1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya ya kwanza kwa medali mjini Beijing

Admin.WagnerD31 Agosti 2015

Rais Uhuru Kenyatta awapongeza wanariadha wa Kenya walionyakua ubingwa wa dunia katika michezo ya riadha ya dunia huko mjini Bejing kwa kunyakua medali 16 , saba kati ya hizo za dhahabu.

https://p.dw.com/p/1GOfQ
China Sperrwerfer Julius Yego aus Kenia
Julius Yegokutoka Kenya bingwa wa kurusha mkukiPicha: picture-alliance/AP Photo/M. Schiefelbein

Rais Uhuru Kenyatta amewapongeza wanariadha wa Kenya kwa ushindi wao katika mashindano ya dunia ya riadha mjini Beijing ambako kenya imeshinda taji hilo la dunia kwa mara ya kwanza. Kenya imejipatia jumla ya medali 16 , ikiwa ni pamoja na medali saba za dhahabu , na kuvipiku vigogo , kama Jamaica na Marekani katika nafasi ya pili na ya tatu.

China, Vivian Jepkemoi Cheruiyot Leichtathletik WM
Vivian Jepkemoi Cheruiyot bingwa wa mita 10,000 dunianiPicha: picture-alliance/dpa/S. Suki

"Vijana wetu kwa mara nyingine tena wameonesha kwamba wanaweza kufanya vizuri kama wachezaji bora dunia, " amesema Uhuru Kenyatta katika taarifa kwa vyombo vya habari.

Amehimiza kuimarishwa kwa mpango wa taifa wa maendeleo ya vijana, kuwapa uwezo vijana wengi wa Kenya ili kuifanya Kenya kuweza kushindana vizuri zaidi katika mashindano ya kimataifa.

Kenya ambayo imekuwa ikitamalaki katika mbio za masafa mafupi na marefu, imepata ushindi adimu katika mbio za mita 400 kuruka viunzi na kurusha mkuki mjini Beijing kwa mara ya kwanza.

Kenia Präsident Uhuru Kenyatta in Nairobi
Rais Uhuru Kenyatta amewapongeza wachezaji wa Kenya kwa kunyakua medali nyingi BejingPicha: Reuters/T. Mukoya

Asbel Kiprop ameshinda mbio za mita 1,500 kwa mara ya tatu na kunyakua dhahabu na kuihakikishia Kenya kuwa juu ya nchi zilizonyakua dhahabu nyingi katika fainali ya mbio hizo jana Jumapili..

Rais wa chama cha riadha nchini Kenya Isaiah Kiplagat , amesema mafanikio hayo yametokana na mipango mizuri katika chama chake.

Kikosi cha wanariadha wanaume wa marekani kimeshinda dhahabu kwa mara ya nne mfululizo katika mbio za mita 400 mara 4 , lakini Mjamaica Novlene Williams-Mills aliweza kukata mbuga na kutokezea wa mwanzo katika mbio kama hizo kwa wanawake akiwashinda wanawake wa Marekani na kujinyakulia medali ya sita ya dhahabu mjini Beijing kwa kikosi cha vigogo hao kutoka katika visiwa vya karibiki.

China Leichtathletik WM in Peking - Männer 1500m - Asbel Kiprop
Bingwa wa mita 1,500 mjini Beijing Asbel KipropPicha: Getty Images/A. Lyons

Kiprop , Usain Bolt na msichana wa Jamaica Shelly Ann Fraser - Pryce ni wanariadha pekee walioshinda katika michezo ya Olimpiki mjini Beijing ambao wamerejea mjini humo na kushinda medali za dhahabu katika ubingwa wa dunia miaka saba baadaye.

Doping ni tatizo

Hata hivyo mashindano yenye kusisimua mjini Beijing yameshindwa kunyamazisha minong'ono ya maswali juu ya matumizi ya madawa ya kuongeza nguvu, doping, na kumpa mkuu mpya wa shirikisho la riadha duniani Sebastian Coe muda wa kutafakari wakati akielekea katika mwaka wa mashindano ya Olimpiki mjini Rio de Janeiro mwakani.

