Leverkusen yapanda hadi nafasi ya pili | Michezo | DW | 29.01.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Leverkusen yapanda hadi nafasi ya pili

Mshambuliaji chipukizi Leon Bailey alionyesha kwa nini Arsenal na Chelsea wanaripotiwa kumnyemelea wakati alifunga bao safi sana katika ushindi wa mabao mawili kwa sifuri wa Bayer Leverkusen dhidi ya Mainz

Bailey mwenye umri wa miaka 20, hata hivyo amewahakikishia mashabiki wa Leverkusen kuwa wataendelea kumuona uwanjani hadi mwishoni mwa msimu. Ushindi huo umeipandisha Leverkusen hadi nafasi ya pili, na pengo la pointi 16 nyuma ya mabingwa watarajiwa Bayern Munich. Heiko Herrlich ni kocha wa Leverkusen "Tuliudhibiti vyema mpira, tukawa na nafasi nyingi. Katika kipindi cha kwanza, nafasi mbili, katika kipindi cha pili, nafasi tatu. Na tungeweza kufanya mashambulizi mawili matatu hivi ya kushutukiza baada kuwa kifua mbele mabao mawili kwa bila. Lakini nadhani tuliwadhibiti Mainz ambao walijilinda vizuri katika kipindi cha kwanza. Ilikuwa vigumu sana kwetu kupenya kwenye eneo la hatari lakini tuweza kushambulia vizuri, na ni vyema kuwa tulitumia counterattack na ndio maana ushindi wetu unafaa".

Fußball: Bundesliga - Bayern München vs TSG 1899 Hoffenheim (Reuters/M. Rehle)

Lewandowski alifunga bao lake la 18 msimu huu

Siku ya Jumamosi Robert Lewandowski alifunga bao lake la 18 la ligi msimu huu, wakati Bayern Munich iliirarua Hoffenheim mabao matano kwa mawili. Sandro Wagner pia alifunga bao lake la kwanza tangu alipojiunga na timu hiyo kutoka kwa Hoffenheim. Florian Grillitsch ni kiungo wa Hoffenheim "Bila shaka ni vizuri wakati ukiwa kifua mbele hapa Munich kwa mabao mawili kwa sifuri. Lakini bayern walifanya kazi nzuri sana na kutumia wachezaji wao bora na wakafunga mabao mawili ya kawaida, na kweli tunapaswa kulinda lango letu vizuri".

VfB Stuttgart waliamua kumpiga kalamu kocha wao Hannes Wolf, baada ya kichapo cha mbili bila dhidi ya nambari tatu Schalke, matokeo ambayo yaliwateremsha hadi nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi. Mshambuliaji wa Stuttgart Daniel Ginczek alielezea kusikitika kwake na matokeo hayo "Ulikuwa mchezo ambao haukuwa na kitu cha kutuzia kucheza vizuri. Tulifungwa moja bila na kisha tukapata upungufu na mambo yakawa magumu kwetu dhidi ya Schalke. Tulihisi hata kama tungecheza kwa masaa mawili hatungeweza kufunga bao".

Leverkusen wako juu ya Schalke na tofauti ya mabao, wakati Eintracht Frankufurt wako katika nafasi ya nne na pengo la pointi moja. Borussia Dortmund wako katika nafasi ya sita baada ya kutoka sare ya mabao mawili kwa mawili na SC Freiburg mechi ambayo DW Kiswahili ilikuletea live kutoka Signal Iduna Park

Fußball Bundesliga | 20. Spieltag | Borussia Dortmund - SC Freiburg (Reuters/L. Kuegeler)

Pietersen alifunga bao kutoka katikati ya uwanja

Mshambuliaji Pierre-Emerick Aubameyang alionyesha mchezo mbaya na alizomewa na mashabiki baada ya kuwachwa nje katika mechi mbili za awali. Dortmund ilizomewa na mashabiki wake na kocha Peter Stoeger alikiri kuwa hakufurahishwa na alichokiona uwanjani "Labda ukiachilia mbali dakika 15 za kwanza, unaweza kusema tu mwishowe kuwa – hata kama hautaki kuskia hilo – tunapaswa kuridhika na pointi moja. Kwa kipindi kirefu cha mchezo tulicheza dhidi ya mpinzani aliyejopanga vizuri, mpinzani imara, mwenye nia ya kupambana. Tuna mahitaji yetu ya kufuzu katika champions league. Tulipaswa kutimiza hilo uwanjani na leo hatukuweza kufanya hivyo".

Katika mechi nyingine ya jana, Wolfsburg ilipata ushindi wa bao moja kwa sifuri dhidi ya Hanover 96. Ulikuwa ushindi wa tatu pekee wa Wolfsburg katika mechi zao tisa za mwisho za Bundesliga na uliwaweka katika nafasi ya 13 wakati Hanover wako katika nafasi ya 10.

Hamburg SV ilitoka sare ya bao 1-1 na RB Leipzig 1-1 wakati Augsburg ilitoka nyuma na kulazimisha sare ya 1-1 na washika mkia FC Cologne. Hertha Berlin na Werder Bremen walishindwa kufungana bao.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu