Kimbunga Favio chaikumba Msumbiji | Masuala ya Jamii | DW | 22.02.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Kimbunga Favio chaikumba Msumbiji

Kimbunga kilicho andamana na upepo mkali unaovuma kwa kasi ya kilomita 230 kwa saa kilivamia eneo la kati la Msumbiji na kusababisha uharibifu.

Picha iliyopigwa kutoka angani ya pwani ya Msumbiji

Picha iliyopigwa kutoka angani ya pwani ya Msumbiji

Kimbunga hicho kwa jina Favio kilivamia ufukweni mwa pwani ya Msumbiji na kung’oa miti pamoja na miti ya stima huku upepo mkali ukivuma na kusababisha mvua kubwa ambayo imeleta hali ya wasiwasi kwa raia wa Msumbiji.

Mamia ya familia za watu wa Msumbiji tayari wamo kwenye mashaka yaliyosababishwa na mafuriko makubwa ya hivi majuzi, wengi wao wakiwa wamelazimika kuyahama makaazi yao.

Kimbunga cha pili kwa jina Gamede kutoka pwani ya bahari Hindi katika eneo la kaskazini mashariki mwa Madagascar kinatazamiwa kuikumba pwani ya Msumbiji kesho afajiri.

Uharibifu wa leo uliosababishwa na kimbunga Favio katika eneo la Vilankulo kusini mwa bandari ya Beira ni pamoja na kuharibu makaazi ya watu au hata kung’olewa mapaa katika baadhi ya nyumba za watu.

Serikali ya Msumbiji tayari ilikuwa imeshawahamisha watu kutoka kwenye maeneo hayo na kuwapeleka katika sehemu za miinuko.

Watu wachache waliokuwa bado wamesalia katika eneo hilo walihangaika huku na kule kujaribu kuokoa mali zao kutoka kwenye majumba yao.

Katibu mkuu wa shirika la misaada la msalaba mwekundu nchini Msumbji Fernanda Teixeira amesema

Ni hali ya kusikitisha mno kuona kwamba watu wa Msumbiji bado wanapambana na athari za mafuriko na kabla hawajasau hayo kimbunga cha Flavio nacho kikaingia kati, amesema kuwa maafisa wa shirika lake bado wanakabiliana na harakati za kugawa misaada kwa familia zilizoathirika na mafuriko.

Watalaamu wa hali ya hewa wamesema kwamba masalio ya kimbunga cha Favio yatasabisha mvua kubwa zinazotazamiwa kufika katika nchi za Zambia, Malawi na Zimbabwe na kuendelea kuujaza maji mto Zambezi.

Msumbiji ilikumbwa na vimbunga mfululizo katika miaka ya 2000 na 2001 vilivyo sambaza mafuriko katika maeneo ya kati na kusini mwa nchi hiyo.

Takriban watu 700 waliuwawa na kusababisha takriban watu wengine nusu milioni kuyakimbia makaazi yao.

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com