1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Machafuko yaendelea Thailand

P.Martin2 Septemba 2008

Licha ya kutangazwa hali ya hatari ,Mkuu wa majeshi Jemadari Anupong Paochinda amesema,hawatotumia nguvu kuwatoa wapinzani waliovamia ofisi ya waziri mkuu.Amesema,matumizi ya nguvu huenda yakasababisha machafuko zaidi

https://p.dw.com/p/FACp
Demonstration gegen Regierung in Thailand Bangkok Anti-government demonstrators sleep Monday, Sept. 1, 2008, in front of gates to Government House in Bangkok, Thailand. Several Thai politicians at an extended parliamentary debate on how to end anti-government protests have joined demonstrators occupying the prime minister's office in calling for his resignation, but a confident Samak Sundaravej insists he will keep the reins of power. (AP Photo/David Longstreath)
Wapinzani wa serikali wakilala mbele ya jengo la serikali mjini Bangkok, Thailand 01 Septemba,2008.Picha: AP

Waziri Mkuu wa Thailand Samak Sundaravej alipoamua kutangaza hali ya hatari baada ya machafuko kusababisha kifo kimoja na kujeruhi watu 45, aliutetea uamuzi wake kwa kusema:

"Maisha yataendelea kama kawaida.Lakini tuna wajibu wa kuchukua hatua dhidi ya kile kilichotokea katika ofisi ya waziri mkuu.Njia pekee ya kuutenzua mgogoro huo ni kutangaza hali ya hatari. "

Lakini jeshi likisita kutumia nguvu dhidi ya wandamanaji,yadhihirika kuwa mgogoro huo hautomalizika upesi hivyo.Isitoshe,chama kikuu cha wafanyakazi kimeitisha mgomo kuanzia siku ya Jumatano na hivyo kuhatarisha huduma za kijamii.Machafuko hayo yanahatarisha vile vile sekta ya utalii iliyo muhimu sana kwa uchumi wa Thailand.Tayari baadhi ya serikali za kigeni zimewashauri raia wake kujiepusha kwenda Thailand mpaka hali ya utulivu itakaporejea nchini humo.Vile vile kuna hofu kuwa ghasia hizo huenda zikazuia uwekezaji wa kigeni.Thamani ya sarafu ya Thailand- Baht imepunguka kwa asilimia 24 tangu kuanza kwa upinzani huo hapo mwezi Mei.

Juu ya hivyo,wapinzani wa serikali ya Samak wanawahimiza wenzao kuandamana barabarani huku vikosi vya usalama vikipiga doria kuzuia mapambano kati ya makundi ya wafuasi na wapinzani wa serikali.Wakati huo huowapinzani walioivamia ofisi ya waziri mkuu wanasema,wao watabakia katika jengo hilo mpaka Samak atakapojiuzulu.

Hilo si tatizo pekee linalomkabili Samak kwani hii leo kiongozi huyo amepata pigo jipya,baada ya Kamisheni ya Uchaguzi kutoa wito kwa Mahakama ya Katiba nchini humo kukivunja chama tawala cha PPP kwa sababu ya udanganyifu wa uchaguzi.Kwa mujibu wa Kamisheni hiyo,chama cha waziri mkuu Samak kilinunua kura kabla ya uchaguzi wa mwezi Desemba.Mahakama huenda ikachukua muda kupitisha uamuzi wake,lakini ikiwa itakubaliana na Kamisheni ya Uchaguzi,basi Samak na viongozi wengine waandamizi katika chama chake watapigwa marufuku kushiriki katika uwanja wa kisiasa kwa kipindi cha miaka mitano.