1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muungano wa Al Sadr wanyakua ushindi Iraq

Saumu Mwasimba
12 Oktoba 2021

Uchaguzi wa bunge uliofanyika mapema nchini Iraq washuhudia idadi ndogo ya wapiga kura wakati umma wa Iraq ukionesha kupoteza matumaini ya kuwepo mageuzi katika mizani ya madaraka

https://p.dw.com/p/41Z9C
Irak | Unterstützer von al-Sadr feiern nach den Parlamentswahlen
Picha: Ayman Yaqoob/AA/picture alliance

Muungano wa vyama unaoongozwa na  kiongozi wa kidini wa madhehebu ya Shia nchini Iraq Moqtada al-Sadr umenyakua ushindi kwenye uchaguzi wa bunge uliofanyika Jumapili. Matokeo yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi yanaonesha kundi la muungano wa al Sadr limenyakua kiasi viti 60 vya bunge la Iraq.

Matokeo ya awali yaliyotangazwa jana Jumatatu yanaonesha kwamba muungano unaoongozwa na ulamaa wa kishia mwenye ushawishi mkubwa nchini Iraq Moqtada al Sadr umeendelea kushikilia nafasi yake kama kundi lenye nguvu kubwa bungeni likinyakua viti visivyopungua 60 kwenye bunge la viti 329. Shangwe za wafuasi wa muungano huo zilitawala kote Iraq hapo jana, baada ya matokeo hayo kutangazwa.

BdTD | Sadr-Anhänger feiern nach den Parlamentswahlen im Irak
Picha: Thaier Al-Sudani /REUTERS

"Leo tunawapongeza wananchi wa Iraq kwa ushindi katika mradi wa mageuzi unaoongozwa na Muqtada al Sadr. Leo tunahisi kwamba Iraq imepata ukombozi. Hisia hizi hatujawahi kuwa nazo tangu mwaka 2003. Leo hii kwahakika Iraq imekombolewa kutoka kwenye ufisadi''

Huyo ni Fadhil Al Taie, mfuasi wa muungano unaoongozwa na Al Sadr. Kiongozi huyo wa madhehebu ya Shia ambaye binafsi hakugombea kwenye uchaguzi huo wa bunge,alizungumza kupitia Televisheni baada ya matokeo kutangazwa na alisikika akiwatia shime wafuasi wake washerehekee ushindi walioupata.

Wagombea 3,249 ndiyo waliopambana kuwania kuchaguliwa kuingia bungeni katika uchaguzi wa Jumapili ambao kimsingi umefanyika mapema kabisa na sio kama ilivyokuwa imepangwa huko nyuma. Hatua hiyo imetokana na shinikizo kubwa lililotokana na miezi kadhaa ya maandamano ya umma wa Iraq uliokuwa ukidai mageuzi nchini humo. Bila shaka kuna walioshindwa vibaya katika uchaguzi huo na miongoni mwao ni kundi la Fatah ambalo ni mshirika wa karibu wa Iran.

Irak Wahlen Der irakische schiitische Geistliche Muqtada al-Sadr
Picha: Alaa Al-Marjani/REUTERS

Kundi hilo limepata pigo kubwa baada ya kunyakua viti 14 pekee ishara ya wazi inayoonesha kwamba muungano huo umeporomoka kutoka viti 47 ilivyokuwa ikishikilia kwenye bunge lililopita. Ni muhimu kuweka wazi kwamba uchaguzi huu wa bunge wa Iraq umeshuhudia idadi ndogo ya wapiga kura waliojitokeza kutokana na kuwepo hali ya wananchi kuchoshwa na makundi ya wachache ya wanasiasa.

Tume ya uchaguzi imesena  ni asilimia 41 pekee ya wapiga kura ndio waliojitokeza idadi ambayo inatajwa kuwa ndio ndogo zaidi kuwahi kushuhudiwa katika chaguzi zilizowahi kufanyika nchini humo tangu alipoangushwa madarakani Saddam Hussein mnamo mwaka 2003. Iraq nchi yenye utajiri mkubwa wa mafuta imekuwa kwenye matatizo makubwa ya migogoro ya kiuchumi na kisiasa kwa miaka kadhaa sasa. Wananchi wengi ya taifa hilo la Mashariki ya Kati hawana imani kubwa na siasa na hawatarajii kwamba uchaguzi huu utaleta mabadiliko yoyote katika mizani ya madaraka iliyopo sasa.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Iddi Ssessanga