1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa Scotland Sturgeon atangaza kujiuzulu

Bruce Amani
15 Februari 2023

Waziri kiongozi wa Scotland Nicola Sturgeon ametangaza nia yake ya kujiuzulu wadhifa huo baada ya miaka minane ya kuongoza serikali yake ya ugatuzi. Sturgeon amesema ni muda muafaka kwake kuondoka

https://p.dw.com/p/4NWBl
PK  Nicola Sturgeon
Picha: Jane Barlow/AFP

Kiongozi huyo wa chama kikubwa kabisa cha Scottish National - SNP amesema kuwa katika kichwa chake na moyoni mwake, anafahamu kuwa ni wakati mwafaka wa kuondoka, baada ya kukaribia muongo mmoja madarakani akishinikiza uhuru wa Scotland.

Sturgeon mwenye umri wa miaka 52 amethibitisha kuwa atasalia kuwa waziri kiongozi hadi pale chama cha SNP kitamchangua kiongozi mpya. Pia atabakia kuwa mjumbe wa Bunge la Scotland hadi angalau uchaguzi ujao, unoapangwa mwaka wa 2026.

Sturgeon anaondoka baada ya kukabiliwa na shinikizo kuhusu mbinu zake za uhuru na kuhusu haki za watu waliobadili jinsia. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Edinburgh, amesema, uamuzi huo hauhusiani kwa namna yoyote na masuala yaliyojitokeza hivi karibuni, bali anauchukua baada ya kujitathmini kwa muda mrefu.