Loew ana imani na timu ya Ujerumani | Michezo | DW | 28.05.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Loew ana imani na timu ya Ujerumani

Kocha wa kandanda timu ya taifa ya Ujerumani Joachim Loew asema ana imani kikosi chake kitakuwa tayari kwa mechi ya kwanza wakati wa mashindano ya kombe la mataifa ya Ulaya.

Kocha wa Timu ya Tiafa ya Ujerumani akiwa kazini

Kocha wa Timu ya Tiafa ya Ujerumani akiwa kazini

Akiwapa matumaini mashabiki baada ya kufungwa na Uswisi katika mechi ya kirafiki.Wakati wimbi la kupambana na rushwa na upangaji matokeo katika ligi ya soka nchini Italia, na bingwa wamaratano wa masumbwi duniani Jonny Tapia afariki dunia .

Mashabiki wa kandanda barani Ulaya na sehemu nyengine za dunia, wanasubiri kwa hamu mashindano ya fainali za kombe la mataifa ya Ulaya 2012 yatakayoanza tarehe 8 mwezi ujao wa Juni nchini Ukraine na Poland nchi mbili waandalizi wa mashindano hayo. Pamoja na hayo tayari makocha wa timu kadhaa wameanza kuangalia wapi pa kurekebisha mambo , baada ya machuano ya kirafiki ya kujipima nguvu iliofanyika mwishoni mwa Juma.

Harakati za micherzo

Haraka za michezo

Tukiitupia jicho baadhi ya michuano hiyo, Kocha mpya wa England Roy Hodgson ameanza vizuri kibarua chake baada ya England kuibwaga Norway bao moja kwa bila,bao lililopachikwa na Ashley Cole. Kikosi cha kwanza cha Hudgson kiliwajumuisha nahodha Steven Gerrad na wenzake kutoka timu yake ya Liverpool Steward Downing na Andy Caroll.

Ilikuwa ni mara ya kwanza England inaishinda Norway nyumbani kwao mjini Oslo katika kipindi cha miaka 32. Baada ya pambano hilo Hudgson alisema pambano lao lilikuwa zuri na kwamba pamoja na hayo atahitaji marekebisho madogo ya ahapa na pale katika kikosi chake. Mechi ya kwanza ya England itakuwa dhidi ya Ufaransa mjini Donezk nchini Ukraine Juni 11.

Kwa upande wake Ufaransa ilikuwa na kibarua kigumu nyumbani mjini Valenciennes , katika mchuano wake wa kirafiki dhidi ya Iceland. Kulikuwa na hali ya kuzorota kwa ngome ya Ufaransa na hasa mchezaji Patrice Eva ambaye makoasa yake yaliipa mwanya Icealand kutingisaha mabao mawili. Wakati zikiwa sare mabao mawili kwa mawili na kubakia dakika 3 na mchezo kumalizika, Ufaransa ikajipatia bao la ushindi lililopachikwa na mchezaji wa kiungo Adil Rami.

Pambano jengine la kujipima nguvu kwa kikosi hicho cha Les Blues cha kocha Laurent Blanch ni hapo Alhamisi wakati Ufaransa itakapoumana na Serbia mjini Reims. Blanc atahitaji kukipunguza kikosi chake cha wachezaji 25 hadi 23 kabla ya kuelekea Ukraine.

Kocha wa Ujerumani Joachim Loew anasema ana matumaini wachezaji wake watafanya vizuri katika mashindano ya kombe la Ulaya, licha ya kufungwa na Uswisi katika mechi ya kirafiki mabao 5-2 mjini Basel. Ni mara ya kwanza Ujerumani inafungwa na Uswisi tangu 1956. Akizungumza na waandishi habari baadae Loew alisema amevunjwa moyo na matokeo lakini akifahamu tangu awali kawamaba hii ni hatua ya mazoezi na imewapa nafasi ya kuona pale panapohitaji marekebisho . Mswisi Eren Dersiyok alilioana lango la Ujerumani mara tatu.

Kikosi cha Ujerumani hakikuwa na kundi la wachezaji kutoka kilabu ya Bayern Munich. Wachezaji wanane wa Bayern wamo katika kikosi cha Ujerumani kwa ajili ya mashindano hayo ya Euro 2012 , lakini walikuwa wamepewa mapumziko ya siku chache baada ya kushindwa katika fainali ya kombe la vilabu bingwa kwa mikwaju ya penalti na Chelsea ya Uingereza .

Ujerumani itajipima tena nguvu katika mechi nyengine ya kirafiki mjini Leipzig hapo Alhamisi itakapoumana na Israel. Katika fainali za kombe la Euro 2012 Ujerumani iko katika kundi gumu linalozijumuisha pia Ureno, Uholanzi na Denmark.

Taarifa nyengine za kandanda

Mshambuliaji Claudio Pizarro anarudi katika kilabu yake ya zamani Bayern Munich ya Ujerumani baada ya miaka mitano, akisaini mkataba wa mwaka mmoja. Lengo ni kuimarisha kikosi cha mashambulizi. Pizarro kutoka Peru ambaye ametokeza kuwa mfungaji magoli bora wa kigeni katika ligi kuu ya Ujerumani Bundesliga na mwenye umri wa miaka 33 anajiunga tena na Bayern baada ya kuwa na Werder Bremen kwa miaka mitatu na amefunga jumla ya mabao 160 katika mechi zake 333 za Bundesliga. Aliwahi kuichezea bayern 2001 hadi 2007 kabla ya kujiunga na Chelsea.

Nchini Italia Wimbi la rushwa na upangaji matokeo lingali likiiandama ligi kuu ya nchi hiyo Seria A. Leo polisi ilimtia nguvuni nahodha wa kilabu ya Lazio Stefano Mauri pamoja na kuivamia kambi ya timu ya taifa ya Italia kwa ajili ya mshindano ya kombe la mataifa ya Ulaya Euro 2012. Hatua ya polisi inahusiana na uchunguzi unaoendelea kuhusu upangaji matokeo ya mechi. Pia polisi imemuarifuz meneja wa mabingwa wa soka Juventus Turin Antonio Conte kwamba naye anachunguzwa.

Mlinzi wa timu ya taifa Domenico Criscito anayechezea mabingwa Urusi Tenit ya St Petersburg pia amearifiwa anachunguzwa na polisi, pale walipowasili katika kam,bi ya timu ya taifa ya Italia. Mchezaji huyo anatarajiwa kuwemo katika kikosi cha mwisho cha wachezaji 23 cha Kocha Cesare Prandelli, kwa ajili ya mashindano hayo ya Euro 2012. Prandelli anatarajiwa kutangaza kikosi chake kamili baadae.

Mojawapo ya harakati za mchezaji Steve Gerrad

Mojawapo ya harakati za mchezaji Steve Gerrad

Katika ringi ya mabondia Muingereza Carl Froch alifanikiwa kulitwaa taji la ubingwa wa wizani wa kati wa Super middle katika shirikisho la ndondi la kimataifa IBF alipomzuwia Lucian Bute wa Rumania mwenye umri wa miaka 32 aliyekuwa akilishikilia taji hilo. Froch mwenye umri wa miaka 34 alikuwa akipigana nyumbani mjini Nottingham na ushindi huo kumfanya kuwa bingwa mara tatu wa dunia baada ya mataji yake mawili ya awali katika shirika la ndondi la WBC.

Naye Bingwa wa zamani Muingereza Amir Khan atapigana na Mmarekani asiyeshindwa hadi sasa katika uzani mwepesi light welter Danny Garcia Julai 14, kuwania taji la shirika la ndondi la World Boxing Council -WBC.

Pambano hilo litafanyika mjini Los Angeles au Las Vegas Awali pambano kati ya Khan na Lamont Peterson tarehe 19 mwezi huu lilifutwa baada ya Peterson aliyemshinda Khan katika mazingira ya kutatanisha na kushinda taji la WBA la Super light weight na lile la IBF la Light welter, kuonekana ametum,ia madawa ya kuimarisha misuli yaliopigwa marufuku.

Taarifa ya kusikitisha katika ulimwengu wa ndondi , ni kifo cha bingwa mara tano wa dunia Johnny Tapia aliyeafariki dunia nyumbani kwake mjini Albuquerque huko New Mexico Marekani jana . Mmoja wa jamaa zake aligundua marehemu amefariki baada ya kufika nyumbani kwake na hivyo kuiarifu polisi.

Tapia aliyekuwa na umri wa miaka 45 alishinda mataji kadhaa ya super fly, bantam na feather tangu alipoanza kupigana ndondi za kulipwa 1988. Mwaka 2007 alilazwa hospitali kwa kile kilichotajwa kuwa huenda ni matumizi ya kupita mpaka ya madawa ya kulevya. Pambano lake la mwisho lilikuwa mwezi Juni mwaka jana lipomshinda Mauricio Pastarana mjini Albuquerque katika raundi ya nane.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman

Mhariri: Mohamed Khelef