1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Klopp na Pep ndio makocha bora wa mwaka England

25 Novemba 2019

Kocha wa Liverpool Jurgen Klopp na mwenzake wa Manchester City Pep Guardiola wamepewa tuzo ya Chama cha Waandishi wa Kandanda ya kocha bora wa mwaka kwenye hafla iliyoandaliwa jana usiku mjini Manchester.

https://p.dw.com/p/3TgV0
Fußball Premier League Jürgen Klopp und Pep Guardiola
Picha: picture-alliance/dpa/AP Photo/R. Vieira

Klopp alifaulu kuipa Liverpool Kombe la Ulaya – UEFA Champions League na kuisaidia kumaliza msimu wa ligi na pointi 97, pointi moja tu nyuma ya Guardiola na mabingwa Manchester City.

Mhispania Guardiola aliiongoza Man City kuweka historia ya kunyakua mataji matatu ya nyumbani kwa kushinda Premier League, Kombe la FA, na Kombe la Carabao katika msimu wa 2018-19.

Mshindi wa tuzo ya kifahari ya Ballon d'Or 2019 atajulikana Desemba 2 mjini Paris, huku Lionel Messi, Virgil van Dijk, na Christiano Ronaldo wakizingatiwa kuwa wawaniaji wakuu kutoka kundi la wachezaji 30 waliotangazwa Oktoba.

Na tukizingumzia ligi ya Premier ya England, kinyang'anyiro kinaendelea kupamba moto, huku Klopp na vijana wake wa Liverpool wakijiimarisha kileleni na pengo la pointi 8 dhidi ya nambari mbili Leicester City. Liverpool walipata uishindi wa 2 – 1 dhidi ya Crystal Palace huku Leicester wakiwafunga Brighton 2 – 0. Na je, Klopp ana wasiwasi kuhusu kuwa na pengo kubwa kileleni mwa ligi na kisha kuliona likipungua? Siwazi kuhusu hilo. ni pointi nane pekee dhidi ya Leicester kwa hiyo hatupaswi kuwasahau. walikuwa mabingwa miaka mitatu iliyopita. Chelsea inacheza vizuri sana msimu huu. kama tungepoteza wiki iliyopita dhidi ya Crystal Palace basi pengo lingepungua hadi pointi tano pekee na watu wangeanza kuzungumza kitu tofauti kabisa kwa hiyo tumetulia tu sisi kuhusu hilo, hatutaki kuwaza kuhusu pengo, hatuwazi kuhusu pointi, tunawaza tu kuhusu mechi inayofuata, hilo limetusaidia sana mpaka sasa na nadhani tuendelee hivyo

Manchester City wanashikilia nafasi ya tatu baada ya kuwafunga Chelsea 2 – 1, na alipoulizwa kuhusu msimu huu unavyoenda kwa vijana wake, kocha Pep. Alisema "bahati mbaya tulikuwa na majeruhi kikosini kwa muda mrefu, na tuna wapinzani bora zaidi, hasa katika Premier League, ambao wanapata ushindi kila wiki, lakini bado ni Novemba kwa hiyo tutaendelea kupambana na kuona itakuwaje mwishowe.

Na baada ya Mauricio Pochettino kutimuliwa wiki iliyopita, kuna makocha kadhaa ambao kwa sasa bila shaka wanapata usingingizi wa mang'amung'amu. Miongoni mwao ni Unai Emery ambaye timu yake ya Arsenal ilitoka sare ya 2 – 2 na Southampton. Mwingine ni kocha wa Manchester United Ole Gunnar Solskjaer ambaye timu yake ilitoka sare ya  3 – 3 na Shefield United. Jose Mourinho alikuwa na mwanzo mzuri katika maskani yake mapya ya Tottenham baada ya ushindi wa 3 – 2 dhidi ya West Ham.