Maandamano yaitikisa Burkina Faso | Matukio ya Kisiasa | DW | 28.10.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Maandamano yaitikisa Burkina Faso

Wapinzani wameanza maandamano ya wiki nzima.Maanfdamano hayo yanafanyika kupinga hatua ya rais Blaise Compaore ya kutaka kurefusha muda wake madarakani baada ya kuiongoza nchi hiyo kwa miaka 27.

Kiongozi wa Upinzani Zephirin Diabre akiongoza maandamano

Kiongozi wa Upinzani Zephirin Diabre akiongoza maandamano

Hali nchini Burkina Faso imeanza kuwa tete,vijana wamepambana na vikosi vya usalama mapema hii leo ikiwa ni siku ya kwanza ya maandamano yaliyopangwa kufanyika kwa wiki nzima.Maanfdamano hayo yanafanyika kupinga hatua ya rais Blaise Compaore ya kutaka kurefusha muda wake madarakani baada ya kuiongoza nchi hiyo kwa miaka 27.

Vikosi vya usalama katika mji mkuu wa Burkina Faso,Ougadougou wamelazimika kuwatawanya vijana waliofunga barabara kuu ya nchi hiyo,wakitumia gesi ya kutoa machozi dhidi ya vijana hao waliojibu kwa kuwarushia mawe kutoka kila kona ya mji huo.Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na mwandishi habari wa shirika la habari la ufaransa AFP mapambano hayo yalianza alfajiri ya leo na yalipangwa na makundi ya upinazni dhidi ya kile walichokiita mapinduzi ya katiba yanayofanywa na wafuasi wa rais Blaise Compaore.

Rais Blaise Compaore

Rais Blaise Compaore

Kufuatia hali hiyo shule zote pamoja na vyuo vikuu vimefungwa kuanzia hii leo hadi muda wa wiki nzima huku upinzani ukiapa kupambana na hatua hiyo ya rais kujiongezea muda wa kubakia madarakani zaidi ya utawala wake wa miaka 27.Bunge la nchi hiyo linatarajiwa siku ya alhamisi kutathmini mapendekezo ya kufanyiwa marekebisho katiba ambayo yatatowa nafasi ya kipindi cha uongozi kuongezwa na kwahivyo kumruhusu rais Compaore kugombea tena uchaguzi kwa muhula mwingine wa miaka mitano pindi uchaguzi ukifanyika mwaka ujao.

Hatua hiyo ya rais Compaore ya kutaka kubakia madarakani imewakasirisha wapinzani na zaidi umma wa taifa hilo ikiwemo vijana wengi katika nchi ambayo asilimia 60 ya idadi ya raia wake milioni 17 ni vijana walioko chini ya umri wa miaka 25.Waandamanaji wenye hasira wamezifunga barabara na kuchoma moto matairi katika mji mkuu wa taifa hilo tangu lilipotangazwa pendekezo hilo la kubadilishwa katiba mnamo Oktoba 21,huku yakishuhudiwa pia maandamano ya wanawake waliojitokeza kwa wingi hapo jana jumatatu wakiwa wamebeba miko ya kupikia kitu ambacho nchini humo kinaangaliwa kama ishara nzito ya kuudhika kwa wanawake.

Maandamano ya mjini Ougadogou

Maandamano ya mjini Ougadogou

Tangu siku ya ijumaa wanafunzi walionekana kutoroka madarasani na kujiunga na maandamano hayo hali iliyosababisha kuvurugika kwa shughuli nyingi katika mji mkuu Ougadougou.Aidha mashirika ya kiraia yametowa mwito pia wa kufutwa kwa mpango huo wa kutaka kuibadili katiba yakisema nchi hiyo inakabiliwa na kitisho cha kulezwa ikiwa hatua hiyo itaendelea.Pamoja na hayo upinzani umewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kulizingira bunge ili kuwazuia wabunge katika shughuli ya kutathmini mpango huo.Itakumbukwa kwamba Compaore amekuwa madarakani tangu alipoongoza mapinduzi mwaka 1987 na amechaguliwa kuingia madarakani mara nne tangu mwaka 1991.

Miongoni mwa wanasiasa waliojitenga na campaore na kujiunga na upinzani ni Waziri wa zamani wa mambo ya nchi za nje Ablasse Ouedraogo.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Mohammed AbdulRahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com