Kikosi cha OSCE Ukraine kuimarishwa | Matukio ya Kisiasa | DW | 13.03.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Kikosi cha OSCE Ukraine kuimarishwa

Shirika la Usalama na Ushirikiano la Ulaya (OSCE) limepiga kura ya kuongeza maradufu ukubwa wa kikosi cha uangalizi Ukraine kufikia 1,000 pia kuongeza muda wa kikosi hicho kubakia nchini humo kwa miezi mengine 12.

Mkuu wa Kikosi cha Uangalizi cha OSCE nchini Ukraine Ertugrul.

Mkuu wa Kikosi cha Uangalizi cha OSCE nchini Ukraine Ertugrul.

Uamuzi huo umeungwa mkono na nchi zote 57 wanachama wa shirika hilo la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya ikiwemo Urusi na Ukraine wakati wa kikao kilichofanyika makao makuu ya shirika hilo mjini Vienna, Austria hapo jana.

Shirika hilo la masuala ya usalama lilikuwa limeweka takriban waangalizi wa kiraia 470 wasiokuwa na silaha nchini Ukraine ambao wanayakinisha kuheshimiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano na kuondolewa kwa silaha nzito kati ya vikosi vya serikali na waasi wanaoegemea upande wa Urusi mashariki mwa Ukraine.

Mamlaka mpya ya shughuli za shirika hilo muda wake sasa utamalizika mwishoni mwa mwezi wa Machi mwaka 2016. Nchi nyingi za Ulaya zinataraji kwamba kuimarishwa kwa kikosi hicho kunaongeza fursa ya kutekelezwa kwa makubaliano tete ya usitishaji wa mapigano mashariki ya Ukraine.

Kuimarisha kikosi cha sasa cha OSCE

Mkuu wa Kikosi cha Uangalizi cha OSCE nchini Ukraine Ertugrul.

Msafara wa kikosi cha serikali ukiondoka mashariki mwa Ukraione.

Hata hivyo wanadiplomasia mjini Vienna wamesisitiza kwamba waangalizi hao zaidi hawatojiunga na kikosi hicho hivi karibuni kutokana na kwamba kipaumbele cha sasa cha shirika hilo la usalama na ushirikiano barani Ulaya (OSCE) ni kuimarisha kikosi kilichopo.

Katika kipindi cha wiki moja iliopita waangalizi wameshuhudia kuondolewa kwa silaha nzito kutoka eneo la mapambano na kupunguwa kwa ukiukaji wa kusitisha mapigano wenye kuhusisha silaha hizo nzito. Hata hivyo Alexander Hug naibu mkuu wa kikosi cha waangalizi cha shirila la OSCE amelalamika mjini Kiev kwamba waangalizi hao bado wanashindwa kuyakinisha kuondolewa kwa silaha hizo nzito.

Akizungumza katika kikao cha Baraza la Usalama na Ulinzi wa Taifa mjini Kiev hapo Ahamisi Rais Petro Poroshenko wa Ukraine amesema serikali yake imejitolea kuheshimu makubaliano ya amani ya Minsk yaliofikiwa hivi karibuni lakini ameongeza kusema kwamba usitishaji wa mapigano haumaanishi kwamba hawatofyatuwa risasi kujibu mapigo.

Rais Petro Poroshenko wa Ukraine.

Rais Petro Poroshenko wa Ukraine.

Poroshenko amekaririwa akisema "Vikosi vya kijeshi vimepatiwa amri, haki na majukumu na viko tayari kujihami wakati vitakaposhambuliwa."

Ruhusa zaidi kwa OSCE

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier akiwa ziarani nchini Marekani amesisitiza kwamba shirika hilo la OSCE linatakiwa lipatiwe ruhusa kamili kuweza kuyakinisha kuondolewa kwa silaha nzito kwenye maeneo ya vita.

Kikosi cha shirika hilo mara kwa mara kimekuwa kikilalamika kwamba kimekuwa kikizuiliwa kukaguwa maeneo ya silaha na pande zote mbili.

Mjumbe wa Ukraine kwa shirika hilo Ihor Prokopchuk naye amesisitiza wito wa serikali yake wa pia kuundwa kwa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Ukraine ikiwa ni ziada ya waangalizi hao wa OSCE wasiokuwa na silaha.

Kwa muijibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa takriban watu 6,000 wameuwawa tokea kuzuka kwa mzozo huo wa Ukraine hapo mwezi wa Aprili mwaka 2014.

Mwandishi : Mohamed Dahman/dpa

Mhariri: Daniel Gakuba

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com