Kashfa nyengine ya kughoshi shahada ya uzamivu | Magazetini | DW | 15.10.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Kashfa nyengine ya kughoshi shahada ya uzamivu

Matamshi ya spika wa bunge la Ujerumani ,kisa cha kughoshi shahada ya uzamivu,na binaadam wa kwanza kuchupa kilomita 39 toka anga za juu hadi ardhinini ndizo mada kuu magazetini.

Spika wa bunge la Ujerumani Norbert Lammert

Spika wa bunge la Ujerumani Norbert Lammert"

Tunaanzia Berlin ambako matamshi ya spika wa bunge la Ujerumani Norbert Lammert dhidi ya kupanuliwa zaidi Umoja wa Ulaya yamezusha fadhaa.Gazeti la "Märkische Oderzeitung) linaandika:

Kati kati ya furaha baada ya Umoja wa Ulaya kuchaguliwa kuwa mshindi wa zawadi ya amani ya Nobel,spika wa bunge la Ujerumani anadai mipango ya kupanuliwa Umoja wa Ulaya isitishwe angalao kwa sasa.Nobert Lammert,hakutafuta mfano mzuri ,kwa kuitaja Kroatia.Kwa sababu ,kile ambacho hajakitaja ni kwamba kujiunga nchi hiyo na Umoja wa Ulaya July mwaka 2013 ni jambo ambalo limeshakubaliwa.Ni kweli kabisa kwamba,ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Ulaya kuhusu maendeleo yaliyopatikana imeweka wazi kabisa kwamba nchi hiyo bado ina walakin.Hata hivyo lawama za Lammert si za haki ikiwa zinawatwika wakroatia milioni nne makosa yanayodhihirika kufanywa na Umoja wa Ulaya.Kuakhirishwa mpango wa kujiunga Kroatia na Umoja wa Ulaya itakuwa sawa na kukorofisha juhudi zote za Umoja wa Ulaya za kusimamia utulivu katika eneo la Balkan.

Annette Schavan Dissertation Doktorarbeit Plagiat

Waziri wa elimu Annette Schavan

Mada nyengine iliyohodhi magazeti ya Ujerumani hii leo inahusu kisa chengine cha kughoshi shahada ya uzamivu.Safari hii anaetuhumiwa kuhusika na kisa hicho ni waziri wa elimu bibi Annette Schavan.Gazeti la "Nordwest-Zeitung" linaandika:

Kansela Merkel hana bahati na mawaziri wenye shahada za uzamivu.Kwamba waziri wa zamani wa ulinzi Karl-Theodor zu Guttenberg amepokonywa sio tu shahada ya uzamifu na kulazimika kujiuzulu serikalini baada ya kudhihirika kwamba kweli amefanya udanganyifu wakati wa mtihani wake wa mwisho wa chuo kikuu,chanzo alikuwa mwenzake-waziri wa elimu Annette Schavan.Lawama zake ndizo zilizomfanya zu Guttenberg asiwe na njia nyengine isipokuwa kujiuzulu.Ni kiroja kikubwa hiki kwamba leo hii ni mwanasiasa huyu huyu wa kutoka jimbo la Baden-Württenberg- anaesifiwa kama mtu mwenye kufuata maadili-kwamba yeye ndie anaekumbwa na kisa hiki hivi sasa.Ikidhihirika kama kweli,basi rafiki huyo mkubwa wa Merkel hatokuwa na njia nyengine isipokuwa kulipa kisogo jukwaa la kisiasa.

Red Bull Stratos - Felix Baumgartner

Felix Baumgartner akichupa kutoka kilomita 39 juu hadi ardhini

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu kisa cha ujasiri ambacho hakijawahi kushuhudiwa hadi sasa ulimwenguni.Gazeti la" Neue Osnabrücker Zeitung" linaandika:

Bila ya wavumbuzi mfano wa Marco Polo,Kolombus na wengineo kama hao,dunia yetu isingekuwa hivi ilivyo.Felix Baumgartner,ingawa hakufanya uvumbuzi wa ajabu,lakini amefanya jambo la hatari ambalo hakuna aliyewahi kulifanya kabla yake.Inawezekana pengine kwamba kitendo chake cha kijasiri cha kuchupa kutoka angani kitawasaidia wachunguzi wa masuala ya tiba na wataalam wa anga za juu.Lakini hata bila ya faida hizo,alichokifanya ni ujasiri wa hali ya juu.Mamilioni ya watu walijionea moja kwa moja kwa njia ya televisheni jinsi Felix Baumgartner alivyokuwa akichupa kutoka kilomita 39 angani hadi ardhini.Zilikuwa hisia sawa na pale mtu wa kwanza alipoteremka mwezini.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

MhaririMohammed Abdul-Rahman