1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kujiuzulu Oezil timu ya taifa kwazua zogo Ujerumani

Sekione Kitojo
23 Julai 2018

Hatimaye volcano yaripuka, baada ya Mesut Oezil kuamua  kujizulu kutoka  timu  ya  taifa  ya  Ujerumani, lawama  na  mashambulizi yazidi dhidi  yake, na mjadala mkali wazuka

https://p.dw.com/p/31xFU
Mesut Özil
Picha: picture-alliance/ULMER/M. Ulmer

Matokeo  yaliyotarajiwa  kuhusiana  na  suala  la  Mesut Oezil yamesababisha  majibu  ambayo  hayakutarajiwa. Hakuna  mtu katika  masimulizi  haya  ya  kusikitisha  amejitokeza  kuwa  mshindi katika sakata  hili.

Berlin Mesut Özil Kabine Merkel
Mesut Oezil akipongezwa na kansela Angela Merkel katika chumba cha kuvalia wachezaji baada ya ushindi wa Die MannschaftPicha: picture-alliance/dpa/Bundesregierung/G. Bergmann

Mesut  Oezil alijiuzulu  kutoka  katika  timu  ya  taifa  ya  Ujerumani Die Mannschaft  kwa  kuwashambulia  vikali , wafadhili, vyombo  vya habari, chama  cha  kandanda  nchini  Ujerumani  DFB na  hususan rais  wa shirikisho  hilo, lakini  ni  vigumu  kuona  kila  upande kuwa ni  kitu  kingine  mbali  na washindwa  katika  suala  hili  la kusikitisha.

Gazeti  la  Sueddeutsche Zeitung limeueleza  uamuzi  wa  mchezaji huyo  kuwa  ni " kipigo kamili cha majira ya  joto"  wakati  mtaalamu maarufu  wa  soka  la  Ujerumani  Raphael Honingstein aliandika katika  ESPN  kuhusiana  na  kujiuzulu  Oezil  kutoka  katika  timu  ya taifa  kuwa  " ni  hali  mbaya  kuliko  kushindwa  kokote  katika kombe  la  dunia."

Oezil, katika  kuvunja  ukimya wake  jana  Jumapili  kuhusiana  na picha  zenye  utata  zilizopigwa  akiwa  pamoja  na  rais  wa  Uturuki Recep Erdogan  kabla  ya  fainali  za  kombe  la  dunia  nchini  Urusi, hakuonesha kujutia kitendo  hicho na  ameonesha  kukasirishwa mno.

Bambi 2010 Mesut Özil
Mesut Oezil akipokea tuzo ya Bambi ambayo ni tuzo ya vyombo vya habari Picha: picture-alliance/dpa/B. Pedersen

Hali ya kisiasa

"Natambua  kwamba  picha  hizo zimesababisha maelezo  mengi katika  vyombo  vya  habari vya  Ujerumani, na  baadhi  ya  watu huenda  wakanishutumu  mimi  kwa  udanganyifu ama  kuwa muongo, picha  hizo  hazina  lengo  la  kisiasa,"  amesema  Oezil, mzaliwa  wa Gelsenkirchen  nchini  Ujerumani  akiwa  na  asili  ya  Uturuki.

Iwapo hilo  ni  kweli, inaonekana kwamba Oezil  hajitambui kwa kufikiri  kwamba  hakutakuwa  na uhusiano utakaohusishwa  na picha  hizo zilizopigwa  wiki  chache  kabla  ya  Erdogan  kuwania kuchaguliwa  tena, kutokana  na  hali  ya  kisiasa  ilivyo  nchini Uturuki.

Erdogan mit Özil (picture-alliance/dpa/Uncredited/Presdential Press Service)
Picha iliyozua gumzo dhidi ya Oezil , ni pale alipopiga picha hii akiwa na rais wa Uturuki Recep ErdoganPicha: picture-alliance/dpa/Presidential Press Service

Hata  hivyo  kansela  wa  Ujerumani Angela  Merkel  amemshukuru Mesut Oezil  kwa  mchango  wake  katika  timu  ya  taifa , Die Manschaft, amesema  msemaji  wa  serikali  ya  Ujerumani leo. "Kansela  anamthamini Mesut Oezil kwa  hali  ya  juu  kabisa. Mesut Oezil ni  mchezaji  kandanda  mzuri  sana  ambaye  ameifanyia mengi timu ya  taifa,"  msemaji  wa  kansela  amesema. 

"Mesut amefanya  sasa  uamuzi  wa  kujitoa  kutoka  timu  hiyo na  ni  lazima uamuzi  wake  uheshimiwe," alimaliza  msemaji  huyo  wa  kansela. Mesut Oezil  leo  ameweka  picha  yake  kwa  mara  ya  kwanza tangu  tafarani  hii  kuzuka  hapo  jana  akiwa  na   jezi  za  klabu yake  ya  Arsenal  ya  mjini  London, akionesha  furaha  kurejea  kwa amani  katika kusakata  kandanda  tena  bila  ya  kuwa  na  mzigo wa timu  ya  taifa  ya  Ujerumani.

Mesut Özil
Mesut Oezil kabla ya mchezo akiwa katika sare za Die MannschaftPicha: picture-alliance/Photoshot

Wakati  huo huo  kamati  ya utendaji  ya shirikisho  la  kandanda nchini  Ujerumani DFB  iliyoketi  leo  na  kujadili  suala  hilo imetupilia mbali madai ya ubaguzi yaliyotolewa  na  Mesut Oezil dhidi  ya  rais wa  shirikisho la DFB  Reinhard Grindel  katika  barua yenye hasira ya kujiuzulu. "Tunapuuzia dhana kwamba  DFB inahusika  na ubaguzi," imeeleza  taarifa.

Sekione  Kitojo, hadi  mara  nyingine kwaherini.

Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / rtre / afpe

Mhariri: Idd Ssessanga