1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiUswisi

UN: Kiwango cha joto duniani kuongezeka kwa nyuzi 1.5

17 Mei 2023

Shirika la Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani limesema kwa mara ya kwanza huenda wastani wa joto duniani kwa mwaka ukaongezeka zaidi ya nyuzi 1.5 katika kipimo cha Celsius juu ya viwango vya kabla ya mapinduzi ya viwanda.

https://p.dw.com/p/4RVtx
Australien | Trockenheit in Menindee
Picha: Dean Lewins/AAP/dpa/picture alliance

Shirika hilo la WMO limesema Jumatano kuwa hali ya joto duniani hivi karibuni inatazamiwa kuvuka lengo kubwa zaidi lililowekwa katika makubaliano ya hali ya hewa ya Paris na uwezekano wa theluthi mbili kwamba moja ya miaka mitano ijayo itafanya hivyo.

Katibu Mkuu wa WMO, Petteri Taalas amesema mwaka uliopita, WMO iliweka uwezekano wa utabiri huu kutokea chini ya asilimia 50, lakini sasa inatabiri uwezekano wa asilimia 66 kwamba tutazidi nyuzijoto 1.5 katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Ongezeko la joto halijapunguzwa

''Ni hakika kwamba tutaona mwaka wenye joto zaidi katika rekodi kwenye miaka mitano ijayo mara tu awamu hii ya hali ya hewa ya La Nina itakapomalizika,'' alifafanua Taalas.

Taalas amesema wanahitimisha kwamba hawajaweza kupunguza ongezeko la joto hadi sasa, na bado wanaenda katika mwelekeo mbaya.

Petteri Taalas, Generalsekretär der Weltorganisation für Meteorologie (WMO)
Katibu Mkuu wa WMO, Petteri TaalasPicha: Salvatore Di Nolfi/KEYSTONE/picture alliance

Lengo la kudhibiti ongezeko la joto duniani kwenye nyuzi 1.5 liliwekwa katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi uliofanyika mjini Paris, Ufaransa, mwaka 2015.

Shirika la WMO lenye makaazi yake mjini Geneva, Uswisi halifikirii kwamba ongezeko la joto duniani litaweza kupanda kabisa juu ya alama hiyo katika miaka michache ijayo.

2022 ulikuwa na nyuzijoto 1.15

Hata hivyo, Taalas amesema shirika lake linatoa tahadhari kwamba watakiuka kiwango cha nyuzijoto 1.5 kwa muda mfupi na kuongezeka kwa masafa. Wastani wa hali ya joto duniani kwa mwaka 2022 ulikuwa kama nyuzi 1.15 juu ya wastani wa kati ya mwaka 1850 hadi 1900.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa pia linatarajia kuwa mwaka mmoja kati ya miaka hiyo mitano, itaushinda mwaka 2016, kama mwaka wenye joto zaidi katika rekodi, kwa sababu ya mabadiliko ya hali ya hewa yanayosababishwa na binadamu na hali ya hewa ya asili ya El Nino.

Talaas ameonya kuwa wanahitaji kujiandaa, kwani hali hiyo itakuwa na athari kubwa kwa afya, usalama wa chakula, usimamizi wa maji na mazingira.

(DPA, AFP)