Kongole Deutsche Welle
23 Januari 2013
Myaka hamsini tamima, mnatujuza habari
Kitendeti kuyasema, yalofichwa sirisiri
Mumevuka milima, nyanda pia na bahari
Ulaya na Afrika, mashabiki tumbi zima
Asia pia wafika, sifa zako zinavuma
Lau watilia shaka, nenda ukazuru Barma
Korija nakuvulia, wewe usiye mfano
Na koja nakuvishia, kwa ishara ya maneno
Na tungo nakutungia, kishairi pamwe ngano
Langu ombi wahariri, mdumishe kazi njema
Waandishi mashuhuri, msilale ni mapema
Fichueni hizo siri, mtupashe himahima
Wasalaam mashabiki, inshallah tutaonana
Qahari awabariki, kwa marefu na mapana
Idhaa yetu na ibaki, nyota yake ikifana
Kongole kwa Deutsche Welle, hamsini kutimia
Tanbihi: Shairi la Wasuwa Maxwell (Malenga Chipukizi Mtanashati) wa Nairobi, Kenya kwa ajili ya Maadhimisho ya Miaka 50 ya Idhaa ya Kiswahili ya DW.
Mhariri: Mohammed Khelef