Kwaherini DW Kiswahili | Masuala ya Jamii | DW | 30.03.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Kwaherini DW Kiswahili

Hamad Omar Hamad, aliyekuwapo hapa Idhaa ya Kiswahili ya Deutsche Welle kwa mafunzo ya mwezi mmoja, leo (30.03.2012) amewaanga rasmi wenyeji wake, timu ya DW Kiswahili kwa ushairi.

Kwaheri ya Kuonana

Kwaheri ya Kuonana

Nataka niwashukuru, kwa zenu njema hisani
Kunipatia uhuru, kungia studioni
Nikaangaziwa nuru, ya kwenda mbele usoni
Kwa hilo nawashuku, Allah atakujazini

Shukran Andrea, hapa kunikaribisha
Ombi langu kupokea, la kuja kujifundisha
Mengi nimejionea, yaliyonifurahisha
Inshaallah 'tayatumia, kuwa dira ya maisha

Niseme ahsanteni, kwa timu yote pamoja
Edi Abdulrahmani, na Adeladus Makwega
Mohammed Dahmani, na Daniel Gakuba
Nyote nawashukuruni, kwa kunonesha umoja

Ahsante bi Samiya, Stumai na Mwasimba
Nina na Sheikh Mtullya, na Iddi bin Sessanga
Nyote 'menisaidia, kwenye fani kujijenga
Kwa Mungu nawaombea, muepushwe na majanga

Kwa Othman Miraji, salam muzipeleke
Na Amina Mjahidi, Josephat na Wibke
Nyote mulinifariji, nisijione mpweke
‘Kanipa nilohitaji, bila kuficha chochote

Khelef bin Ghassani, kake nisiye mwengine
Pendo, Eliza na Ummi, Wanjiru nao wengine
Bruce mwana Amani, na Kitojo Sekione
Kwa uwezo wa manani, kwengineko tukutane

Ni mengi nilojifunza, ndani ya mwezi mmoja
Ningependa ningeweza, kwongeza mwaka mmoja
Nikaweza yamaliza, yale yaliyonitoja
Ni mengi yahanikiza, hapatoshi kuyataja

Kutaka kwongezwa tena, ni kawaida ya mja
Si uroho ni uungwana, kuomba panapo haja
Twaanza pasiponona, kisha tukataka paja
Ada ya mja kunena, jaalae akangoja

Mwisho wa shairi hili, naomba isonge mbele
Idhaa ya Kiswahili, ya redio Deutsche Welle
Iwe idhaa ya kweli, ishinde zilo za kale
Izidi pasha habari, na Kiswahili ikyokole.

Hamad Hamad, 30 Machi 2012, Bonn

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com