Maandalizi ya msimu mpya wa Bundesliga | Michezo | DW | 04.08.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Maandalizi ya msimu mpya wa Bundesliga

Huku kipindi cha mapumziko cha ligi ya kandanda ya Ujerumani Bundesliga kikikaribia kufikia mwisho na ligi hiyo ikitarajiwa kuanza Ijumaa Agosti 22, timu zinaendelea kufanya maandalizi kwa kuwasajili wachezaji wapya.

Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Uswisi, Haris Seferovic, mwenye umri wa miaka 22, ameondoka klabu yake ya Real Sociedad ya Uhispania na kujiunga na Eintracht Frankfurt ya Ujerumani kwa mkataba hadi mwaka 2017. Seferovic, ambaye alifunga bao la ushindi la Uswisi dhidi ya Ecuador katika mashindano ya kombe la dunia la kandada yaliyofanyika nchini Brazil mwezi Juni na Julai, ni mchezaji wa tatu wa safu ya mashambulizi kusaini mkataba na Eintracht Frankfurt msimu huu wa kiangazi akiwafuata Nelson Valdez kutoka Paraguay na Mbarzil Lucas Piazon.

Seferovic, ambaye ni wa asili ya Bosnia, alikuwa na miaka mitatu bado na klabu hiyo ya Uhispania. Vyombo vya habari vya Ujerumani vimeripoti kuwa Eintracht Frankfurt imelipa kiasi cha euro milioni tatu kumpata mshambuliaji huyo. Timu hiyo, ambayo msimu huu wa kiangazi ilimteua kocha wa zamani wa Werder Bremen, Thomas Shaaf kuwa kocha mpya, itaanza michuano ya Bundesliga dhidi ya Freiburg mnamo Agosti 23.

Wakati huo huo, timu ya Schalke imetangaza siku ya Ijumaa kwamba winga wa timu hiyo, Sydney Sam, amepata jeraha kwenye msuli wa sehemu ya nyuma ya mguu wake. Sam, mwenye umri wa miaka 26,alijiunga na Schalke akitokea Bayer Leverkusen, lakini maandalizi yake kwa ajili ya msimu ujao wa Bundesliga yatakwamishwa na jeraha hilo. Wikendi hii Schalke inaandaa mashindano ya kifariki yatakayozijumuisha timu nne, zikiwemo Newcastel na West Ham kutoka England na Malaga kutoka Uhispania.

Mwandishi: Josephat Charo/AFP/APE
Mhariri: Bruce Amani