Magazeti ya Ujerumani juu ya Lubanga | Magazetini | DW | 16.03.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Magazeti ya Ujerumani juu ya Lubanga

Magazeti ya Ujerumani karibu yote yameizingatia kwa mapana na marefu hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa inayopambana na uhalifu ya mjini The Hague kwa Mbabe wa kivita, Thomas Lubanga.

Mahakama ya Kimataifa ya mjini The Hague

Mahakama ya Kimataifa ya mjini The Hague

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limechapisha makala juu ya hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya mjini The Hague kwa Thomas Lubanga , aliyekuwa kiongozi wa waasi katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.Lubanga alipatikana na hatia ya kuwatumikisha watoto kama askari.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limemkariri Waziri wa sheria wa Ujerumani, Sabine Leutheusser Schnarrenberger akisema kuwa hukumu hiyo ni wasaa wa kihistoria katika sheria za kimataifa. Waziri huyo amesema kutokana na hukumu hiyo madikteta,viongozi wa waasi na wahalifu wengine duniani kote watafikiria mara mbili kabla ya kutenda uhalifu.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limemkariri Waziri huyo wa Ujerumani akisema kuwa hatua ya Mahakama ya Kimataifa ya mjini The Hague kumtia hatiani mbabe wa kivita Lubanga imewapa watu moyo kwamba haki za binadamu zinaiimarika duniani. Juu ya hukumu hiyo gazeti la "Westfalen Blatt" limesema katika maoni yake kuwa madikteta na wahalifu wa kivita hawataweza tena kujifanya viziwi, ishara zinapotolewa na jumuiya ya kimataifa. Lakini gazeti la "Westfalen Blatt" linasema kwamba Mahakama ya Kimataifa ya mjini The Hague ina udhaifu, kwa sababu nchi muhimu kama vile Marekani, China na Urusi hazimo katika mchakato wa mkataba wa Roma ulioweka msingi wa kuanzishwa kwa Mahakama ya mjini The Hague.

Gazeti la "Financial Times Deutschland" pia limelalamika katika maoni yake kwamba kesi zinazosikilizwa na Mahakama ya mjini The Hague zinachukua muda mrefu sana.

Gazeti la "Die Zeit" wiki hii limechapisha makala juu ya filamu ya kiongozi wa kundi la Lord's Resistance Army, Joseph Kony. Filamu hiyo iliyopelekwa katika ukanda wa "You Tube" ilitayarishwa na shirika moja la hisani la Washington. Katika filamu hiyo watayarishaji wametoa mwito kwa majeshi ya Uganda yanayosaidiwa na Marekani wa kumkamata Joseph Kony. Katika makala yake mwandishi wa gazeti la"Die Zeit" ametilia maanani kuwa katika muda wa siku kumi tu baada ya filamu hiyo kuonyeshwa katika Ukanda wa "You Tube", simu zilipigwa mara zaidi ya milioni mia moja.

Watoto na vijana nchini Ujerumani waliijadili filamu hiyo mpaka mijadala yao iliwafikia wazazi wao. Aghalabu wazazi wa watoto hao hawafuatilii masuala ya kisiasa wanapoangalia mitandao ya kijamii. Mwandishi wa gazeti la "Die Zeit" anasema bila ya kujali jinsi mtu anavyoitathmini ,filamu hiyo ina lengo linaloeleweka; binadamu wote ni sawa, iwe barani Afrika au kati kati ya San Fransisco. Ameeleza katika makala yake kwamba mara tu udhalimu unapotajwa kwa jina, panatolewa miito juu ya kuutokomeza.

Mwandishi wa "Die Zeit" amesisitiza kwamba jambo muhimu siyo fedha nyingi, au kampeni kubwa za wanasiasa, bali ni mchango wa kila mtu.Na anauliza jee lisingekuwa jambo zuri ikiwa wahalifu kote duniani wanaingiwa wasiwasi kutokana na kampeni kama hiyo ya "You Tube"? Joseph Kony, muasi wa Uganda, analiongoza kundi la Lord's Resistance Army linalowateka nyara watoto na kuwageuza mashine za mauaji.

Gazeti la "Der Tagesspiegel" limearifu juu ya mnada uliofanyika mjini Berlin hivi karibuni kwa lengo la kukisaidia kijiji kimoja nchini Burkina Faso. Gazeti hilo limearifu kuwa mnada huo uliongozwa na msanii maarufu wa Ujerumani, Aino Laberenz,ambae ni mjane wa Christoph Schlingensief, alieuanzisha mradi wa kijiji cha sanaa za maonyesho na maendeleo nchini Burkina Faso. Watu karibu 500 walishiriki kwenye mnada huo ambapo zaidi ya Euro Millioni moja zilichangishwa.

Mwaka jana Bibi Aino Laberenz aliongezea mradi wa shule na ameliambia gazeti la "Der Tagesspiegel" kuwa sasa zahati itafuatia kwenye mradi huo uliopo karibu na mji mkuu wa Burkina Faso, Ouagadougou.

Mwandishi: Mtullya, Abdu

Mhariri: Miraji Othman