Kivu Kaskazini: Mkoa unaodhibitiwa na wapiganaji
Karibu makundi 40 ya wapiganaji yako katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Kusini. Watu wapatao milioni 2 wamekuwa wakimbizi na vijiji vimeharibiwa. Mradi wa Mtandaoni wa "Local Voices" unawapa sauti waathirika.
Sauti za wenyeji
Karibu makundi 40 ya wapiganaji yako katika mikoa ya mashariki mwa Kongo ya Kivu Kaskazini na Kusini. Watu wapatao milioni mbili wameyakimbia makaazi yao na vijiji vingi vimeharibiwa. Mradi wa mtandaoni wa "Local Voices unawapatia sauti waathirika. Mradi huu wote unapatikana kwenye tovuti ya www.localvoicesproject.com.
Katika jina la Mungu
Jenerali aliejipachika cheo mwenyewe, Janvier ana historia ndefu ya ghasia na mauaji. "Ni mapenzi ya Mungu," Janvier ambaye ameshikilia Biblia mkononi alisema. Anaongoza kundi la wapiganaji maarufu kama Muungano wa Wazalendo kwa ajili ya Kongo huru (APCLS). Miaka 8 nyuma, alijenga makao yake katika kilima kilicho karibu na kijiji cha Lukweti, ambacho tangu wakati huo kinajulikana kama Mlima Sinai
Kutafuta sababu katika maisha
Jenerali huyo ameamrisha mashambulizi, na "Fidel Castro," kama anavyojiita mwenyewe, anapanga kupigana na kundi lingine adui lililo chini ya uongozi wa Ntabu Cheka. Kwake hii ni kazi tu. Vinginyevyo kuna umasikini tu kijijini Lukweti. Vijana wengi zaidi hawajasoma. Baadhi wanasema, "upiganaji umeleta maana katika maisha yangu."
Ni kuuwa tu
Baada ya kuvuka daraja la kijiji, wapiganaji wanasonga mbele kuelekea Pinga. Huko watawauwa -wapiganaji wa Ntabu Cheka na labda raia pia. Hawataki kuzungumzia mambo hayo. Mji wa Pinga umekuwa uwanja wa vita baina ya makundi hasimu ya wanamgambo kwa miaka kadhaa. Watu wengi wameuawa na maelfu wamekimbia.
Urafiki na wapiganaji
Awe raia au mpiganaji, wote wanapenda soka. Licha ya pengo kubwa kati yao - mmoja anabeba silaha, mwingine hana kitu - urafiki unajengeka baina ya wakaazi wa Lukweti na waasi wa APCLS. Hata baadhi wanatoka familia moja.
Mshikamano au uyakinifu?
Baraza la kijiji maarufu kama "Barza" linafanya maamuzi yote muhimu kijijini Lukweti. Akizungumzia namna wanavyoishi wanakijiji na waasi wa APCLS, Mzee Massomo anamwaga tu sifa. "Wanatulinda dhidi ya wanamgambo wengine ambao wangetunyanyasa," anasema "Tunawapa chakula." APCLS, anasema ina nidhamu kuliko jeshi la serikali.
Kuwa mwanamke katika kundi la wapiganaji
Kahindo, mwenye umri wa miaka 22, amepumzika katika kibanda karibu na machine ya kusaga mhogo. Kazi yake, kama ilivyo kwa wanawake wengi ndani ya APCLS, ni kutafuta chakula. Anachukuwa sehemu ya chakula kinachovunwa na wakulima, ambao tayari ni masikini.
Wanawake mashakani
"Sitaki kuolewa na mpiganaji," anasema Neema Riziki mwenye umri wa miaka 16 kutoka Lukweti. "Wanawake wengi wangependelea kuolewa na wapiganaji, kwa sababu eti wanawatunza vizuri wake zao. Lakini baadhi ya marafiki zangu wamegeuka wajane mara tu baada ya kuolewa. Na ili kuendelea kuishi, baadhi yao wanalaazimika kuuza miili yao."
Mihadarati kwa ajili ya wapiganaji
Mama Soleil (katikati) analima bangi mbele ya gofu la kiwanda cha toka enzi za ukoloni katika mji jirani wa Nyabiondo. Ni mwanamke maarufu. Wateja wake ni wapiganaji na wanajeshi. Ukivuka ukuta huo, walinda amani wa Umoja wa Mataifa wameweka kambi yao.
Hakuna maendeleo bila barabara
Mkulima huyo amehangaika kwa zaidi ya masaa manne kutoka Lukweti kwenda mji jirani wa Nyabiondo, ambako anataka kuuza sokoni pombe aina ya mbege aliyoitengeneza kutokana na ndizi. Watu wengi kijijini Lukweti wanategemea zao la ndizi.
Ushirikiano kati ya polisi na wapiganaji
Ndani ya kibanda, mwanamme kutoka uongozi wa wapiganaji anakutana na mkuu wa polisi wa mji wa Nyabiondo. Kwa mtu wa nje inaweza kuwa vigumu kutofautisha kati ya wapiganaji na maafisa wa polisi.
Kwa msaada wa Mungu
Mchungaji wa Kiprotestanti wa Lukweti anaomba kwa hisia katika misa ya ibada ya Jumapili. Wakati wakikabaliwa na hali isiyoisha ya ukosefu wa usalama na hofu, wanakijiji wanajiliwaza na kupata matumaini katika imani zao.
Matumaini ya amani
Vijana wacheza ngoma kutoka Muungano wa Amani wanaimba "komesha vurugu!" Hili ni jambo la kishujaa kulifanya, kwa sababu wapiganaji wanachochea chuki za kikabila, na mara nyingi vijana wadogo hupambanishwa wao kwa wao. Vijana hao waimbaji kutoka makabila mbalimbali ni ushahidi kwamba inawezekana kwa makabila tofauti kuishi pamoja mashariki mwa Kongo.