hiyo haikutokea.Na mhariri anasema.

Kile kilichopewa jina Day Zero katika mji unaokumbwa na ukame mkali wa Capetown kimekhairishwa.Siku hiyo ilikusudiwa kwamba hakuna tone hata moja la maji litakalotoka kwenye mabomba ya maji,na kwahakika siku hiyo ilianza kutongazwa mara nyingi toka miezi kadhaa iliyopita.Lakini sasa alau serikali ina matumaini kwamba tukio hilo bado  linaweza kuepukika mwaka huu. Lakini hiyo haimanishi kwamba tatizo la maji limeondoka.Afrika Kusini bado inakabiliwa na mgogoro wa maji na imetangaza ukame katika mji huo wa Capetown na sehemu nyingine kwamba ni janga la kitaifa.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com