Kimetto avunja rekodi ya Berlin marathon | Michezo | DW | 30.09.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Kimetto avunja rekodi ya Berlin marathon

Mkenya Dennis Kimetto ameshinda awamu ya 41 ya mbio za Berlin Marathon kwa kutumia saa 2 dakika 2 na sekunde 57, akiwa mkimbiaji wa kwanza kumaliza mbio hizo chini ya saa mbili , na dakika 3.

Rekodi ya awali ya saa 2, dakika 3 na sekunde 23 iliwekwa na Mkenya pia , Wilson Kipsang mjini Berlin mwaka jana. "Najisikia vizuri kwasababu nimeweka rekodi mpya ya dunia. Nafurahi sana." Amesema hivyo Kimetto mshindi wa mbio hizo za Marathon mjini Berlin alipoulizwa na waandishi habari kuhusu hisia zake katika ushindi wa mbio hizo. Na akaongeza "mashabiki walinifanya nijiamini na nilifikiri kwamba naweza kushinda."

Mshindi wa pili Emmanuel Mutai pia amevunja rekodi ya zamani akimaliza kwa saa 2 dakika 3 na sekunde 13 na anaamini inawezekana kukimbia marathon kwa chini ya saa mbili.

41. Berlin Marathon 28. Sept. 2014 Matebo Kebede

Wanariadha katika mbio za Marathon mjini Berlin

"Kutokana na kile nilichokiona leo, muda unapungua zaidi na zaidi. Kwa hiyo kama sio leo, inawezekana kesho," Mutai mwenye umri wa miaka 29 amesema. Huenda mara nyingine tunaweza kupata saa 2, dakika moja."

Pia amesema. "Mbio zilikuwa ngumu tangu mwanzo. Lakini mwanzoni kasi ilikuwa chini ,mno. Kwa hiyo baada ya kufikia nusu ya mbio hizo tulijaribu kuongeza kasi na kwamba mwishoni tuliweza kupata matokeo mazuri. Mara nyingine natumai naweza kuwa mshindi wa kwanza".

Mutai amekimbia marathon hii kwa kasi zaidi katika historia kwa kutumia saa 2, dakika 3 na sekunde 2 mjini Boston mwaka 2011, licha ya kuwa haikuhesabiwa kuwa ni rekodi ya dunia kwasababu njia ya mbio hizo ilifikiriwa kuwa imenyooka sana na yenye mteremko.

Katika mbio za jana mjini Berlin Mutai aliweka rekodi ya dunia kwa kukimbia kilometa 30 kwa saa 1, dakika 27 na sekunde 37, akiipiku rekodi ya Patrick Makau ya hapo awali ya saa 1, dakika 27 na sekunde 38 ya mwaka 2011.

Abera Kuma wa Ethiopia alikuwa wa tatu katika mbio hizo akiwa mbele ya Wakenya Geofrey Kamworor na Eliud Kiptanui.

Tirfi Tsegaye kutoka Ethiopia ameshinda mbio hizo kwa upande wa wanawake kwa kutumia saa 2, dakika 20 na sekunde 18 , huku mkimbiaji mwingine kutoka Ethiopia Feyse Tadese akishika nafasi ya pili.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / dpae / rtre , ZR
Mhariri: Iddi Ssessanga