15. Leichtathletik-Weltmeisterschaft in Peking 2015 Usain Bolt
Usain Bolt wa JamaicaPicha: Reuters/D. Gray

Wakati mkimbiaji Usain Bolt aliongoza kundi la mastaa katika uwanja wa kiota cha ndege mjini Beijing, watu wenye shaka pia haikuwa vigumu kuwapata kufuatia madai ya matumizi makubwa ya madawa hayo kwa wanariadha maarufu.

Swali hilo nilimtupia pia rais wa chama cha riadha nchini Kenya Isaiah Kiplagat, ambapo Kenya imekumbwa hivi karibuni na madai kama hayo kwa wanariadha wake. Alikuwa na haya ya kusema.

Großbritannien Sebastian Coe Politiker
Sebastian Coe mkuu wa shirikisho la vyama vya riadha duniani IAAFPicha: Reuters/Action Images/M. Childs Livepic

Bundesliga : Borussia kileleni

Kwa upande wa kandanda, Bundesliga imekamilisha mchezo wake wa tatu jana , ambapo Borussia Dortmund imefanikiwa kwa mara ya tatu kupata ushindi msimu huu na kukalia usukani wa ligi baada ya kuishinda kirahisi Hertha Berlin kwa mabao 3-1.

Shinji Kagawa alionesha kurudi katika hali yake bora baada ya kupanga njia ya mabao mawili ambapo Borussia Dortmund iliweza kufikisha pointi tisa , ikiwa pamoja na mabingwa Bayern Munich , zikitofautiana kwa magoli.Kocha wa Borussia Dortmund Thomas Tuchel amesema amefurahishwa sana na mchezo huo.

Deutschland Fußball Bundesliga 3. Spieltag Borussia Dortmund - Hertha BSC
Borussia Dortmund wakiandika bao katika mchezo dhidi ya Hertha BerlinPicha: picture-alliance/dpa/B. Thissen

"Nimefurahishwa sana na mchezo huu. Vile tulivyofanikisha, na jinsi gani tulivyochukua tahadhari. Tumeweza leo kujitokeza, na mwishoni lakini ilibidi tulionesha jinsi tunavyoweza kulinda lango letu na kuonesha kwamba tunaweza kuweka upinzani. Pia tumeonesha jinsi tunavyofurahia kucheza kandanda. Mambo haya mawili yanakwenda sambamba. Ndio sababu nina furaha sana, kuona tunavyoweza kufanya kila mara uwanjani."

Bayern ilionekana kuwa moto wa kuotea kwa mbali, pale walipoishinda Bayer Leverkusen kwa mabao 3-0 siku ya Jumamosi ambapo thomas Mueller alipachika mabao 2.

Deutschland Fußball Bundesliga Bayern München - Bayer Leverkusen
Bayern Munich moto wa kuotea kwa mbaliPicha: Getty Images/Bongarts/M. Hangst

Hamburg SV ambayo iliugua msimu uliopita na kukaribia kushuka daraja ilipata kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya FC Koln, kipigo ambacho kocha Bruno Labbadia wa Hamburg amesema hakikustahili.

"Nafikiri kuhusu kipigo hicho cha mabao 2-1 hatupaswi kusema kitu. Yalikuwa makosa makubwa ya mwamuzi. Kila mmoja ameona. Inatia uchungu sana, kwasababu ni udanganyifu mkubwa. Tulipaswa kushinda. Tumefadhaishwa mno, na jinsi tulivyoshindwa, kwasababu nahisi, kwamba mchezo huu ungemalizika kwa sare."

Borussia Moenchengaldbach imeendelea kufanya vibaya mwanzoni mwa msimu huu. Licha ya kuwa msimu bado mchanga, lakini kipigo mfululizo katika michezo mitatu, inaashiria hali mbaya na taa nyekundu inawaka kwa kocha Lucien Favre.

Deutschland Fußball Bundesliga 3. Spieltag Werder Bremen gegen Borussia Mönchengladbach
Werder Bremen yaandika ushindi wa kwanza dhidi ya MoenchengladbachPicha: Getty Images/Bongarts/S. Franklin

Timu hiyo inayoshiriki katika michuano ya Champions League msimu huu , inakabiliwa na matatizo kadhaa upande wa ulinzi na ushambuliaji, baada ya kuondoka wachezaji muhimu kama Kruse aliyetimkia kwa makamu bingwa Wolfsburg na mchezaji wa kati Kramer aliyeko katika kiksi cha Bayer Leverkusen.

Borussia Moenchengladbach imepokea jana Jumapili kipigo cha mabao 2-1 mbele ya werder Bremen ambayo nayo imepata ushindi wake wa kwanza msimu huu na kujihakikishia pointi tatu.

Deutschland Fußball Bundesliga 3. Spieltag Werder Bremen gegen Borussia Mönchengladbach
Lucien Favre kocha wa MoenchengladbachPicha: Getty Images/Bongarts/S. Franklin

Premeir League : Vigogo hoi

Katika Premier League: mshambuliaji wa pembeni Raheem Sterling alipachika bao lake la kwanza akivalia sare ya Manchester City wakati kikosi hicho cha kocha Pellegrini kikipata ushindi mfululizo katika michezo yake mitatu, baada ya kuishinda Watford kwa mabao 2-0.

Chelsea iliangukia pua ikiwa nyumbani Stamford Bridge baada ya kipigo kutoka Crystal Palace cha mabao 2-1, Manchester United nayo haikusalimika baada ya kuchezea kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Swansea City na Liverpool iligaragazwa kwa kufungwa mabao 3-0 dhidi ya West Ham United. Arsenal ilipata ushindi baada ya kibarua kigumu dhidi ya Newcastle United na kuambulia ushindi wa bao 1-0.

Fifa WM 2014 Uruguay England
Raheem Sterling wa Man City (kushoto)Picha: Reuters

Dirisha la uhamisho lafungwa

Leo (31.08.2015) ni siku ya mwisho kwa dirisha la uhamisho kufungwa. Timu mbali mbali zinafanya matayarisho ya mwisho ili kuwapata wachezaji wanaowahitaji, ambapo mshambuliaji wa Wolfsburg Ivan Perisic anahamia rasmi Inter Milan , Fabio Borini wa Liverpool anaelekea Sunderland ambapo mshambuliaji huyo wa Italia anaelekea kukamilisha mambo ya lazima kama uchunguzi wa afya na masuala mengine.

Lakini nahodha wa Southampton Jose Fonte amesema kuwa timu hiyo haipaswi kuwaachia wachezaji wake kuihama timu hiyo kabla ya dirisha kufungwa kesho Jumanne.

Mlinzi huyo pamoja na wachezaji wengi wamemtaka mchezaji wa kati Victor Wanyama kubakia kunduni, wakati mchezaji huyo kutoka Kenya ametoa maombi yaliyokataliwa ya kutaka kuhamia Tottenham Hotspurs, na pia timu hiyo imeshangazwa na maombi ya Manchester United kumtaka mshambuliaji wao Sadio mane.

Mchezaji wa kati wa Brazil Casemiro amerefusha mkataba wake na vigogo wa Uhispania Real Madrid hadi mwaka 2021, wakati kitita cha euro milioni 79.8 kilicholipwa na Manchester City kumpata mchezaji wa kati wa Wolfsburg Kevin de Bruyne , kimeleta wasi wasi katika Bundesliga kwamba wachezaji nyota wanavutika kuhamia Uingereza.

Fußball Bundesliga - Borussia Dortmund - FC Schalke
Julian Draxler kutoka Schalke 04 kwenda WolfsburgPicha: Getty Images

Mshambuliaji wa Monaco Anthony Martial mwenye umri wa miaka 19 anafanya mazungumzo na Manchester United na amesafiri kwenda nchini Uingereza kwa ajili ya kutia saini mkataba na timu hiyo.

Nayo Wolfsburg ya Ujerumani inafanya mipango ya kumpata mchezaji wa kati wa Schalke 04 Julian Draxler , kwa mujibu wa duru za shirika la habari la Ujerumani dpa , pande zote mbili zimekubaliana , lakini uhamisho bado haujakamilika.

Wakati huo huo Senegal itapambana na Afrika kusini katika mpambano wa kila mwaka wa kuwania kombe la Mandela Septemba 8, kwa mujibu wa taarifa ya shirikisho la kandanda la Afrika kusini iliyotolewa leo.

Mwandishi : Sekione Kitojo / dpa / afpe / rtre

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman