1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leverkusen, Dortmund zaona vimulimuli

27 Januari 2014

Ilikuwa ni wikendi yenye kisirani kwa mahasimu wa viongozi wa ligi Ujerumani Bundesliga, baada ya Bayer Leverkusen na Borussia Dortmund kushindwa kupunguza pengo baina yao na viongozi Bayern

https://p.dw.com/p/1Axs4
SC Freiburg - Bayer Leverkusen
Picha: picture-alliance/dpa

Bayern Jumamosi walijiweka imara kileleni kwa kuendeleza walikowachia katika duru ya kwanza ya msimu, walipowanyamazisha Borussia Moenchengladbach kwa kuwafunga magoli mawili kwa sifuri. Vigogo hao sasa wanashikilia usukani wakiwa na pointi 47 baada ya kutoshindwa mchuano mmoja kati ya mechi zao 42 mfululizo, na hivyo kuweka pengo la pointi 10 dhidi ya nambari mbili Leverkusen walioshindwa mabao matatu kwa mawili na Freiburg.

Na pengo hilo huenda likapanuka hata zaidi mwishoni mwa siku ya Jumatano wiki hii, wakati Bayern itakaposhuka dimbani kucheza mchuano uliopangwa upya dhidi ya Stuttgart, ambao hawakucheza wakati wlaipokuwa nchini Morocco kucheza katika dimba la kombe la Klabu bingwa duniani, ambalo walikuja nalo mjini Munich. Thomas Müller ndiye aliyefunga goli la pili kupitia mkwaju wa penalty "Tayari tulifahamu kwamba Gladbach hawangeweza kuudhibiti mpira kwa zaidi ya dakika 90 kwa sababu sisi tunawazidi na tunautafuta mpira kwa haraka. Kulikuwa na tukio la mchezaji kuunawa mpira, tukajikinga vyema, kipa wetu Manuel Neuer akawa mzuri na hata wakawa na bahati mbaya kwamba mpira uligonga mwamba. Kwa jumla tulikuwa timu bora, lakini Gladbach wameonyesha kuwa wanaweza kupambana".

Mchezaji wa Dormtund Jakub Blaszczykowski atakuwa nje katika kipindi kilichosalia cha msimu kutokana na jeraha
Mchezaji wa Dormtund Jakub Blaszczykowski atakuwa nje katika kipindi kilichosalia cha msimu kutokana na jerahaPicha: picture-alliance/dpa

Mlinda lango wa Gladbach Marc-André ter Stegen alikiri kuwa wapinzani wao Bayern walikuwa moto wa kuotea mbali. "Ni wazi Bayern ilikuwa timu bora kutuliko, lazima ukubali. Walifunga goli mapema na hivyo ikawa vigumu kwetu. Wakati Bayern wanaongoza moja bila, inakuwa vigumu. Tulijaribu kwa muda mrefu kuyaweka mambo sawa lakini hilo halikuwezakan, lakini nadhani kwetu sisi hatuhitaji kushindana na Bayern Munich. Kuna mechi nyingi sana ambazo ni muhimu kwetu".

Borussia Dortmund ilishindwa kuizuia Augsburg katika mechi iliyoishia sare ya kufungana magoli mawili kwa mawili na hivyo vijana hao wanjano wakasalia katika nafasi ya tatu na pointi 33 , ikiwa ni nne nyuma ya nambari mbili Leverkusen.

Mshambuliaji wa Schalke Klaas-Jan Huntelaar alirejea kwa kishindo baada ya kupona jeraha
Mshambuliaji wa Schalke Klaas-Jan Huntelaar alirejea kwa kishindo baada ya kupona jerahaPicha: picture-alliance/dpa

Schalke 04 ilisonga hadi nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi, ikiwa na pointi 31 huku Klaas-Jan Huntelaar akitikisa wavu katika mechi hiyo iliyokuwa yake ya kwanza baada ya kurejea kutoka mkekani kw amiezi mitano na kuwasaidia vijana hao wa samawati kuwabwaga Hamburg mabao matatu kwa sifuri. Huyu hapa Huntelaar akizungumza baada ya kuulizwa kama anaridhika na hali yake baada ya kupona jeraha. "Ndiyo nimeridhika. Nimeweza kucheza kwa dakika 75 baada ya kuugua jeraha wka muda mrefu. Nimekuwa nikisubiri sana kurejea tena katika hali hii. Kwa hivyo nikafanya mazoezi na kwa kuanza na ushindi ni vizuri kabisa bila shaka".

Werder Bremen ilitekwa kwa sare ya sifuri kwa sifuri na washika mkia Eintracht Braunschweig. Katika mechi nyingine za Jumamosi, Nuremberg iliifunga Hoffenheim magoli manne kwa sifuri ikiwa ndio ushindi wao wa kwanza kabisa msimu huu, wakati nayo Hannover ikiicharaza Wolfsburg magoli matatu kwa moja. Mainz ilisajili ushindi wa mabao mawili kwa moja dhidi ya Stuttgart. Na Eintracht Frankfurt ikaizaba Hertha Berlin bao moja kwa sifuri.

Mwadishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman