Liverpool kukabidhiwa kombe lililiwaponyika miaka 30 sasa
20 Julai 2020Liverpool haihitaji tena kusaka pointi za ligi nchini England lakini kukabidhiwa taji lao la kwanza la Premier League siku ya Jumatano katika uwanja wao wa Anfield itakuwa tukio lenye hisia kali kwao pamoja na mashabiki wao. Premier League inakunja janvi wiki hii , Juventus Turin itanyakua taji lake la tisa mfululizo la Serie A iwapo itashinda michezo yake mitatu katika muda wa siku saba, wakati huo huo nchini Ufaransa taratibu shughuli viwanjani zinaanza kurejea kwa mtanange wa fainali ya kombe la nchi hiyo kati ya Paris Saint-Germain na St Etienne siku ya Ijumaa.
nahodha wa Liverpool Jordan Hernderson huenda ni majeruhi lakini atakuwa tayari kulinyanyua juu kombe la ubingwa wa ligi siku ya Jumatano na sherehe maalum katika uwanja wa Anfield zitafanyika baada ya mchezo dhidi ya Chelsea.
Hapa Ujerumani machampioni wa Bundesliga mara nane mfululizo Bayern Munich pamoja na RB Leipzig wanarejea katika kambi za mazowezi baada ya wiki kadhaa za mapumziko baada ya msimu wa ligi ya Ujerumani kumalizika mwishoni mwa mwezi uliopita.
Leipzig tayari wanafahamu watapambana na Atletico Madrid katika awamu ya robo fainali ya michuano hiyo itakayofanyika kwa mfumo wa mtoano mjini Lisbon, wakati Bayern itabidi kwanza kukamilisha kazi ya awamu ya timu 16 dhidi ya Chelsea, baada ya kushinda mchezo wa mkondo wa kwanza kwa mabao 3-0.
Manchester United inapaswa kumbadilisha mlinda mlango wake David de Gea na kumpa nafasi mlinda mlango mwingine Dean Henderson msimu ujao, mshambuliaji wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza Alan Shearer alisema baada ya Mhispania De Gea kufanya makosa kuonesha mchezo wa kukatisha tamaa katika kipigo cha mabao 3-1 katika nusu fainali ya kombe la AF jana Jumapili dhidi ya Chelsea, na kuwa gumzo la mashabiki na viongozi nchini Uingereza.
Mlolongo wa makosa
Mlolongo wa makosa aliyofanya De Gea umesababisha miito ya kutaka kumbadilisha kutoka chaguo la kwanza na kumsimamisha Henderson katika lango la Manchester, baada ya kuonesha umahiri akilinda lango la Sheffield United.
Lakini kocha wa Chelsea Frank Lampard alimtetea De Gea kwa kusema:
"Sio kwasababu namheshimu sana De Gea kama mlinda mlango. Nafahamu watu kila mara watamshambulia mlinda mlango wakati akifanya makosa kama yale, kwasababu wanamkosoa. Lakini kile nilichofanya ni kumwambia Mason Mount wakati wa mapumziko kwamba nataka kuona akipiga mashuti kuelekea golini zaidi. Alipiga shuti moja kipindi cha kwanza , alijaribu kama kuupiga kwa kuuzungusha na kwangu mimi, unapaswa kujaribu nje ya box dhidi ya walinda mlango wa kiwango cha juu, na De Gea ni mlinda mlango wa kiwango cha juu, unapaswa kupiga mikwaju kwenye kundi la walinzi.Ni kweli kwamba hakukamata vizuri na ukaingia wavuni na huenda hilo ni kosa."
Kocha wa Manchester United Ole Gunnar Solskjaer alimueleza De Gea kama mtu shupavu baada ya mchezo huo, lakini mlinzi wa zamani wa klabu hiyo Phil Neville alisema mlinda mlango huo hajiamini. Ole Gunnar Solskjaer alikuwa na haya ya kusema kuhusu mlinda mlango wake David de Gea baada ya kufanya makosa na kuizawadia Chelsea ushindi mnono wa fainali ya FA.
"Kila mmoja anapaswa kucheza vizuri na kila mmoja ana fursa kila mara kucheza ili kuonesha mchango wake kwa timu. David anafahamu alipaswa kuokoa goli la pili, lakini imekwisha tokea. Tunapaswa kusonga mbele. Tunapaswa kuangalia mbele kwa ajili ya michezo ya Jumatano. Unaweza kuona, ni vigumu kwa mlinda mlango kujisahihisha, mbali na David kuokoa kwa ustadi wa hali ya juu mara mbili, mara tatu baadaye."