Leicester wabanduliwa, City wapepea FA Cup | Michezo | DW | 07.01.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Leicester wabanduliwa, City wapepea FA Cup

Kulikua na matokeo ya kushangaza katika kipute cha FA Cup huko nchini England Jumapili kwani mabingwa wa zamani wa nchini humo Leicester City walibanduliwa na klabu inayoshiriki ligi ya daraja la nne Newport County.

Mechi hizo zilikuwa za raundi ya tatu ya kinyang'anyiro cha kombe la FA. Leicester walilazwa mabao mawili kwa moja. Rachid Ghezzal alifunga goli la kusawazisha katika dakika ya 82 baada ya Jamille Matt kuwatia Newport uongozini, lakini klabu hiyo ya daraja la nne ilikuwa na mawazo mengine kwa kuwa walipata mkwaju wa penalti huku zikiwa zimesalia dakika tano mechi kufikia mwisho na Padraig Amond akaupachika wavuni mkwaju huo.

Manchester City walikuwa wanachuana na klabu ya Rotherham ya ligi ya daraja la pili na kocha Pep Guardiola alifanya mabadiliko ya wachezaji wanane kutoka kwenye kile kikosi kilichowatandika Liverpool mabao mawili kwa moja katikati ya wiki. Lakini licha ya mabadiliko yote hayo kikosi hicho bado kilikuwa chenye nguvu zaidi dhidi ya wapinzani wao kwani mabingwa hao wa England walitoa ushindi mnono wa magoli saba bila huku Raheem Sterling, Riyadh Mahrez, Gabriel Jesus, Nicolas Otamendi na Leroy Sane wakiwa miongoni mwa walioandikisha majina yao katika daftari la wafungaji.

Jumamosi mabingwa watetezi wa taji hilo Chelsea walipata ushindi wa mbili bila walipopambana na Nottingham Forest katika mechi ambayo ilikuwa ndiyo ya mwisho kwa mchezaji wa kiungo cha kati Cesc fabregas ambaye anaihama klabu hiyo ya London magharibi. Kabla kutua huko Stamford Bridge fabregas alikuwa anasakata soka Barcelona Uhispania na kabla hapo aliichezea Arsenal ya huko London. kuna uvumi kwamba huenda akajiunga na Monaco huko Ufaransa iliyo chini ya ukufunzi wa Thierry Henry.

Ole Gunnar Solksjaer aliendeleza mwanzo wake mwema kama kocha wa muda wa Manchester United baada ya kushinda mechi yake ya tano mfululizo alipoizaba Reading mbili bila uwanjani Old Trafford. Arsenal ambao wameweka rekodi kwa kushinda taji la FA Cup mara nyingi zaidi kuliko timu yoyote ile, waliwalemea Blackpool kwa tatu bila.

Leo hii Jumatatu Liverpool ndio watakaokuwa wanaingia uwanjani kutafuta ushindi watakapocheza na Wolverhampton Wanderers.

Mwandishi: Jacob Safari/APE/AFPE/DPAE

Mhariri: Gakuba Daniel