1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kipchoge anawinda medali ya tatu ya Olimpiki katika marathon

11 Aprili 2024

Mkenya Eliud Kipchoge anatarajia kuweka historia kwa kushinda medali yake ya tatu mfululizo ya Olimpiki ya mbio za marathon katika Michezo ya mwaka huu mjini Paris.

https://p.dw.com/p/4efXr
Eliud Kipchoge
Bingwa mara mbili wa Olimpiki wa Kenya Eliud KipchogePicha: Gao Jing/Xinhua/picture alliance

Muethopia Abebe Bikila, Waldemar Cierpinski kutoka iliyokuwa Ujerumani Mashariki na Kipchoge ndio wanariadha pekee walioshinda medali mbili za dhahabu za Olimpiki katika marathon wakati walipoyatetea mataji yao.

Kipchoge, ambaye atatimiza umri wa miaka 40 Novemba mwaka huu ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa matarajio yake ni kushinda medali ya tatu ya Olimpiki.

Wakati kukiwa na maswali kuhusu kama Kipchoge anapanga kustaafu hivi karibuni, amesisitiza dhamira yake ya kujaribu kuwapa motisha watu wa viwango vyote kuendelea kupambana.