1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kimbunga Patricia chashambulia Mexico

24 Oktoba 2015

Kimbunga kikali kabisa Patricia kimeikumba pwani ya Mexico jana Ijumaa(23.10.2015),kiking'oa miti na kusababisha mvua kubwa na kuzusha hofu kwamba upepo mkali unaoambatana na kimbunga hicho utaacha uharibifu mkubwa.

https://p.dw.com/p/1GtVe
Mexiko Hurrikan Patricia Evakuierung
Watalii wakiondolewa kutoka katika hoteli katika fukwe za MexicoPicha: Reuters/H. Romero

Maafisa wamewahamisha wakaazi wa maeneo ya pwani, wamewaondoa watalii kutoka katika hoteli wazizofikia katika fukwe za nchi hiyo, kufunga bandari za eneo hilo, viwanja vya ndege na shule katika majimbo kadhaa kabla ya kimbunga kilichopewa kiwango cha tano kufika katika jimbo la magharibi la Jalisco.

Mkurugenzi wa mamlaka ya taifa ya maji Roberto Ramirez ameiambia televisheni ya Milenio kuwa kimbunga hicho kiliwasili pwani katika mji wa Emiliano Zapata, kiasi ya kilometa 95 magharibi ya bandari muhimu ya Manzanillo.

Mexiko Hurrikan Patricia Evakuierung
Wakaazi wa maeneo yaliyokumbwa na kimbunga Patricia wakipewa hifadhiPicha: Reuters/H. Romero

Kimbunga Patricia kimepungua kasi

Kituo cha taifa cha Marekani kinachohusika na masuala ya vimbunga kimesema kimbunga Patricia kimedhoofika kwa kiasi kikubwa kilipotua usiku, kikiwa na kasi ya upepo ya kilometa 270 kwa saa ambacho kilipungua hadi kilometa 260 kwa saa wakati kimbunga hicho kilipoingia zaidi ndani ya nchi hiyo.

Kimbunga Patricia kilichokuwa katika kasi ya kilometa 325 kwa saa masaa kadhaa hapo kabla kikiwa na nguvu zaidi kuliko kasi ya kimbunga kikali Haiyan ya kilometa 315, ambacho kilisababisha zaidi ya watu 7,350 kuuwawa ama kupotea wakati kilipolikumba taifa la Ufilipino Novemba mwaka 2013.

Mvua na upepo umelikumba eneo la pwani masaa kadhaa baada ya Patricia kujikusanya jioni ya Alhamis kuwa kimbunga cha kiwango cha tano; kiwango cha juu cha kipimo cha Saffir-Simpson.

Mexiko Hurrikan Patricia Satellitenbild
Picha za satalaiti zinazoonesha kimbunga PatriciaPicha: Reuters/NASA/Handout via Reuters

Miti yang'olewa

"Tunakabiliwa na maafa ya asili, nguvu ambayo hatujawahi kuiona kabla duniani", Rais Enrique Pena Nieto aliiambia radio Formula mapema siku hiyo. "tunakabiliwa na wakati mgumu sana." Hata hivyo hakukuwa na ripoti mara moja za maafa.

Katika jimbo la Colima ambako mji wa Manzanillo upo, kiasi ya miti 350 imeng'olewa kutoka ardhini "lakini kwa bahati nzuri hakuna uharibifu wa mali," waziri wa kilimo Jose Calzada ameiambia televisheni ya Milenio.

Maduka yamefungwa katika mji wa kitalii wa Puetro Vallarta, upande wa kaskazini zaidi ya kule kimbunga Patricia kilipoingilia, na wenye maduka wamefunga maduka yao wameweka vizuwizi katika madirisha ya maduka yao kwa ajili ya usalama.

Kiasi ya raia 7,000 wa kigeni na watalii 21,000 raia wa Mexico walikuwa mjini Puerto Vallarta kabla ya kimbunga hicho kuwasili.

Mexiko Hurrikan Patricia Satellitenbild
Picha za satalaiti zikionesha njia ya kimbunga PatriciaPicha: picture-alliance/dpa/NOAA

Hoteli zilizoko ufukweni mwa bahari hazina watu na wataalii kadhaa waliondolewa haraka kwenda katika maeneo salama, viwanja vya ndege na vituo vya mabasi.

Maafisa wa serikali wamesema watu 3,500 wameondolewa kutoka Puerto Vallarta kwa mabasi na ndege.

Eneo lililotayarishwa na shirika la msalaba mwekundu limegeuka kuwa hifadhi ya watu 109 mjini Puerto Vallarta, ikiwa ni pamoja na Wamarekani, Wacanada na Wataliano.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Caro Robi.