Maelfu waandamana kuomboleza kifo cha Nemtsov | Matukio ya Kisiasa | DW | 01.03.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Maelfu waandamana kuomboleza kifo cha Nemtsov

Maelfu ya watu wameandamana Jumapili (02.03.2015) mjini Moscow kuomboleza kifo cha kiongozi wa upinzani Boris Nemtsov ambaye ameuwawa kwa kupigwa risasi mjini humo.

Maelfu walioandamana Moscow kuomboleza kifo cha Boris Nemtsov. (01.03.2015)

Maelfu walioandamana Moscow kuomboleza kifo cha Boris Nemtsov. (01.03.2015)

Umma wa watu ulijipanga kwenye misururu katika daraja la Bolshoi Msokvoretsky karibu na Ikulu ya Kremlin ambapo mwanasiasa huyo mashuhuri alipigwa risasi nne na mtu asiyejulikana hapo Ijumaa usiku.

Waambolezaji walikuwa wamebeba mauwa na kupepea bendera za Urusi zilizofungwa utepe mweusi kutowa heshima zao kwa Nemtsov.Baadhi yao walikuwa wamebeba mabango yenye kuonyesha uso wake na wengine walikuwa na maadishi yenye kusema "Propaganda Inauwa".

Waandalizi wa maandamano hayo ya Jumapili miongoni mwao alikuwa ni Nemtsov mwenyewe awali walikuwa wamepanga kufanya maandamano ya kupinga sera za Rais Valdimir Putin hapo Jumapili. Walikuwa wamekubali kuyahamishia maandamano hayo katika kitongoji cha Moscow baada ya serikali ya jiji kutoruhusu yafanyike katikati ya jiji.Hata hivyo kufuatia mauaji hayo ya Nemtsov serikali ilikubali kuruhusu maandamano hayo yafanyike katikati ya jiji.

Kiongozi mwengine wa upinzani ambaye alikuwa mtu wa kwanza kuitisha maandamano hayo Alexei Navalny hakuweza kuhudhuria maandamano hayo kutokana na kwamba anatumikia siku 15 kizuizini kwa madai ya kugawa vipeperushi kinyume na sheria.

Kanda zaonyesha mauaji

Kiongozi wa upinzani Urusi Boris Nemtsov wakati wa uhai wake.

Kiongozi wa upinzani Urusi Boris Nemtsov wakati wa uhai wake.

Nemtsov ambaye aliwahi kuwa naibu waziri mkuu mwishoni mwa miaka ya 1990 chini ya utawala wa Boris Yeltsin na mkosoaji mkubwa wa Rais Valdimir Putin tokea mwaka 2000 ni mwanasiasa mashuhuri kabisa kuwahi kuuwawa katika kipindi cha Urusi baada ya kuvunjika kwa muungano wa Kisovieti.

Chaneli ya televisheni ya serikali mjini Moscow ya TV Tsentr ilionyesha mkanda wa uchunguzi wa video ambao umedokeza muuaji yumkini akawa amefyetuwa risasi kutoka lori la kusafisha barabara lililokuwa linaendeshwa kwa mwendo mdogo wakati lilipokuwa likipishana na Nemtsov.

Mkanda huo uliorekodiwa kutoka masafa ya mbali unaonyesha lori hilo likipishana na vivuli vya watu wawili waliokuwa wakitembea kwa miguu ambao inaaminika kwamba walikuwa ni Nemtsov na rafiki yake wa kike.

Wakati lori hilo lilipowapita mpita njia mmoja tu alibakia na kuna mtu alieonekana akikimbia kutoka kwenye lori hilo kuelekea kwenye gari linalopita ambalo lilisimama katikati ya barabara na kumpakia mtu huyo kabla halijaondoka kwa haraka.

Tuhuma za wachunguzi

Umma uliofurika katikati ya Moscow kuomboleza kifo cha Boris Nemtsov. (01.03.2015

Umma uliofurika katikati ya Moscow kuomboleza kifo cha Boris Nemtsov. (01.03.2015)

Wachunguzi hawakuzungumzia mkanda huo hapo Jumapili. Kamati ya Uchunguzi ya Urusi ambacho ni kitengo chenye nguvu kubwa kinachoripoti moja kwa moja kwa Putin ilidokeza hapo Jumamosi kwamba Nemtsov anaweza kuwa ameuwawa na wanachama wa upinzani wanaotaka kuiyumbisha nchi.Awali Putin alisema kupitia msemaji wake kwamba uhalifu huo ulikuwa ni uchokozi.

Kamati hiyo ya Uchunguzi pia imesema kwamba uhalifu huo yumkini ukawa unahusiana na Waislamu wa itikadi kali kwa sababu ya shutuma za Nemtsov dhidi ya shambulio la kijarida cha dhihaka cha Ufaransa Charlie Hebdo au kutoka kwa watu wa misimamo mikali wa pande zote mbili za mzozo ndani ya Ukraine.

Wafuasi wa upinzani na waangalizi huru wamepuuza madai hayo ya wachunguzi na kuelezea hofu yao kwamba mauaji hayo yatachochea umwagaji damu zaidi wa kisiasa nchini humo ambapo serikali na vyombo vya habari inavyovidhibiti vinatowa sura ya wapinzani kama vibaraka wa mataifa ya magharibi.

Nemtsov amekuwa mkosoaji mkali wa sera za Urusi kwa Ukraine na amekuwa akimshutumu Putin kwa kuendesha vita visivyotangazwa katika nchi hiyo jírani.

Mara kwa mara amekuwa akitangazwa kuwa "adui wa wananchi" na wafuasi wa serikali wa misimamo mikali ambao hivi karibuni wameanza kuandaa vuguvugu dhidi ya Maidan uwanja wa uhuru ulioko Kiev ambao ulikuwa chimbuko la mapinduzi ya Ukraine mwaka mmoja uliopita.

Mwandishi : Mohamed Dahman/dpa/AFP

Mhariri : Daniel Gakuba

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com