Kobler: Hatuwezi kuwa kwenye kila kijiji | Matukio ya Afrika | DW | 06.11.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Kobler: Hatuwezi kuwa kwenye kila kijiji

Umoja wa Mataifa unasema serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imewakamata washukiwa 200 wa mauaji ya maangamizi ya Beni kufuatia operesheni ya pamoja kati ya kikosi chake na jeshi.

Martin Kobler

Mkuu wa MONUSCO, Martin Kobler.

Wakati Kikosi chake cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Kongo (MONUSCO) kiliposhirikiana bega kwa bega na jeshi la serikali ya Rais Joseph Kabila kuliangamiza kundi lililokuwa linakuja juu kwa kasi, Vuguvugu la Machi 23 au M23 kwa kifupi, takribani Wakongo wote walielekea kubadilisha mawazo yao kuhusu dhima ya kikosi hicho cha Umoja wa Mataifa, ambacho kimekuwa huko mwaka wa 15 sasa.

Kutoka jeshi lenye sare za Umoja wa Mataifa linalosimama tu wakati waasi wakisonga mbele kutwaa maeneo kwa maeneo mikononi mwa serikali, hadi jeshi linalotumia vifaa na rasilimali zake kuwazuia waasi hao, Wakongo walianza kuamini kuwa MONUSCO ni kikosi kilichotumwa kuwalinda na sio kushuhudia tu wakati wakikabiliwa na maafa.

Lakini mtazamo huu kwa mara nyengine uliingia majaribuni wiki chache zilizopita, pale waasi wa ADF-Nalu, kundi linaloipinga serikali ya Yoweri Museveni ya Uganda, walipovishambulia vijiji kadhaa mashariki mwa Kongo, na zaidi ya watu 120 wakapoteza maisha yao.

Maandamano ya raia Beni

Mkuu wa MONUSCO, Martin Kobler (kushoto) akikitembelea kikosi hicho mjini Goma.

Mkuu wa MONUSCO, Martin Kobler (kushoto) akikitembelea kikosi hicho mjini Goma.

Tangu hapo kumekuwa na maandamano ya mara kwa mara dhidi ya MONUSCO na wakati mwengine hata mashambulizi. Hata hivyo, mkuu wa MONUSCO, Martin Kobler, hatishwi na maandamano ya raia dhidi ya kikosi chake na anajaribu kuyaelewa.

"Wakati nilipokuwa Goma mwezi Agosti mwaka 2013, siku hizo kadhia ya M23 ikiwa ya hali ya juu, nilishuhudia pia maandamano. Gari yangu ilipigwa mawe, kwa sababu muonekano wa MONUSCO haukuwa mzuri kwa raia. Ninaweza kuzielewa hasira zao, kwamba inakuwaje pawe na kikosi cha Umoja wa Mataifa kwenye ardhi yao lakini kisipambane kwa ajili yao," alisema mwanadiplomasia huyo ya Kijerumani kwenye mahojiano yake na Deutsche Welle.

Hasira za watu wa Goma zilishuka baada ya uingiliaji kati wa Umoja wa Mataifa na vikosi vya nchi washirika vilivyotumwa huko kukabiliana na M23. Matokeo yake, Novemba mwaka jana, kundi la M23 likajikuta likilazimika kuweka silaha chini na kugeukia mchakato wa kisiasa.

Haja ya suluhisho la kisiasa

Suluhisho la kijeshi likawa limepatikana dhidi ya kundi hilo, lakini kama anavyosema Kobler, suluhisho la kweli kabisa ni la kisiasa, ambalo sio tu kwa Goma, bali kwa eneo zima la mashariki mwa Kongo halijapatikana hadi leo. Na hicho ndicho kinachoikumba Beni hivi leo.

Mkuu wa MONUSCO, Martin Kobler (wa pili kulia) akikitembelea kikosi hicho mjini Goma.

Mkuu wa MONUSCO, Martin Kobler (wa pili kulia) akikitembelea kikosi hicho mjini Goma.

"Bado kuna makundi mbalimbali ya Mai-Mai na sasa waasi wa ADF Nalu wa Uganda ambao wana mafungamano na siasa kali za kidini. Nilikuwa huko wiki mbili zilizopita na nitarejea tena. Makamanda wetu wako huo pia na maafisa wa ngazi za juu wa MONUSCO, lakini ni muhimu sana kuwaeleza watu kile tunachoweza kukifanya na kile tusichoweza kukifanya. Hatuwezi kuwa kwenye kila kijiji, maana Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni nchi kubwa yenye misitu na mapori," alisema Kobler.

Kongo nchi iliyo mashariki ya kati ya Afrika ni taifa la pili kwa ukubwa wa kieneo barani Afrika ikitanguliwa na Nigeria, na ya 11 kwa idadi ya watu wengi duniani, ikiwa na wakaazi milioni 75. Ukubwa wake ni sawa na Ulaya ya Magharibi nzima.

Ndio maana, anavyoamini Kobler, hakuna suluhisho pekee la kijeshi linaloweza kuyamaliza matatizo ya taifa hilo, bila ya kuwa na dhamira ya kweli ya kisiasa.

Mwandishi: Dirke Kopp
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Saumu Yussuf