1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lacroix amaliza ziara DRC, hali bado tete

3 Desemba 2019

Mjumbe wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anayesimamia operesheni za kulinda amani amekamilisha ziara yake ya siku tatu nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo huku hali ya kiusalama katika jimbo la Kivu ikiwa imezorota.

https://p.dw.com/p/3U8II
Jean-Pierre Lacroix, Blauhelme
Picha: picture-alliance/AP Photo/Al-Hadji Kudra Maliro

Baada ya kutembelea miji ya Beni na Goma huko Mashariki Jean-Pierre Lacroix amekutana mjini Kinshasa na maafisa wa serikali pamoja na wabunge wa Kivu ya kasakazini.

Ziara hiyo ya naibu katibu mkuu wa umoja wa mataifa imekuja siku kadhaa kabla ya baraza la usalama la Umoja huo kuongeza muhula wa kikosi cha Monusco nchini Kongo.

Jean-Pierre Lacroix hata hivyo hakukutana na rais Felix Tshisekedi kama ilivyopangwa. Umoja wa Mataifa haukuelezea sababu lakini ikulu ya rais imesema kwamba ajenda ya rais ilikuwa nzito. Hali hiyo inaashiria huenda kuna uhusiano mgumu ulioko hivi sasa baina ya serikali ya Kongo na Umoja wa Mataifa.

Naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa amekutana na waziri mkuu Sylvestre Ilunga pamoja na waziri wa ulinzi na wa mambo ya nje ambao walitathmini uhusiano baina ya kikosi cha kulinda amani cha MONUSCO na serikali ya Kongo.

Jean-Pierre Lacroix, Blauhelme
Mjumbe wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Jean-Pierre Lacroix alikuwa nchini Congo kwa ziara ya siku tatu.Picha: picture-alliance/AP/Keystone/M. Trezzini

Lacroix amesema kwamba umoja wa mataifa abado unategemea kuwepo ushirikiano wa karibu na serikali kwa ajili ya kumaliza tishio la kiusalama dhidi ya raia huko Beni "Hatuwezi kufichana ukweli, ni kwamba kunatatizo sugu la kiusalama huko Kivu lakini pia kuna tatizo pia linaloonekana kuwa ni uchumi wa vita ambao kuna watu wanaochochea machafuko hayo kwa faida zao binafsi.Tulizungumzia pia mandamano ya hivi karibuni ambayo yanaonyesha hasira za raia,lakini ni wazi kwa wote kwamba kushambulia watu wanaojihusisha na kupambana na ugonjwa wa Ebola ni kitendo cha kulaani kwa sababu kitaathiri vita dhidi ya Ebola." 

Msimamo huo wa Umoja wa Mataifa wa kuwanyooshea kidole watu wanaochochea machafuko huko Kivu ulizusha maoni mengi. Kwenye mitandao ya kijamii raia wengi wa Congo walielezea kwamba msimamo huo unaashiria jeshi hilo la MONUSCO kushindwa kuwajibika kikamilifu katika kuwalinda raia.

Mbali na viongozi wa serikali, Lacroix pia alikutana na wabunge wote wa jimbo la Kivu ya Kaskazini. Waliohudhuria kikao hicho wamesema kwamba ilikuwa ni kama mazungumzo ya viziwi wawili. Mbunge.

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linataraji kuongeza muda wa kikosi hicho cha MONUSCO ifikapo Disemba 31. Kikosi hicho kipo kwa zaidi ya miaka 20 nchini Congo na bajeti ya dola bilioni moja kila mwaka lakini kinalaumiwa kwa kutowajibika kuwalinda raia.