Kiongozi wa upinzani adai kuibiwa ushindi Gabon | Matukio ya Afrika | DW | 03.09.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Kiongozi wa upinzani adai kuibiwa ushindi Gabon

Wakati kiongozi wa upinzani nchini Gabon Jean Ping anadai kuwa amedhulumiwa ushindi wanachama kadhaa wa upinzani wameachiwa baada ya kuzuiwa na polisi.

Bwana Jean Ping amesema yeye ndiye alieshinda uchaguzi wa rais siku mbili baada ya matokeo ya uchaguzi huo kutangazwa rasmi na tume ya uchaguzi. Bwana Jean Ping amemlaumu Rais aliyemo madarakani Ali Bongo Ondimba kwa kufanya hila ili kushinda uchaguzi.

Kiongozi huyo wa upinzani hapo jana alitaka matokeo ya uchaguzi ya kila kituo yatolewe hadharani na amesisitiza kwamba suluhisho litapatikana iwapo tu ukweli juu ya matokeo ya uchaguzi utaheshimiwa.

Aliwaambia waandishi habari "mimi ndiye Rais" baada ya kuachiwa kutoka kwenye makao yake makuu yaliyozingirwa na maafisa wa usalama hapo awali. Ping alisema dunia yote inajua nani ni Rais wa Jamhuri ya Gabon

.Ametahadharisha kwamba Gabon inaelekea kwenye vurumai na amesema njia ya kuepusha hatari hiyo ni kuheshimu matokeo ya kweli ya uchaguzi.Kiongozi huyo wa upinzani ameitaka jumuiya ya kimataifa iingilie kati.

Matokeo kutobadilishwa

Hali katika mji mkuu wa Libreville.

Hali katika mji mkuu wa Libreville.

Lakini wachunguzi wamesema jambo hilo halitawezekana na pia wamesema hakuna uwezekano wa wananchi kuanzisha vuguvugu la kumwondoa Bongo madarakani.

Mkurugenzi wa utafiti wa masuala ya kiuchumi barani Afrika Francois Conradie amesema matokeo ya uchaguzi hayatabadilishwa.Lakini ameeleza kuwa Rais Bongo amepoteza uhalali na kwamba katika muhula wake ujao atakabiliwa na upinzani utakaotokana na harakati za jumuiya za wafanyakazi.

Tume ya uchaguzi ilimtangaza Rais Ali Bongo kuwa mshindi kwa kupata asilimia 49,85 ya kura. Mpinzani wake Jean Ping alipata asilimia 48.16.

Ali Bongo alichaguliwa kuutumikia muhula wa kwanza mnamo mwaka wa 2009, baada ya baba yake Omar Bongo kufariki.Omar Bongo alitawala kuanzia mwaka wa 1967.

Kuibuka kwa ghasia

Makao makuu ya chama cha upinzani katika mji mkuu wa Libreville.

Makao makuu ya chama cha upinzani katika mji mkuu wa Libreville.

Machafuko yalizuka baada ya wafuasi wa Jean Ping kujitokeza barabarani na kuandamana. Kwa mujibu wa habari watu watano wamekufa kutokana na ghasia hizo.Kiongozi wa upinzani Jean Ping amesema watu hao wamejitokeza kupigania haki zao.

Ameeleza kwamba kila mara, watu wa Gabon wanapopiga kura ya kumchagua kiongozi wanaomtaka "yanajikusanya mawingu ya balaa" na kumleta yule ambae hatakiwi na wananchi.Hata hivyo ameahidi kwamba safari hii mambo yatakuwa tofauti.

Wajumbe wa Umoja wa Ulaya wameukosoa utaratibu wa uchaguzi wa nchini Gabon kwa kusema kwamba haukuwa wa uwazi.

Ufaransa kutoingilia Gabon

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Marc Ayrault.

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Marc Ayrault.

Wakati huo huo wanachama 27 wa upinzani waliokuwa wanazuiliwa na polisi wameachiwa.

Msemaji wa serikali ya Gabon alieleza kuwa watu hao waliruhusiwa kwenda makwao.Lakini mwakilishi wa wapinzani Paul -Marie Gondjout alidai kwamba polisi waliwatenganisha wafuasi wao .

Kwa mujibu wa habari polisi walilishambulia jengo la makao makuu ya upinzani na kuwaua watu wawili Alhamisi iliyopita.

Ghasia ziliendelea ambapo watu walipora maduka ,kuchoma moto majumba na pia kupambana na maafisa wa usalama.

Rais Bongo amewalaumu wapinzani kwa kuchochea ghasia.

Juu ya matukio ya nchini Gabon Waziri wa mambo yanje wa Ufaransa Jean-Marc Ayrault amesema enzi za Ufaransa za kujiingiza katika mambo ya ndani ya nchi za Afrika sasa zimeshapita.Akizungumza katika mahojiano na Televisheni ya Ufaransa ya France 2, Waziri Ayrult alisema kwamba Ufaransa ni mshirika wa Afrika lakini haitaki kujiingiza kwa namna yoyote katika masuala ya ndani ya nchi za bara hilo.

Mwandishi:Mtullya Abdu/rtre/afp/dpae

Mhariri:Mohamed Dahman