Kishindo cha Ceta chaukaba Umoja wa Ulaya | Magazetini | DW | 25.10.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Kishindo cha Ceta chaukaba Umoja wa Ulaya

Kushindwa mazungumzo ya biashara huru kati ya Umoja wa ulaya na Canada-Ceta,na kuhamishwa wahamiaji wa msitu wa Calais ndizo mada zilizohanikiza magazetini

 

Tunaanzia lakini mjini Brussels nchini Ubeligiji,yanakokutikana makao makuu ya Umoja wa Ulaya ambako jimbo dogo la Wallonie limezusha wasi wasi uwezo wa Umoja wa ulaya kufikia makubaliano na mataifa mengine. Gazeti la "Hannoversche Allgemeine" linaandika:"Umoja wa Ulaya umebakiwa na jukumu la aina gani sasa ? Hilo ndilo suala linalogubika mvutano kuhusu makubaliano ya biashara huru pamoja na Canada-Ceta. Hii ni dalili moja tu ya mizozo mikubwa iliyoko. Kutoka kila pembe inatoweka imani kuelekea demokrasia wakilishi. Ingawa demokrasia hiyo haiko mbali na wananchi kama wengi wanavyodai. Hata katika daraja ya Ulaya hali si tofauti. Bunge la Ulaya ni taasisi iliyochaguliwa na wananchi na ina jukumu la kupitisha maamuzi kuhusu makubaliano mfano wa haya ya Ceta. Lakini katika uchaguzi wa bunge la Ulaya mwaka 2014 chini ya nusu ya wananchi wa umoja wa ulaya walitoa sauti zao. Kwa hivyo kasoro za demokrasi upande wa wapiga kura,zinabidi pia kujadiliwa."

Nini kitafuata baada ya mzozo wa Ceta?

Gazeti la "Allgemeine Zeitung" la mjini Mainz lina maaoni sawa na hayo na kuandika:"Kwa vyovyote vile kasheshe ya Ceta itakavyomalizika,kiini cha mzozo kinastahiki sifa; lakini utaratibu wa kuushughulikia mzozo huo  ni wa mashaka na unadhihirisha kwa mara nyengine tena hali ngumu iliyoko katika Umoja wa Ulaya. Pindi Umoja wa Ulaya ukiingia ufa katika nchi mojawapo mwanzilishi wake,baasi hilo litakuwa pigo kubwa na pengine mwisho wa Umoja wa Ulaya katika mfumo wake wa sasa.Brexit tayari ni pigo kubwa. Lakini bila ya shaka sio la mwisho. Kwa hivyo hatima bado haijulikani.

Kambi ya Msituni ya Calais yakongolewa

Kambi za msituni katika mji wa kaskazini wa Ufaransa Calais zimeanza kukongolewa baada ya wahamiaji waliokuwa wakiishi katika hali duni kabisa katika kambi hizo kuanza kuhamishiwa katika vituo vya mapokezi tangu jana. Wahariri wengi wa magazeti ya Ujerumani wanasifu uamuzi wa serikali ya Ufaransa wa kuifunga kambi hiyo ya msituni kama inavyoitwa. Hata hivyo kuna wanaoelezea wasi wasi wao,mfano wa mhariri wa gazeti la "Neue Osnabrücker" anaeandika:" Ni vizuri kwamba kambi mwitu za wakimbizi huko Calais hatimae zinazokongolewa. Maelfu ya watu,wakiwemo miongoni mwao watoto wadogo,wanaondoshwa katika eneo hilo la matope,uchafu na baridi kali. Lakini tatizo hasa halijapatiwa ufumbuzi. Wengi wa wakimbizi hao wanaoingia ndani ya mabasi,watarejea huku huku. Kwao wao Uingereza ndio lengo,ndio ndoto yao na hasa kwasababu jamaa zao wako huko na huko wanahisi wana nafasi nzuri ya kupata kazi. Wafaransa sio peke yao wanaobidi kuwajibika. Calais ni aibu kwa Ulaya nzima. Kwasababu huko ndiko inakobainika wapi inaelekea sera ya pamoja ya wakimbizi barani ulaya.

 

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Khelef