1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kizaazaa siku ya mwisho ya Ligi ya Premier

27 Julai 2020

Licha ya kuvurugwa na janga la corona ambalo liliilazimu Ligi ya Premier kusitishwa kwa siku 100 kuanzia Machi, Liverpool walikamilisha kampeni yao iliyovunja rekodi kwa kushinda kombe la kwanza la ligi baada ya miaka 30

https://p.dw.com/p/3fz0W
BG Kurioses Weltweit | UK Fans bei der Wiederaufnahme der Premier League - Everton v Liverpool
Picha: Reuters/M. Childs

Msimu huu pia ulishuhudia kuanzishwa kwa matumizi ya mfumo wa video katika kusaidia maamuzi ya refarii – VAR, ambapo mabao mengi na maamuzi ya penalty yalizusha ubishi. Vilabu vitano viliwabadilisha makocha huku Watford, ambao walishushwa ngazi katika siku ya mwisho wakiwafuta makocha mara tatu kwenye msimu mmoja.

Vijana wa Jurgen Klopp walijikusanyia pointi 79 katika mechi 27, kabla ya kumaliza msimu na rekodi ya ushindi wa mechi 32 na pointi 99.

Wakati huo huo, Manchester United walifanikiwa kuziba pengo la point inane na kumaliza katika nafasi ya tatu na hivyo kufuzu katika Champions League. Kocha Ole Gunnar Solskjaer anasema kazi bado ipo kwa sababu sasa wanaelekeza macho yao katika Europa League "Msimu ujao, tutakapocheza Ligi ya Mabingwa badala ya Ligi ya Europa utakuwa tofauti kwa sababu tunataka kusonga juu kwenye msimamo wa ligi. Kwa hiyo hatutoondoa macho yetu kwenye ligi na kuwapumzisha wachezaji katika Ligi ya Europa. Bila shaka tuna kandanda la Ulaya, huo utakuwa msingi wetu. Msimu ujao utakuwa mgumu hata Zaidi katika kushindania mataji hayo."

England | Jürgen Klopps Manager von Liverpool feiert mit Virgil van Dijk
​​​​​​Klopp aliwapa Liverpool taji la kwanza la PL katika miaka 30Picha: picture-alliance/SOLO Syndication/Daily Mail/K. Quigley

United waliizima ndoto ya Leicester City ambao sasa watalazimika kucheza Europa League baada ya kumaliza katika nafasi ya tano. Jamie Vardy alipata tuzo ya mfungaji bora kwa kutia nyavuni mabao 23. Kocha Brendan Rodgers amewapongeza vijana wake kwa kuwa na msimu mzuri. "Ubora wa timu za upande wa juu wa ligi hii ni wa kiwango cha juu kabisa. Na tumeshindana na hilo hata ingawa hatujafanikiwa katika kumaliza kwenye nne bora. Kwa hiyo, huo ni ujumbe mkubwa kutoka kwa wachezaji na jinsi walivyofanya vizuri katika kipindi kizima cha msimu huu."

Frank Lampard na vijana wake wa Chelsea walijikatia tiketi ya Champions League kwa kumaliza wan ne na wana fursa ya kubeba kombe la FA katika fainali ya Agosti Mosi dhidi ya Arsenal. Lampard amesema kishinda tiketi ya Ulaya kutarahisisha biashara ya usajili katika klabu hiyo ambayo tayari imewaleta winga Hakim Ziyech na mshambuliaji Timo Werner na wanaripotiwa kumuiwa kiungo wa Ujerumani Kai Havertz "Tunafahamu na nimeshajibu maswali kuhusu hilo kabla ya mchezo kuwa masuala ya kifedha ya Ligi ya Mabingwa ni makubwa. Tunajua hilo. Tunafahamu fahari ambayo wachezaji nyota hutaka kucheza katika Ligi ya Mabingwa. Wachezaji wakubwa ambao wako hapa tayari na wachezaji chipukizi wanataka kucheza katika Ligi ya MABINGWA.

Jose Mourinho alikuwa mmoja wa mabadiliko saba ya makocha yaliyofanywa wakati alipochukua nafasi ya Mauricio Pochettino na kuisaidia Tottenham Hotspurs kupanda kutoka nafasi ya 14 hadi ya sita na kujikatia tiketi ya Europa League.

Mikel Arteta alichukua mikoba ya Unai Emery katika klabu ya Arsenal na licha ya kuwa na msimu mbaya kabisa katika historia yao kwenye ligi kwa miaka 25, huenda bado akashinda taji lake la kwanza kama kocha watakapocheza dhidi ya Chelsea katika fainali ya FA.

Katika upande wa mkia wa ligi, Ilikuwa kilio kwa Bournemouth baada ya kipindi chao cha miaka mitano kwenye Premier League kufikia kikomo. Walishuka pamoja na Norwich na Watford.

Lakini ilikuwa ni machozi ya furaha kwa mshambuliaji wa Kitanzania Mbwana Samatta na wenzake wa Aston Villa baada ya kuponea chupuchupu shoka la kuiaga ligi.

afp/ap/dpa/reuters