Klopp ndiye meneja mpya wa Liverpool | Michezo | DW | 09.10.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Klopp ndiye meneja mpya wa Liverpool

Aliipatia mafanikio makubwa Borussia Dortmund, jee atayaendeleza akiwa na Liverpool?m Hayo ndio maswali yanayoulizwa na Kila mtu baada ya Mjerumani huyo kuchukua usukani Anfield

Klopp alipotua Liverpool

Klopp alipotua Liverpool

Juergen Klopp amesaini mkataba wa miaka mitatu kuinoa timu hiyo ya Liverpool (Bwawa la maini) ilioko katika ligi kuu ya England –Premier League, baada ya Brendan Rodgers kuachishwa kazi kutokana na kuzorota kwa timu akiiacha nafasi ya 10 katika msimamo jumla wa ligi .

Klopp alianza kazi ya Ukocha katika kilabu ya Mainz 2001 , baada ya hapo kabla kuwemo kama mchezaji wakati ilipokuwa daraja la pili. Mwaka 2004 akafanikiwa kuipanidisha daraja na kuingia ligi kuu.. Katika kilabu ya Liverpool Klopp anajikuta katika hali sawa na ile wakati alipochukuwa uongozi wa Dortmund mwaka 2008, kuzorota katika ligi kuu .

Kwa hakika timu zote mbili zilishinda vikombe mbali mbali misimu iliopita hapo kabla na Klopp alipochukua mamlaka ya kuwa mkufunzi katika Dortmund, kilabu hiyo ilikuwa pia ikikumbwa na hatari ya kufilisika kukiachilia mbali kuwa na ndoto kubwa.Hivi sasa akiwa meneja wa Liverpool atategemewa kuiletea ushindi na hasa ikikumbukwa mabingwa hao wa zamani wa Ulaya hawajafanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya England –Premier League kwa mwaka wa 25 sasa. Akizungumza na vyombo vya habari mjini Liverpool Klopp alisema ,"Kuwa hapa ni heshima kubwa ninayoweza kuifikiria, kuwa katika kilabu moja wapo kubwa duniani- jinsi watu wanavyoishi na kandanda hapa Liverpool na mashabiki wake duniani kote. Hii si kilabu ya kawaida ni kilabu mahsusi. Ninafuraha kuwa hapa na kusaidia. Si muhimu vipi watu wanakuangalia ila ni muhimu wanakuangalia vipi pale utakapoondoka."

FC Liverpool beim Finale in Istanbul

Bwawa la maini enzi za mafanikio

Klopp mwenye umri wa miaka 48 aliyefanikiwa kuinusuru Dortmund mabingwa wa Ulaya 1997, wasiteremke daraja la pili chini ya mtangulizi wake Thomas Doll, anakabiliwa na kibarua kizito na Liverpool . Lakini wachambuzi wanasema pamoja na hayo Klopp ni mtu mwenye kutoa motisha kuanzia kwa wachezaji, mashabiki hadi bodi ya wakurugenzi wa kilabu na hilo litamsaidia sana kuweza kufanikiwa . Klopp au Kloppo kama anavyouitwa na mashabiki , ni kocha anayependelea mpira wa kasi.

Mwaka 2010 alimpandisha Mario Goetze katika kikosi cha kwanza , akamsajili Mjapani Shinji Kagawa kwa euro laki tatu kutoka ligi ya daraja la pili ya Japan na kuwageuza wachezaji kadhaa kuwa nyota katika timu ya taifa ya ushindi ya Ujerumani katika kombe la dunia wakiwemo Mats Hummels, Erik Durm, Kevin Grisskreuz na Roman Weidenfeller.

Kwa mtindo wake wa kushambulia haraka na hadi kipenga cha mwisho, Dortmund iliweza kuleta mshtuko na msisimko katika Bundesliga na ulaya kwa jumla na hata kuwakata ngebe Bayern Munich pamoja na kuvutia mamilioni ya mashabiki wa soka sehemu mbali mbali za dunia, huku ikisambaza pia shughuli zake za kibiashara nje ya bara la Ulaya.

Katika hatua hiyo, Dortmund chini ya uongozi wa Klopp , ilishinda ubingwa wa ligi ya Ujerumani 2011 na mwaka uliofuata ambapo pia ilinyakua kombe la Ujerumani na lile la Super pamoja na kufika fainali za ubingwa wa Ulaya 2013, iliposhindwa na Bayern Munich katika fainali ya kwanza ya mashindano hayo iliozikutanisha timu mbili za Ujerumani.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, afp,dpa

Mhariri:Yusuf Saumu