1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Machafuko yagubika uchaguzi wa rais Algeria

Oumilkheir Hamidou
12 Desemba 2019

Baada ya maandamano ya miezi kadhaa yaliyomng'owa madarakani rais Bouteflika Waalgeria wanapiga kura katika uchaguzi uliogubikwa na machafuko na unaoangaliwa kama mbinu za kuwarejesha madarakani viongozi wa zamani

https://p.dw.com/p/3UhYA
Algerien Präsidentschaftswahl
Picha: picture-alliance/AP/D. Cole

Machafuko yameripotiwa katika jimbo la kaskazini la Kabylie ambako vituo visivyopungua viwili vya uchaguzi vilifungwa huko Bejaia na kimoja kuvunjwa. Kituo cha tatu bado kinazingirwa na wanaharakati wanaopinga uchaguzi huo wa rais.

Mjini Tizi Ouzou, mji mkubwa wa jimbo hilo la milimani wanakoishi watu wa kabila la Berber, harakati zote za kupiga kura zimesitishwa.

Mjini Algiers, mji mkuu wa Algeria vikosi vya kuzuwia fujo vimetumia nguvu kuwatawanya waandamanaji zaidi ya elfu kumi wanaopinga uchaguzi huo wa rais wanaosema umelengwa kuirejesha madarakani serikali ya rais aliyepinduliwa Abdulaziz Bouteflika. Mashahidi wanasema wanaharakati kadhaa wamekamatwa ili kuzuwia mikururo mikubwa zaidi ya watu kuandamana. Hata hivyo waandamanaji wamefanikiwa kuvunja vizuwizi vilivyowekwa na polisi katika uwanja wa jengo kuu la posta - kitovu cha vuguvugu la "Hiraki" au vuguvugu la maandamano yanayoitikisa Algeria tangu mwezi Februari uliopita.

Waandamanaji wanaopinga uchaguzi wa rais
Waandamanaji wanaopinga uchaguzi wa raisPicha: Reuters/R. Boudina

Matokeo hayategemewi kutangazwa kabla ya ijumamosi

Mbali na maandamano, katika vituo vya kupiga kura mjini Algiers, baadhi ya vijana wameteremka vituoni mapema kupiga kura wakisema "ni jukumu lao.""Nnapiga kura kwasababu naogopa nchi yetu isije ikatumbukia katika janga la mashaka" anasema Karim, mwenye umri wa miaka 28, huku Mahdi Said mwenye umri wa miaka 76 akionyesha kadi yake ya kupiga kura iliyojaa mihuri: "daima nimekuwa nikipiga kura, na leo pia nimepiga kura, ni wajib."Anasema.

Idadi ya wapiga kura katika uchaguzi huo wa rais ilifikia asili mia 7.92 mnamo saa tano za mchana saa za Algeria au, saba kwa saa za Afrika Mashariki. Katika uchaguzi wa rais mwaka 2014 idadi ya walioteremka vituoni wakati kama huo ilifikia asili mia 9.15.

Idadi kubwa ya wasimamizi wa uchaguzi wanaashiria wapigakura wengi hawatoteremka vituoni. Wagombea wote watano wa kiti cha rais wanatajwa na waandamanaji kuwa "watoto wa mfumo" na wanatuhumiwa kutumikia masilaha ya watawala wa zamani.

Vituo vya kupiga kura vitafungwa saa tatu za usiku kwa saa za Afrika mashariki na matokeo yatatangazwa pengine jumamosi au baadae